Sunday, 31 August 2014

JIJI LA DAR HALITAKI TANGANYIKA

WANANCHI wa Dar es Salaam wanapendelea zaidi Muungano wa Serikali Moja kuliko wananchi wengine wa Tanzania Bara na Zanzibar, imefahamika.
Mara ya kwanza utafiti kufanyika kwa njia ya simu za mkononi
Mara ya kwanza utafiti kufanyika kwa njia ya simu za mkononi barani Afrika
Kwa mujibu wa utafiti wa karibuni zaidi maarufu kwa jina la Sikiliza Dar uliofanyika Juni mwaka huu, nne kati ya kumi ya wananchi wa Dar es Salaam walionyesha kupendelea zaidi mfumo wa serikali moja kuliko maeneo mengine yote ya Tanzania.

Katika utafiti wa Sauti za Wananchi uliofanyika Februari mwaka huu na kuhoji kaya za Tanzania Bara na ule wa Wasemavyo Wazanzibari uliofanyika wakati huo kuhoji kaya za Zanzibar, majibu yalikuwa chini ya yale ya Dar es Salaam.

Kwenye tafiti zilizofanyika Februari, asilimia 28 ya wananchi wa Tanzania Bara walionyesha kupendezwa na mfumo wa serikali moja wakati asilimia mbili tu ya Wazanzibari walionyesha kupendelea mfumo wa huo wa serikali moja.

Wananchi wa Dar es Salaam kupitia Sikiliza Dar pia wameonyesha tofauti baina yao na wenzao wa Tanzania Bara na Zanzibar kwa kuwa wachache wanaohitaji kuwepo kwa mfumo wa serikali tatu.

Kwa mfano, wakati utafiti wa Sauti za Wananchi ulionyesha kwamba asilimia 22 ya wananchi wa Bara walikuwa wanataka Muungano wa serikali tatu huku asilimia 46 ya Wazanzibari wakitaka mfumo huo pia; ni asilimia 20 tu ya wakazi wa Dar es Salaam waliohojiwa na utafiti huo ndiyo waliosema wanataka serikali tatu.

Tafiti zote hizi tatu za Bara, Zanzibar na Dar es Salaam hufanyika kwa njia ya mahojiano ya simu ambapo watu kutoka katika kaya (familia) tofauti hupigiwa simu na kuulizwa maswali kuhusiana na masuala anuai.

Tofauti na kawaida, katika utafiti wa safari hii wa Sikiliza Dar, maswali yaliyoulizwa yalikuwa sawa na yale yaliyoulizwa mwezi Februari kwa wenzao wa Bara na Zanzibar.

Katika eneo jingine, wananchi wa Dar es Salaam pia wameonyesha kutotaka kuendelea na Muungano kuliko wenzao hao wa Zanzibar na Bara –ambako asilimia saba ya wananchi waliohojiwa walisema wako tayari kuvunja mkutano.

Katika utafiti wa Sauti za Wananchi uliohoji kaya 1547 za Bara na Wasemavyo Wazanzibari uliohoji kaya 445, asilimia mbili za Visiwani na asilimia nne tu za Bara ndizo zilizounga mkono kuvunjika kwa Muungano.

Katika swali la iwapo wananchi wanataka mfumo uliopo sasa uendelee, Dar es Salaam walikuwa katikati ya Zanzibar na Bara, ambapo asilimia 16 walitaka mfumo uendelee, wakati Zanzibar ilikuwa asilimia tano na Bara iliongoza kwa kuwa na asilimia 25.

Utafiti wa Sikiliza Dar ni mradi unaotekelezwa na gazeti hili la Raia Mwema kwa kushirikiana na taasisi ya Ustawi wa Uchumi (Centre for Economic Prosperity).

Katika siku za nyuma utafiti huu ulikuwa ukifanywa na taasisi ya Twaweza ya Dar es Salaam ambayo bado inaendesha tafiti za Sauti za Wananchi na Sauti za Wazanzibari.

Tafiti hizi ni za kwanza barani Afrika kwa kufanywa kwa kutumia mtindo wa kupiga simu za mkononi.

Chanzo: Raia Mwema, Tanzania