|
Mwenyekiti wa Nec Jaji Mstaafu Damian Lubuva |
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imekubali kuahirisha upigiaji
Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa iliyopangwa kufanyika Aprili 30,
mwaka huu kutokana na kutokamilika kwa uandikishaji wa Daftrai la
kudumu la wapiga kura kwa kutumia teknolojia ya Biometric Voters
Registration (BVR).
Hatua hiyo inakuja baada ya kuwepo mfululizo wa
matamko na ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali wa demokrasia kwamba
zoezi hilo lisingewezekana kwa sasa hasa kutokana kusuasua kwa mwenendo
wa BVR.
Mwenyekiti wa Nec Jaji Mstaafu Damian Lubuva
aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuwa kazi ya
uboreshaji daftari la wapiga kura ni ya msingi kabla ya taratibu zote za
upigaji kura.
Jaji Lubuva aliyeonekana kuwa mpole zaidi, alisema
kwa uzoefu walioupata Njombe, zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu
la wapiga kura bado halijakamilika katika mkoa huo na mingine
iliyosalia.
“Hivyo tume haitaweza kuendelea na zoezi la
upigaji kura ya maoni na zoezi hilo lililotangazwa hapo awali kufanyika
Aprili 30, 2015 limeahirishwa hadi tarehe itakapotangazwa na Nec baada
ya kushauriana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar,” alisema Jaji Lubuva.
Kwa nyakati tofauti, vyama vya siasa, asasi za
kiraia, taasisi za kidini na wananchi wamekuwa wakiishauri Nec
kuahirisha Kura ya Maoni huku vyama vya siasa vikimtaka Rais Jakaya
Kikwete atii makubaliano yaliyofikiwa na Kituo cha Demokrasia (TCD)
mwaka jana ya kuahirisha zoezi hilo hadi baada ya Uchaguzi mkuu.
Jaji Lubuva alisema kuwa tume yake inaendelea
kuboresha daftari la wapiga kura nchi nzima ambapo wanatarajia
kukamilisha ifikapo Julai mwaka huu. Nec ilieleza kuwa baada ya kumaliza
uandikishaji mkoani Njombe watahamia mikoa ya Ruvuma, Lindi, Mtwara na
Iringa.
Chanzo: mwananchi.co.tz