Wednesday 24 September 2014

KIUMBE CHA AJABU KUIBUKA PEMBA





Katika hali isiyo ya kawaida huko maeneo ya bahari ya Shamiani (kwa Gombe) jimbo la kiwani mkoa wa kusini Pemba kumeibuka kiumbe kikubwa cha ajabu kutoka baharini ambacho kimepwewa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa baadhi ya wakaazi wa maeneo ya jirani na eneo hilo ambao wamefurika kwa wingi kwenda kuona kiumbe hicho wamesema kuwa ni mara ya kwanza kuona kiumbe cha namna hicho kikiwa kimepwewa ndani ya bahari.

Baadhi yao wameeleza kuwa huenda pengine kiumbe hicho cha ajabu chenye urefu takribani mita 40 na upana zaidi ya mita 25 kikawa ni samaki aina ya nyangumi au chongowe.

Katika hali ya kushangaza ndani ya fukwe hizo za bahari ya kwa Gombe watu zaidi ya 200 kutoka maeneo jirani ya Likoni,mwambe na ngambu shamiani wamejitokeza kuona kiumbe hicho cha ajabu ambacho tayari kimekufa.

Aidha makundi ya wananchi wanaendelea kukata minofu ya aina hiyo ya kiumbe huku wengine wakijaza madumu yao mafuta yanayotiririka kutoka kwa kiumbe hicho.

Kwa upande wake mtalamu wa viumbe vya bahari Zanzibar kwa masharti ya kutotajwa jina amesema msimu huu viumbe vya bahari aina ya nyangumi hupita katika ukanda wa bahari ya hindi.

“Inaonekana baadhi ya watu huwapiga viumbe vya bahari vya aina hii ndio maana hufariki dunia,hali hii inaitia nchi yetu jina baya kimataifa tunaonekana tunawaua kwa makusudi’’aliongezea mtaalamu huyo.

Alieleza kuwa kitengo chao kimeshatoa elimu sana ili wananchi waache tabia hii ya kuwaangamiza viumbe hawa kwani dunia haikubali kwa sasa kwa vile ni viumbe adimu na muhimu. 

Aidha alieleza alishauri wananchi wakiona kiumbe kama hicho kikiwa hai basi watoe taarifa kwa wahusika ili aweze kurudishwa baharini.

Hali hii ya kuonekana kiumbe cha ajabu ni mara ya kwanza kwa maeneo haya ambapo kumeibua mshangao.

Chanzo: WhatsApp

No comments:

Post a Comment