Tuesday, 16 September 2014

MBUNGE KEISSY AWAKERA WAZANZIBARI

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Ally Juma Khatibu akizungumza baada ya kukerwa na kauli za Mjumbe mwenzake, Ally Keissy, bungeni Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi 

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Ally Keissy jana alilazimika kusindikizwa na askari wa Bunge kuondoka katika viwanja vya eneo hili kumnusuru na hasira za wajumbe kutoka Zanzibar waliokerwa na mchango wake kuhusu masuala ya Muungano.

Kessy alisimama bungeni hapo saa 5:52 asubuhi kutoa mchango wake kuhusu Katiba akijikita zaidi katika suala la muundo wa Muungano na kusema kwamba Zanzibar inabebwa na Tanganyika.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanganyika inabeba mzigo mkubwa ambao haubebeki, hapa tunahudumia wabunge 83 kutoka Zanzibar ambao wanatibiwa wao na wake zao na watoto kwa gharama za Tanganyika wakati hawachangii,” alisema na kuongeza kuwa haiwezekani kwa Tanganyika kubeba mzigo mkubwa kama huo wakati katika Jimbo lake la Nkasi wananchi wanalia na shida ya maji.

Alisema katika Kamati yao Namba Moja, Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu alitoa semina iliyoonyesha kuwa Zanzibar haichangii chochote kwenye Muungano na kuwa hata mishahara wakati mwingine wanategemea Tanganyika.

Keissy alisema wananchi wakilijua jambo hilo, wataikataa Katiba inayopendekezwa na kuitupilia mbali kwa kuwa inatoa upendeleo kwa Wazanzibari na kuikandamiza Tanganyika.

“Mimi naweza kuwa na wanawake sita, nikazaa nao lakini kila mtoto anaendelea kutunzwa na baba yangu, jambo kama hili halivumiliki hata kidogo japo najua kuwa ukweli unawauma,” alisema huku baadhi ya wajumbe wakipaza sauti wengine kumpinga na wengine kuomba mwongozo wa mwenyekiti.

Alipinga suala la rais wa Zanzibar kuwa makamu wa rais wa Muungano kwa maelezo kuwa katika mfumo wa vyama vingi jambo kama hilo haliwezekani na kuhoji itakuwaje awe makamu wa kwanza wa rais wakati hajachaguliwa na wananchi wa Tanzania Bara?



Baada ya kauli hiyo, kelele za wajumbe kutoka Zanzibar ziliongezeka baadhi wakisimama na kuwasha vipaza sauti kumshambulia Keissy, “chizi huyo, chizi huyo, hafai kwanza ni Mwarabu,” zilisikika sauti huku nyingine zikimtaka aombe radhi.

Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta alimpa nafasi mmoja wa wajumbe hao, Fatuma Hamis Salehe kutoa taarifa, ndipo alisema wajumbe wa Zanzibar wapo kisheria ndani ya Bunge hilo na wala si kwa fadhila, hivyo akamtaka Keissy kuomba radhi.

Hata hivyo, Kessy alijibu akisema, “Siko tayari kuomba radhi katika jambo hili, mimi nazungumzia masuala ya Ndullu, alikuja pale katika kamati na kwamba tangu kifo cha Karume hamjawahi kuchangia, mnaposema mimi Mpemba au Mwarabu basi ninyi ni Wakongo,” alisema kwa sauti ya juu.

Alisema posho wanazolipwa bungeni hapo, zimetoka upande wa Tanganyika na Zanzibar haijachangia hata senti moja.

Baada ya hapo kelele ziliongezeka sawia na idadi ya waomba mwongozo, Mjumbe kutoka Kundi la 201, Ally Juma Khatibu, alisimama hata bila ya kupewa ruksa na kuanza kuzungumza kwa ukali akisema Kessy ni mbaguzi na mtu anayestahili adhabu kali.

Baadaye alipewa nafasi Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye aliwataka wajumbe kuwa wavumilivu na kupuuza baadhi ya mambo kwani kipindi kilichobakia ni cha kumalizia.

Alifuata Mjumbe, Mahmoud Thabit Kombo aliyesema Keissy hajui historia kwani Zanzibar ilipoteza utambulisho wake katika kiti cha Umoja wa Mataifa na kuiachia Tanzania, jambo ambalo nchi hiyo ndogo inastahili kupongezwa.

Mjumbe mwingine, Abdalla Sharia Ameir alimtuhumu Keissy kuwa ni mtu mwenye asili ya Arabuni ndiyo maana anapiga kelele kwa Waafrika na kutaka akapimwe akili.

Ameir alimtaka Keissy atoke nje kama ni mwanamume na hapo alianza kutangulia lakini alipoona hakuna wa kumfuata, alirudi hadi karibu na kiti alichokaa Keissy ndipo wajumbe wengine walipoingilia kuwatuliza.

Kwa upande wake, Hamad Rashid Mohamed alimwita Keissy mchochezi asiyejua historia ya Tanganyika na Zanzibar katika Muungano.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wassira alimtahadharisha Keissy kuwa mchango wake unaweza kuzua vita na kumtaka awe makini wakati wote na ndimi zake... “Japo ni maoni yake, lakini mengine yana gharama kubwa, lazima uchunge ulimi wako.”

Baadaye, Sitta alisimama akimtaka Keissy aombe radhi, jambo alilolikubali kiaina akisema, “Nilichokizungumza kina ukweli katika Bunge la Muungano lakini kama nimekosea naomba msamaha,” alisema.

Asindikizwa kutoka

Baada ya Sitta kuahirisha kikao, Keissy alifuatwa na mmoja wa wahudumu wa Bunge, Waziri Kizingiti na kumshika mkono hadi kwa wapambe wa Bunge waliomchukua na kumpeleka katika Ofisi ya Spika iliyopo kwenye jengo la Bunge na baadaye kutoka naye nje wakitumia mlango unaotumiwa na Waziri Mkuu kuingia na kutoka bungeni akiwa amezungukwa na askari wa Bunge watano hadi mlango wa kutoka nje ya eneo la Bunge ambao kwa kawaida hutumiwa na viongozi wakuu wa Serikali na Bunge.

“Mheshimiwa Keissy? Gari lako liko wapi uende ukapakie,” alisikika mmoja wa wapambe akimuuliza Keissy ambaye alisema hana gari akiwataka wamwache arudi ndani akachukue begi lake lakini alikataliwa na badala yake alipelekwa hadi sehemu ya ukaguzi katika lango la kuingilia na kupewa kiti huku akiwa amezungukwa na wapambe hao.

Nje ya Ukumbi wa Bunge, wajumbe kutoka Zanzibar walikuwa wakimsubiri atoke kwa takriban dakika 30 bila mafanikio.

“Keissy yuko wapi? Kama mwanamume kweli atoke, wanamfichaficha ndani ili iweje? Tumechoka na matusi yake,” alisikika mmoja wa wajumbe akisema.

Akizungumza baada ya kufika hotelini, Keissy alisema hakuna anachoogopa kwa sababu alisimama katika ukweli katika mazungumzo yake.

“Mimi nilizungumza badala ya Watanganyika na ukweli ndiyo huo hata kama kuna watu ambao hawataki kuusikia,” alisema Keissy.

Alisema aliyasema maneno hayo kwa nia ya kutaka kuboresha Muungano katika Katiba inayoandikwa hivi sasa na si kuuvunja kama alivyotafsiriwa na Wassira.

No comments:

Post a Comment