Saturday 20 September 2014

SMZ: HAKUNA MWENYE UBAVU WA KUIPORA PEMBA

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein 

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema Kisiwa cha Pemba ni miliki ya Zanzibar na sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hakuna nchi yoyote yenye ubavu wa kukichukua kisiwa hicho, imeelezwa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumzia mvutano wa mipaka uliojitokeza katika usawa wa Bahari ya Hindi kwenye mwambao wa Somalia na Kenya na kulihusisha eneo la Pemba ikielezwa kuwa ni sehemu ya Kenya.

Kauli ya Waziri huyo imekuja baada ya hivi karibuni kuripotiwa kuwa Somalia imeishtaki Tanzania katika Mahakama ya Kimataifa kuwa inakalia Kisiwa cha Pemba ambacho ni mali ya Kenya.

Vilevile Somalia imeishtaki Kenya katika mahakama hiyo na kwamba nayo iko katika hatari ya kupoteza umiliki wa visiwa katika Pwani ya Bahari ya Hindi.

Aboud alisema mipaka ya nchi inaonyesha wazi Kisiwa cha Pemba kimekuwa ni sehemu ya Zanzibar na hakuna sababu ya kulitilia shaka jambo hilo kuhusu mvutano uliojitokeza baina ya mataifa hayo na kuamua kufungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa.

“Kelele za mlango daima haziwezi kumnyima usingizi mwenye nyumba, Kisiwa cha Pemba ni mali ya Zanzibar na sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania…mipaka hiyo itabaki hivyo,” alisema Waziri Aboud.

Alisema katika sura ya kwanza ya Katiba ya Tanzania (2)(1) imeeleza bayana kuwa, eneo la Jamhuri ya Muungano ni la Tanzania Bara pamoja na sehemu ya bahari inayopakana nayo.

Alisema hakuna sababu yoyote ya Wazanzibari kuwa na hofu na kwamba SMZ chini ya Jamhuri ya Muungano iko makini katika kulinda rasilimali na mipaka yake.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk Mahadhi Juma Maalim alisema Serikali imeanza kufuatilia kwa karibu suala hilo ili kupata ukweli kwa kile kilichoripotiwa kuhusu Kisiwa cha Pemba kuwa katika eneo la Kenya.

Dk Mahadhi alisema kwa kuwa kesi ya mipaka kati ya Kenya na Somalia iko katika Mahakama ya Kimataifa, kwanza watahitaji kufahamu madai ya pande mbili hizo katika kesi ya msingi.

Walioshtakiwa na kufikishana mahakamani

“Serikali itafuatilia ili kupata ukweli wa kuibuka kwa madai hayo ingawa mipaka yetu inafahamika kitaifa na kimataifa…hatuna wasiwasi na jambo hilo na kama kutakuwa na ulazima wa kuingia katika kesi hiyo, tutalazimika kufanya hivyo tukiwa tunajiamini,” alisema Dk Mahadhi.

Hata hivyo, Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar, Awadh Ali Said alisema kwamba Kisiwa cha Pemba na Mombasa vilikuwa ni sehemu ya Zanzibar chini ya utawala wa kisultan akiwa chini ya uangalizi wa Uingereza mara baada ya ukataji wa mipaka baada ya Mkutano wa Berlin Ujerumani mwaka 1884/85.

“Ni ajabu kusikia kuwa Pemba ni sehemu ya Kenya badala ya kusikia Mombasa ni sehemu ya Zanzibar, kabla na baada ya mwaka 1963 bendera ya Sultan wa Zanzibar ilipepea huko Mombasa na maeneo yote umbali wa maili kumi toka usawa wa bahari yakiwa chini ya himaya ya Zanzibar,” alisema Awadh.

Chanzo: Mwananchi, Tanzania





No comments:

Post a Comment