Tuesday 9 September 2014

SHAIRI - MADAFU



Unapokunywa ni raha,         Wasifia ihsani
Wajipa nawe furaha,            Tena isiyo kifani
Ila kuna na karaha,               Kawaulize wandani
Ukiyapenda madafu,             Ujifunze na kukweya

Mbona hukwenda Kiunga,    Kama umkwezi kweli
Au ukapita Tanga,                 Kuangua yalo mali
Umeng'ang'ana Ukonga,        Kwenye madafu mawili
Ukiyapenda madafu,              Ujifunze na kukweya

Ukwezi sharti ujuzi,               Na jitihada muruwa
Hautaki mtu `lazy’,                Asiyejituma sawa
Hebu tizama wakwezi,          Namna wanavyopagawa
Ukiyapenda madafu,             Ujifunze na kukweya 

Si lazima uwe kipa,               Kwa mnazi kuukweya
Pengine ukala papa,              Kidhani tasaidiya
Mabingwa hutoka kapa,       Mchovu yu kidedea
Ukiyapenda madafu ,           Ujifunze na kukweya    

Unafurahia ladha,                 Na kiu kuondokewa
Kujiona wewe ‘father’,        Baada ya kukamuwa
Hayaokotwi ‘brother’,         Mnazini metolewa
Ukiyapenda madafu,            Ujifunze na kukweya  

Mashairi yana ladha yake na hasa yakiandikwa kwa lugha fasaha na aina yake.
Shairi hili limeandikwa na Wazir Khamsin

1 comment:

  1. Tungo ameandika, nzuri yakuvutiya
    Elimu imenifika, Ushairi kupitiya
    Kalamu nikaishika,Dafu nalifagiliya
    Mtunzi umesifika, ushairi kupitiya

    Mizani zimetuliya, nami najifundishiya
    Dafu kwetu asiliya, kinywaji kilotuliya
    Pwani twajiliwaziya, kinywaji kufurahiya
    Mtunzi umesifika, Ushairi kupitiya

    Fumbo la dafu sawiya, kwangu nimeliridhiya
    Wachanga kufundishiya, nasi tuje furahiya
    Kalamu uloandikiya, shani naitunukiya
    Heshima nakupatiya, haki umeitendeya

    Mtunzi wa Vitabu.
    rahmamahmoudmk@yahoo.com




    ReplyDelete