Saturday, 13 September 2014

IMANI ZAIDI KWA BI KENYATTA KULIKO WANASIASA

Bi Margaret Kenyatta, mke wa Rais Uhuru Kenyatta

Wakenya wana imani zaidi na mke wa Rais wao (First Lady) Margaret Kenyatta kuliko mtu yeyote anayejulikana nchini Kenya, kulingana na utafiti mpya uliofanywa na Ipsos Synovate.

Umma nao unamwamini zaidi kuliko bunge, mahakama, baraza la mawaziri na serikali za mitaa.

Asilimia 39 ya walioulizwa kwenye utafiti huo uliofanywa mwezi Agosti na kutolewa siku ya Alhamis wameelezea “kuwa na imani sana” na mama huyo, asilimia 73 wakiwa wanavutiwa naye huku 15% tu wakiwa na hisia hasi dhidi yake.

Idadi ya Wakenya walioonyesha kutovutiwa na Bi Kenyatta pia ni ndogo kuliko utafiti wowote aliofanyiwa mtu maarufu.

Rais Uhuru Kenyatta ameongoza miongoni mwa wanasiasa, asilimia 43 ya waliohojiwa wakionyesha kuwa na imani naye.

Hata hivyo idadi hiyo imeshuka kwa 10 kutoka Novemba mwaka jana alipokuwa na asilimia 53 ya walio na imani naye.

Imani kwa Naibu Rais nayo imeshuka kutoka asilimia 48 hadi 38 katika kipindi sawa na Rais Kenyatta.

Asilimia 28 imeonyesha kuwa na imani na kiongozi wa Cord, Raila Odinga na 20% kwa mkuu wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka
Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Cord Raila Odinga


Tom Wolf ambaye alikusanya maoni ya watu kutoka Ipsos Synovate alisema kushuka kwa asilimia za Rais na Naibu wake ni kupungua kwa mcheche wa baada ya uchaguzi.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wamehoji takwimu hizo, wakisema mfumo uliotumika hauna uwiano.

“Nafasi ya Rais na naibu wake kwa sasa haziwezi kulinganishwa. Rais hapa Kenya bila shaka ataongoza tu akishindanishwa na wapinzani au wenzake, “ alisema Prof Fredrick Wanyama.

Aliongeza kuwa maoni ya watu “yalikusudia kuonyesha kuwa viongozi wa upinzani hawawajibiki”.

Dr Adams Oloo alisema utafiti huo uliofanywa ni sawa na kulinganisha tufani na chungwa.

Chanzo: Daily Nation, Kenya                 
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu


No comments:

Post a Comment