UMEPATA kusikia jina la Dk. Asanterabi Malima?
Jambo
moja ambalo wanafunzi waliosoma naye nchini Tanzania hawabishani kuhusu
Malima ni ukweli kwamba alikuwa ni mwanafunzi mwenye akili nyingi
darasani.
Shafii Dauda ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha
kwanza katika Shule ya Sekondari Azania jijini Dar es Salaam,
anamkumbuka Asanterabi kama mwanafunzi mwenye akili aliyefanya vizuri
sana katika masomo yake ya kumaliza kidato cha nne.
Shafii, ambaye
sasa ni miongoni mwa watangazaji na wachambuzi maarufu wa
mchezo wa
soka hapa nchini alikuwa kidato cha kwanza wakati Malima alikuwa kidato
cha nne.
Akili ile ya Malima imemfikisha nchini Marekani ambako
sasa amefanya ugunduzi wa kidude chenye saizi ya pini ndogo (milimita
0.250) kinachoweza kubaini magonjwa ya kuambukiza, kansa na moyo katika
hatua ya awali kabisa.
Mtafiti wa Kisayansi
Ugunduzi huu, utakapofika mwisho wake,
unaweza kuokoa maisha ya watu wengi duniani. Fikiria tu kwamba unakuwa
na kifaa ambacho mojawapo ya magonjwa hayo yakikuanza unaubaini mapema
na kwenda kutibiwa.
Mamilioni ya watu wataokolewa maisha yao na kijana huyu wa Kitanzania.
“Siku
zote nimekuwa na ndoto za kugundua kitu ambacho kitaweza kuokoa maisha
ya watu. Baba yangu alifariki kwa ugonjwa wa moyo ambao ungegundulika
mapema kama kungekuwa na kifaa kama hiki.
“Kwa sasa sitaweza
kuokoa maisha ya baba yangu lakini ninaweza kuokoa maisha ya wazazi au
watoto wa watu wengine kutokana na ugunduzi huu nilioufanya. Nafurahi
kwamba ndoto yangu imetimia.
“Kansa, baadhi ya magonjwa ya
kuambukizwa na magonjwa ya moyo huwa yanachelewa sana kugundulika. Watu
wengi hupoteza maisha, na kwa nchi zilizoendelea hutumia pesa nyingi
sana kuwatibu waathirika.
“Kifaa nilichogundua ni kidude cha
ukubwa wa pini (0.250mm) kinachoweza kupima na kugundua hayo magonjwa
mapema. Ili, yaweze kutibika kirahisi, kuokoa maisha na kupunguza
gharama,” anasema
Asanterabi katika mazungumzo yake na Raia Mwema
yaliyofanyika kwa njia ya mtandao juzi Jumatatu.
Asanterabi ni
mtoto wa aliyepata kuwa waziri wa fedha wa Tanzania, Profesa Kighoma Ali
Malima, aliyefariki dunia Agosti 6, 1995 jijini London, Uingereza,
katika mojawapo ya vifo vya kushtusha katika historia ya Tanzania.
Kifaa
alichokigundia kijana huyu wa Kitanzania kinafahamika kwa jina la
Biolom na ugunduzi huu aliufanya akishirikiana na wanafunzi wenzake
wawili wa Chuo Kikuu cha Northeastern kilichopo Boston; Cihan Yilmaz na
Jaydev Upponi.
Pamoja na udogo wake, kipini hicho kina jumla ya
maeneo manne –yote yenye kazi maalumu, na ubunifu huo tayari
umetambuliwa na Serikali ya Marekani.
Katika mazungumzo yake na
vyombo vya habari vya Marekani, Asanterabi alipata kusema kwamba vifaa
vingi vya kisasa hubaini magonjwa; kwa mfano kansa, katika wakati ambapo
ni vigumu mtu kupata tiba na kupona.
“Kazi yetu hii
itakapokamilika, tutaweza kubaini magonjwa haraka zaidi na mapema zaidi
na hivyo watu watapata tiba mapema na kuokoa maisha.
“Nchini
kwangu (Tanzania), akinamama wengi hufariki dunia kwa sababu ya kuugua
ugonjwa wa kansa ya kizazi, kifaa hiki kitaweza kusaidia watu wengi
kupona kutoka katika matatizo yao,” alisema.
Kidude hicho ni
kidogo sana kwa umbo na namuuliza kama wameamua iwapo mtu anaweza
kukinunua na kubaki nacho nyumbani akijitazama mwenyewe au ni lazima
aende hospitali.
“Dhamira yetu hapo ni kipimo kitumike mtu akienda
hospitali au kliniki (for annual check-up). Lakini japokuwa kinafanya
kazi, kupata ruhusa kwa kukiingiza kama pini ni vigumu. Tunafanya vipimo
(test) kwa kupima damu iliyotoka kwa mgonjwa,” anasema.
Elimu yake
Asanterabi
ni zao la mfumo wa masomo wa kawaida uliokuwepo hapa nchini miaka
michache iliyopita (kabla ya ujio wa hizi za kata na ‘academy’).
Alisoma katika Shule ya Sekondari ya Tambaza jijini Dar es Salaam kwa mwaka mmoja kabla ya kuhamia Azania.
Miaka
20 iliyopita, hizi zilikuwa ni shule zilizokuwa zikichukua watoto
waliofaulu vizuri kimasomo miongoni mwa wanafunzi wa shule za msingi za
Mkoa wa Dar es Salaam.
“Tambaza nilisoma mwaka mmoja tu lakini
kutokana na fujo zilizokuwapo nikahamishwa na wazazi na ndipo nikaenda
Azania nilikosoma mpaka kumaliza kidato cha nne. Nashukuru kwamba
nilifaulu vizuri kwa kupata daraja la kwanza. Kimsingi, nilipata alama A
katika masomo yangu yote,” anasema.
Pamoja na muda wote
alioutumia Marekani na umaarufu ambao ameupata kama mmoja wa vijana
wenye bongo zinazochemka nchini humo, Asanterabi bado hajasahau maisha
ya hapa nchini na, hususan, maisha ya shule.
Kimsingi, Asanterabi
anasikitishwa sana na matokeo mabovu ambayo baadhi ya shule alizosoma
katika miaka ya nyuma zimekuwa zikiyapata katika miaka ya karibuni.
“Kwa
kweli nakumbuka sana walimu wangu. Pale Tambaza, kwa mfano, namkumbuka
sana mwalimu mmoja alikuwa anaitwa Mama Msuya, huyu nadhani ndiye
alikuwa mwalimu bora kuliko wote pale. Huyu alikuwa anafundisha
Jiografia.
“Katika shule ya Azania, namkumbuka sana Mama Shija
ambaye naye alikuwa akitufundisha somo la Kemia. Mzizima namkumbuka sana
mwalimu mmoja alikuwa anaitwa Thind - best mathematician ever (mwana
hisabati bora kuliko wote niliowahi kufundishwa nao).
“Elimu ni
sehemu nyingine ambao inanisisimua mno. Nimefuatilia katika tovuti ya
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ( moe.org.tz ) kuwa mwaka 2011,
karibu asilimia 50 ya wanafunzi walipata alama sifuri. Tambaza,
Forodhani, Kibasila na Azania zilikuwa na watu wenye akili kuliko wote,
pengine Tanzania nzima.
“Niko sasa nafanya kazi na vichwa vya
bongo huku Marekani tuone tunaweza kufanya nini kutoa mchango kwa
"online video learning" (mafunzo kwa njia ya mtandao maana wengi wetu
tulisoma bure tu na huo utakuwa sehemu ya mchango wetu kwa Taifa,”
anasema.
Matarajio
Kutokana na ubunifu huo alioufanya na wenzake hao, Malima
sasa anatakiwa kuanzisha kampuni ambayo itafanya biashara ya ubunifu
huo utakaoleta mapinduzi katika sekta ya afya duniani kote.
Haya
ni mabadiliko makubwa katika maisha ya Asanterabi ambaye aliwahi
kunukuliwa na vyombo vya habari vya Marekani akisema kwamba siasa iko
kwenye damu ya familia yao.
Baba yake alikuwa mwanasiasa na msomi
maarufu nchini na kaka wa Asanterabi, Adam, sasa ni Naibu Waziri wa
Fedha katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete. Pia ndiye Mbunge wa Jimbo
la Mkuranga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Kusema kweli mimi
sijawahi kujiona kama mjasiriamali (mfanyabiashara). Watu wengi walijua
kwamba nitakapokuwa mkubwa nitafuata tu nyayo za wazee wangu. Lakini leo
niko hapa.
“Kwenye maisha yangu, sikutaraji kwamba ipo siku
nitakuja kufanya ubunifu kama huu. Baada ya kufika hapa nilipofika, sasa
naamini kwamba naweza kupiga hatua zaidi,” anasema.
Ingawa fedha
si msukumo mkubwa katika maisha ya Asanterabi, ugunduzi huu unaweza
kumfanya kuwa mmoja wa Watanzania matajiri endapo kidude hiki kitaanza
kuuzwa.
Hesabu zake ziko hivi
“Tunafikiri kitakapokuwa
tayari, kidude kimoja kinaweza kuuzwa kwa wastani wa dola moja hivi ya
Marekani (Shilingi 1650) kama tukiweza kufanya uzalishaji mkubwa.
“Gharama
ya kupimwa inaweza kugharimu kiasi cha kati ya dola 10-15. Mahospitali
huwa wanachaji hela nyingi mno kama daktari ndio atafanya vipimo na
maamuzi. Ila kama ni nesi gharama si kubwa,” anasema.
Katika dunia
yenye watu zaidi ya bilioni sita, uwezekano wa kuuza pini hizo milioni
mia moja kwa mwaka ni mkubwa na kwa kiasi hicho pekee, mauzo ya zaidi ya
dola milioni 100 kwa mwaka (zaidi ya shilingi bilioni 165)
yanawezekana.
Asanterabi na wenzake watakuwa na mgawo wao hapo na
ifahamike kwa sababu ya sheria kali za hatimiliki nchini Marekani, hizi
ni fedha ambazo familia ya wagunduzi watakula hadi kwa wajukuu, vitukuu
na kuendelea.
Mitihani iliyomkumba
Safari ya Asanterabi kutoka Tanzania kwenda Marekani
haikuwa rahisa namna hiyo. Ikumbukwe kwamba alifiwa na baba yake wakati
ndiyo kwanza akiwa na umri wa miaka 15 tu.
Ni msiba ambao nusura
ubadili kabisa maisha ya kijana huyu ambaye baadhi ya wanafunzi
waliowahi kusoma naye wanamtambua kwa jina la “Mzaramo wa Chole.”
Chole
ni miongoni mwa mitaa maarufu ya eneo la Oysterbay jijini Dar es Salaam
ambako Asanterabi alikulia. Pengine, jina hilo linatokana na ukweli
kwamba kuna watu wachache wa kabila la Wazaramo analotoka Malima
wanaoishi huko.
Majina ya namna hii hayakuwa na maana ya ubaguzi wa kikabila lakini ni sehemu ya utani wa kikabila uliokuwa Tanzania wakati huu.
Utafiti
na ubunifu huu wa Asanterabi si habari kubwa hapa Tanzania pekee kwani
inaonekana kwamba hata Marekani nako ameanza kutambulika.
Juni
mwaka huu, wakati wa sherehe za maadhimisho ya Wiki ya Afrika katika
Jimbo la Massachussets uliko mji wa Boston, Gavana wa Jimbo hilo, Deval
Patrick, alimpa Asanterabi tuzo maalumu ya Ujasiriamali akimpongeza kwa
ubunifu wake huo utakaosababisha nafuu kwa maisha ya wanadamu na pia
ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.
“Si kwamba ugunduzi huu utabadili
maisha ya wengi na uchumi kwa wakazi wa Marekani pekee, lakini ugunduzi
huu utasaidia sana kuokoa maisha ya mamilioni ya wananchi katika nchi
anakotoka Malima ya Tanzania,” alisema Gavana huyo.
Miaka michache
iliyopita, Asanterabi alikuwa akijipanga kuwa mmoja wa waajiriwa katika
mojawapo ya kampuni kubwa duniani ya Toshiba, lakini sasa ugunduzi huu
umemfanya kujiandaa kuwa mmoja wa viongozi wa kampuni muhimu hapa
duniani.
Pamoja na umbali mkubwa uliopo sasa, baadhi ya watu
wanaomfahamu Asanterabi wanamkumbuka kama kijana mpole ambaye
hakuharibiwa na ukubwa wa jina la baba yake.
“Mzaramo wa Chole
alikuwa mpole sana kipindi kile anasoma Azania na kwa kweli hakuwa na
mambo mengi kama walivyo watoto wengi wa wakubwa,” anasema Mintanga
Malulu aliyesoma katika shule hiyo wakati mmoja na Asanterabi.
Jambo
zuri kuhusu Asanterabi ni kwamba ni mzalendo na anayependa nchi yake.
Katika mazungumzo yake na Raia Mwema, alisema kwamba kwa namna yoyote
ile ugunduzi wake huo utaifaidisha Tanzania.
Tayari Tume ya
Sayansi na Teknolojia Tanzania (Costech) imetangaza kuvutiwa na
mafanikio ya Asanterabi katika Nyanja hiyo ya sayansi.
Taarifa
iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Dk. Flora
Tibazarwa, inasema ingawa utafiti huo bado haujafikia katika hatua ya
mwisho, matumaini ni makubwa.
“Tuna taarifa kuhusu ugunduzi wa Dk.
Malima lakini hatuwezi kusema chochote kwa sasa kwa vile bado uko
katika hatua za awali na haujapita katika vipimo vyote. Jambo zuri ni
kwamba dalili za kufanikiwa ni kubwa,” ilisema taarifa hiyo.
Ni
safari ndefu, ndefu sana kutoka Tanzania hadi Marekani. Lakini, kama
mwisho wake ni kama ule wa Asanterabi, safari inakuwa njema.
Wakati
tukiagana baada ya kumaliza mazungumzo yetu, bado alionyesha
kusikitishwa na matokeo katika shule za sekondari maarufu; Hivi, kuna
nini kinatokea huko kwa Azania na Tambaza?
Sikuwa na majibu. Labda
nitapata kama nitafanya utafiti. Labda, itabidi Asanterabi agundue
kidude kingine kitakachotoa majibu kuhusu kushuka kwa elimu hapa nchini.
Swali
moja kubwa ambalo nimejiuliza baada ya mazungumzo yangu na Asanterabi
ni moja tu; Hivi kweli Taifa hili litakuja kutoa akina Asanterabi
wengine katika miaka 20 ijayo katika mfumo wetu wa elimu tulionao sasa?
Chanzo: Raia Mwema, Tanzania
No comments:
Post a Comment