Mubarak alisafirishwa kwa helikopta ya jeshi kufikishwa mahakamani siku ya Jumamosi |
Mahakama ya Misri inatarajia kutoa uamuzi kwenye kesi inayomkabili aliyekuwa Rais wa Misri Hosni Mubarak kwa makosa ya rushwa na kuua waandamanaji wakati wa ghasia za mwaka 2011.
Mubarak, mwenye umri wa miaka 86, anashtakiwa pamoja na watoto wake wa kiume na aliyekuwa waziri.
Alikutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha mwaka 2012, lakini hukumu hiyo baadae ilibadilishwa.
Mubarak aliiongoza Misri kwa takriban miaka 30 kabla ya ghasia kuibuka na kuondolewa.
Aliachia madaraka baada ya wiki kadhaa za vurugu zilizosababisha vifo vya mamia ya waandamanaji nchini humo.
Kesi hiyo mpya ilianza Aprili 2013, na imeahirishwa mara chungu nzima.
Wachambuzi wanasema Mubarak huenda akaachiwa huru, baada ya mashahidi wengi kubadilisha ushahidi wao na ukiegemea upande wake.
Mubarak tayari anatumikia miaka mitatu gerezani kwa ubadhirifu wa mali ya umma.
Alikutwa na hatia mwaka 2012 kwa mashtaka yanayohusiana na mauaji ya waandamanaji pamoja na aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani Habi al-Adly, na kuhukumiwa kifungo cha maisha.
Watoto wake wa kiume Alaa na Gamal nao kwa sasa wanatumikia kifungo cha miaka minne jela kwa ubadhirifu wa mali za serikali.
Pamoja na baba yao walitozwa faini $3m na kuamriwa kurejesha $17.6m waliotuhumiwa kuiba.
No comments:
Post a Comment