HUONI WANAVYOKULA, KWA UKWASI NA MADAHA
KWAO NI KAMA KULALA, HAWAIPENDI KARAHA
SIWAONE NI MAFALA, NI WENYE NYINGI STAHA
NA UNAPOKULA NAO, JIKANYE HAYO MATONGE
SIJIONE UMJUZI, KWA MATONGEYO MAKUBWA
UKADHANI HAWAWEZI, KULA NA WAO UBWABWA
WASTAHABU ULEZI, LAINI USIO MWIBA
NA UNAPOKULA NAO, JIKANYE HAYO MATONGE
VIJITI YAO ASILI, HUKO WALIKOZALIWA
WALA NAVYO KWELI KWELI, KAMA KUTAFUNA MIWA
WAVITUMIA KWA WALI, NA HATA KWENYE HALUWA
NA UNAPOKULA NAO, JIKANYE HAYO MATONGE
VIMACHO VYAO VIDOGO, NDIVYO MNAVYOWASEMA
HAWAUONI MUHOGO, NA WAKILA WANAHEMA
MAMBO MDOGO MDOGO, NDIYO UFIKE SALAMA
NA UNAPOKULA NAO, JIKANYE HAYO MATONGE
Shairi hili limeandikwa na Wazir Khamsin
No comments:
Post a Comment