Saturday, 27 September 2014

CHELSEA CLINTON AJIFUNGUA MTOTO WA KIKE

Chelsea Clinton (September 2014)
Mtoto wa Chelsea ni mjukuu wa kwanza wa Bill na Hillary Clinton

Chelsea Clinton, binti wa aliyekuwa Rais wa Marekani Bill Clinton na aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Hillary Clinton, amejifungua mtoto wa kike.

"Mimi na Marc tuna mapenzi, furaha na tunatoa shukran wakati tukisherehekea kuzaliwa kwa binti yetu, Charlote Clinton Mezvinsky, " Bi Clinton aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa twitter.

Bi Clinton, mwenye umri wa miaka 34, aliolewa na Marc Mezvinsky mwaka 2010, na kutangaza kuwa mjamzito Aprili 2014.

Binti huyo anazaliwa huku Bi Hillary Clinton akiwa na nia ya kugombea urais mwaka 2016.

Anaonekana kuwa mgombea mkuu kupitia chama cha Democrat na mrithi wa Rais Barack Obama, na alisema atachukua uamuzi wa kugombea au la mwanzoni wa mwaka 2015.

Bill Clinton alikuwa rais wa 42 Marekani , kuanzia Januari 1993 hadi Januari 2001.

Chelsea Clinton, alisomea vyuo vikuu vya Stanford, Columbia na Oxford, anasimamia Wakfu wa Clinton akishirikiana na wazazi wake.

Bi Clinton aliacha kazi iliyokuwa ikimlipa $600,000 kwa mwaka kama mwandishi maalum wa habari wa NBC mwezi Agosti ili ashughulike na ujauzito wake.


No comments:

Post a Comment