Wednesday, 10 September 2014

RAIS KIKWETE HATAONGEZA MUDA BUNGE LA KATIBA

Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania, John Cheyo akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari, alipokuwa akitoa tamko kuhusu mchakato wa Katiba na Uchaguzi Mkuu wa 2015, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi 

Makubaliano baina ya Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kutaka Bunge Maalumu lifikie ukomo Oktoba 4, mwaka huu yamezua sintofahamu mjini hapa huku uamuzi huo ukionekana kuwachanganya viongozi wa Bunge hilo.

Kutwa nzima ya jana, viongozi wa Bunge Maalumu walishinda kwenye vikao vya mashauriano huku wabunge wa CCM wakitarajiwa kukutana jana usiku kwenye makao makuu ya chama hicho kupewa taarifa rasmi za uamuzi huo.

Katika makubaliano baina ya TCD na Rais Kikwete, imeamuliwa kuwa uamuzi wa Rais kupitia Tangazo la Serikali (GN) 254 la kuongeza siku 60 hadi Oktoba 4 uheshimiwe na baada ya tarehe hiyo Bunge liahirishwe.

Uamuzi huo ni kinyume cha azimio la Bunge Maalumu la Agosti 5, 2014 ambalo lilirekebisha Kanuni ya 14 (4) na kuifuta Jumamosi katika siku zilizotajwa kuwa za kazi, pia sikukuu na siku za Jumapili.

Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta alikaririwa akiwaambia wajumbe wa Bunge hilo kwamba Rais alikuwa ameridhia kwamba siku 60 alizotoa hazingejumuisha Jumamosi, Jumapili na siku za sikukuu.

Chanzo: Gazeti la Mwananchi, Tanzania



Ni kwa msingi huo, Bunge hilo likapanga kwamba lingeendelea na shughuli zake hadi Oktoba 31, wakati Mwenyekiti wa Bunge atakapokabidhi Katiba inayopendekezwa kwa Rais Kikwete.

Hata hivyo, makubaliano yaliyofikiwa baina ya viongozi wa TCD na Rais yanaonekana kuvuruga kabisa ratiba ya Bunge hilo ambalo jana na juzi, Kamati ya Uongozi ilikutana mara kadhaa kuona jinsi ya kunusuru mchakato huo.

Ingawa haikufahamika mara moja kama vikao hivyo vya kamati ya uongozi inayoongozwa na Sitta mwenyewe vinajadili nini, lakini taarifa zimedai huenda kukawa na mabadiliko makubwa ya ratiba.

Habari nyingine zinadai kwamba mabadiliko hayo huenda yakapunguza muda wa baadhi ya shughuli za kazi za Bunge hilo ili liweze kukamilisha kazi yake ikiwamo wajumbe kupiga kura ya uamuzi.

Katika kikao cha jana asubuhi, kamati hiyo ilishindwa kurekebisha ratiba yake ili iendane na siku zilizosalia, hivyo kuahirishwa kwa kuwapa kazi wataalamu wake kuleta mapendekezo ambayo yangejadiliwa jana mchana.

Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alithibitisha jana kwamba ratiba ya Bunge imebadilika kutokana na hoja nyingi kukubalika ndani ya kamati.

“Kamati ya uongozi itakutana baadaye (jana) kuangalia vipengele ambavyo hawakukubaliana kwenye kamati ndivyo wavipangie muda na ratiba itajulikana baada ya kikao hicho,” alisema Hamad.

Hofu ya akidi

Hata hivyo, habari zaidi zinadai kwamba uongozi wa Bunge Maalumu ulichanganywa na kuwapo kwa hoja za baadhi ya wajumbe wake kutaka kwenda Makka kwa ajili ya kushiriki Ibada ya Hijja, hali inayotishia akidi kwa ajili ya kuendesha vikao.

Kanuni za Bunge Maalumu zinataka kuwapo kwa nusu ya wajumbe kutoka pande zote za Muungano wakati wa kuendesha vikao vyake na theluthi mbili ya wajumbe hao kila upande wakati wa kufanya uamuzi au kupiga kura.

“Tumetoka kwenye kikao mchana huu na pengine tutaitana tena maana hatujafikia mwafaka, kuna mambo mengi yamejitokeza lakini kubwa ni hili la wenzetu ambao wanataka kwenda Hijja, kuondoka kwao kunaweza kuathiri akidi kwa kiasi kikubwa,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya kamati hiyo.

Kutokana na matakwa hayo, hivi sasa Ofisi ya Katibu wa Bunge inafanya tathmini ili kufahamu idadi ya wajumbe ambao watakwenda Hijja Septemba 22, mwaka huu, ambao wengi wanatoka Zanzibar.

Hamad alikiri kwamba kuna mambo mengi ambayo ofisi yake inayafanyia kazi na kwamba hilo la Hijja ni mojawapo... “Kwa sasa siko katika nafasi ya kuzungumza kwa kirefu, kikao cha Kamati ya Uongozi kimeisha na bado kuna kazi nyingi za kuona jinsi tunavyoendelea.”

Tayari Bunge hilo limetikiswa na kutokuwapo kwa wajumbe waliosusia vikao tangu Aprili 16, mwaka huu ambao ni wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao unaundwa na vyama vya CUF, Chadema na NCCR Mageuzi na baadhi kutoka Kundi la 201.

Taarifa ya TCD

Jana saa 7:00 mchana, Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo alikutana na wanahabari na kueleza kuwa katika mazungumzo yao na Rais wamekubaliana mambo matano ya msingi kwa mustakabali wa nchi.

Alisema pamoja na kazi ya msingi iliyofanywa na Bunge Maalumu, mchakato unaoendelea hauwezi kutoa Katiba Mpya ambayo itatumika katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

“Muda hautoshi kukamilisha mchakato na kufanya mabadiliko yatakayohitajika ya sheria, kanuni na taasisi mbalimbali zinazohitajika,” alisema Cheyo ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP).

Alisema kura ya maoni ilipangwa kufanyika Aprili 2015 na kama itabidi irudiwe, basi itabidi irudiwe itakuwa Juni au Julai 2015, muda ambao Bunge la Jamhuri linatakiwa livunjwe.

“Ili Katiba Mpya itumike katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, itabidi uhai wa Bunge na Serikali uongezwe zaidi ya 2015, jambo ambalo sisi viongozi wote hatuliungi mkono,” alisema Cheyo.

Alisema kwa kutambua kuwa kama kura ya maoni ikifanyika, italazimisha Uchaguzi Mkuu wa 2015 kuahirishwa, wamekubaliana kura hiyo iahirishwe hadi baada ya uchaguzi huo.

Bunge Maalumu

Cheyo alisema Bunge Maalumu kwa sasa linafanya kazi kwa mujibu wa Tangazo la Serikali (GN), namba 254 lililotolewa na Rais Kikwete ambalo uhai wake utakoma Oktoba 4.

“Inategemewa kuwa Oktoba 4 Katiba inayopendekezwa itapatikana. Tulikubaliana hatua hii iachwe ifikiwe na baada ya hapo Bunge liahirishwe hadi baada ya Uchaguzi Mkuu 2015.

“Tarehe 4 Oktoba ndiyo mwisho. Hiyo ndiyo sheria iliyopo, sisi hatuna mamlaka ya kuandika GN mpya, GN imetolewa na Bunge hili liko kihalali. Tulichokuwa tunabishana lisife kesho,” alisema.

Akijibu maswali ya wanahabari kama ana uhakika Bunge hilo litaweza kukamilisha kazi yake ndani ya siku zilizobaki, Cheyo alisema “Tumeheshimu sheria iliyopo tarehe nne Watanzania wanategemea Katiba Mpya itakuwa imepatikana, sasa kama haitapatikana hilo msiniulize kwa sababu hilo si jukumu langu.”

Alipoulizwa kama rais ajaye baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 ataendeleza mchakato pale ulipoishia alisema: “Naomba Mungu rais ajaye awe anayejali maoni ya wananchi hilo naomba kabisa. Sasa tukipata rais ambaye hatutambui sisi wote na mawazo yetu, basi tutakuwa tumekosea katika kupiga kura.”

Mabadiliko ya 15 ya Katiba

Cheyo alisema kwa vile Uchaguzi Mkuu wa 2015 utafanyika kwa kutumia Katiba ya 1977, ni vyema yakafanyika mabadiliko madogo ili kuruhusu uchaguzi huru na wa haki.

Mabadiliko hayo yatalenga kuwezesha uwapo wa tume huru ya uchaguzi, mshindi wa urais ashinde kwa zaidi ya asilimia 50, kuruhusu mgombea binafsi na kuingiza ibara itakayoruhusu matokeo ya urais kupingwa mahakamani.

“Vyama vya siasa ambavyo vinapenda kupendekeza mambo mengine ya kurekebisha katika Katiba ya 1977 vinaombwa kufanya hivyo kwa vile muda tulionao ni mdogo,” alisema Cheyo.

Alisema walikubaliana kuwa marekebisho hayo yafanyike katika Bunge la Jamhuri litakaloanza Novemba 5 na ikishindikana yafanywe Februari 2015.

Ukawa kurudi bungeni

Cheyo alisema suala la kurudi au kutorudi ndani ya Bunge Maalumu la Katiba kwa wajumbe wa Ukawa halikuwa sehemu ya mkutano kati ya Rais na TCD.

“Kila siku nasema uamuzi wa vyama tuuheshimu. Wale wana sababu zao za kutoingia bungeni ni lazima tuheshimu msimamo wao kwa sababu wanazo sababu,” alisema.






No comments:

Post a Comment