Tuesday, 23 September 2014

SHAIRI - BINGWA AMETOKA KAPA

Alileta zake mbwebwe, Na mashabiki lukuki
Akasema hata Wembe, Ukiletwa hakatiki
Yeye anakula sembe, Wali kwake hashituki
Bingwa ametoka kapa, Aso bingwa hali gani?
 
Akaivaa na jezi, Ugani akajitosa
Na kuwaita Malezi, Wale walokula kasa
Kumbe vile hajiwezi, Ni lijoka la kipisa
Bingwa ametoka kapa, Aso bingwa hali gani?
 
Aliposhindwa ugani, La kusema alikosa
Kusingizia utani, Kumbe vile ni garasa
Walikwama wa maini, We utumbo ndo kabisa
Bingwa ametoka kapa, Aso bingwa hali gani?
 
Unapokwenda mechini, Muhimu ujizatiti
Usijitie kundini, Na kuleta tashtiti
Ukija bila plani, Utarudi umaiti
Bingwa ametoka kapa, Aso bingwa hali gani?

Shairi hili limeandikwa na Wazir Khamsin

No comments:

Post a Comment