Sunday, 16 November 2014
HARAKATI ZA KISWAHILI AFRIKA MASHARIKI
Hivi sasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kuna harakati za kuraghabisha maendeleo ya wananchi wa nchi za Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi, lengo likiwa kuwashirikisha wananchi wa ngazi mbalimbali katika shughuli za uchumi, siasa, utamaduni, elimu, biashara na masuala ya kijamii.
Siku za nyuma, wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, walikuwa na uhusiano na ushirikiano wa karibu. Kutokana na hali hii, ilionekana kuwa Lugha ya Kiswahili ilitiliwa mkazo kuanzia enzi za ukoloni wa Ujerumani na Uingereza. Viongozi wa ukoloni wa Uingereza, walifikia hatua ya kuanzisha Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki mwaka 1930. Vikao viliendeshwa kwa mzunguko.
Kwa mfano, kuanzia mwaka 1930 Kamati ilikuwa ikikutana Dar es Salaam, mwaka 1943 ilihamia Nairobi, 1952 Makerere (Uganda) na mwaka 1963, ilirudi Dar es Salaam. Mwaka 1964 Kamati ilikabidhi kazi zake Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Chuo cha Uchunguzi wa Kiswahili na baadaye kuwa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) ambayo sasa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI).
Jitihada za kukiimarisha Kiswahili katika Afrika Mashariki, ziliibuka tena mwaka 1994 walipokutana wakuu wa nchi za EAC, lengo lilikuwa ni kuimarisha tangamano kwa wananchi wa nchi hizo ili kuhimiza maendeleo yao.
ZINDUKA
Hili ni neno la Kiswahili na kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya TATAKI toleo la tatu, maana yake ni toka katika hali ya kutoelewa jambo au hali ya bumbuazi au kuzirai. Kwa Kirundi au Kinyarwanda maana yake ni kuamka kutoka katika hali ya kusinzia.
Zinduka ni wito kwa wananchi wa Afrika Mashariki, hasa viongozi kuongeza kasi, juhudi na mshikamano kwa kuzileta pamoja jamii mbalimbali.
Kaulimbiu ni sauti za watu, maendeleo endelevu kupitia sanaa, utamaduni, fursa za uchumi na siasa. Kwa mantiki hiyo Kampuni ya Nation Media Group(NMG), ilianzisha kitengo kinachojulikana kama ‘Swahilihub’ kwa madhumuni ya kutumia vyombo vya habari kama magazeti, redio na televisheni kwa lengo la kuwawezesha wananchi wa Afrika Mashariki wahamasike kukitumia Kiswahili katika shughuli zao za kila siku.
Inafahamika kwamba, nchi zinazozungumza Kiswahili kwa viwango tofauti ni Ethiopia, Djibuti, Kenya, Tanzania Bara, Zanzibar, Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Kongo, Burundi, Rwanda, Malawi, Msumbiji, Malawi, Zambia hata Zimbabwe.
Kiswahili ndiyo njia pekee ya kuamsha ari ya kutaka kuimarisha ushirikiano wa wananchi wa jumuiya hii katika shughuli za biashara, uchumi, elimu, utamaduni na za kijamii kama kutembeleana, kuoana, kuzikana na kadhalika.
Huko Arusha, Tamasha la Zinduka lililofanyika tarehe 6-8 Novemba 2014 na suala la tangamano lilijadiliwa kuhusu Lugha ya Kiswahili. Wajumbe wa tamasha hilo waliona kuwa Kiswahili kina nafasi kubwa katika kuimarisha mshikamano wa wananchi hao, lakini inakabiliwa na matatizo mbalimbali hata katika nchi kama Tanzania na Kenya, ambazo ziko mstari wa mbele katika ukuzaji wa Kiswahili.
Baadhi ya matatizo hayo ni ukosefu wa uzalendo kwa viongozi wa nchi hizi. Kwa mfano, inakuwaje viongozi wa juu kama marais, mawaziri, makatibu wakuu, wakurugenzi na mameneja wa mashirika ya umma, wanaendelea kutumia Kiingereza badala ya Kiswahili katika shughuli zao za kazi kama kwenye mikutano, semina na warsha?
Vilevile katika magazeti na vitabu vinavyochapishwa, lugha inayotumika haizingatii misingi ya lugha fasaha na iliyo sanifu, upatanishi wa kisarufi pamoja na tahajia sahihi.
Katika televisheni, mambo ni mabaya zaidi kwani matatizo yako zaidi katika matamshi, ambapo lafudhi ya lugha za asili yameshamiri, jambo lililowasikitisha wajumbe wa tamasha hilo ni kule kuchanganya Lugha ya Kiswahili na Kiingereza, kunakofanywa na wanasiasa na wanataaluma katika shughuli zao.
Ilionekana, kuwa hata katika vitabu vinavyotumika shuleni kuna dhaifu mkubwa na yako makosa mengi na siyo kwa lugha sahihi, bali pia ya kitaaluma.
Katika tamasha hilo, baadhi ya mada zilizojadiliwa ni pamoja na;
Nafasi ya vyombo vya habari katika ukuzaji wa Kiswahili. Kiswahili na matumizi yake katika maendeleo ya kijamii.
Historia fupi ya usanifishaji wa Kiswahili.
Changamoto za mawasiliano katika Afrika Mashariki. Ukuzaji wa Kiswahili katika fani ya tafsiri.
Hatua mbalimbali zilizofikiwa katika ukuzaji wa Kiswahili kwa nchi za Afrika Mashariki. Ili Lugha ya Kiswahili iwe kweli ni kiungo cha kuiendeleza jamii ya Afrika Mashariki ilipendekezwa kuwa;
Kuundwe kamati ya pamoja yenye wawakilishi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kushughulikia usanifishaji wa Kiswahili.
Kuandaliwe machapisho ya kufundisha Kiswahili kwa hatua za awali, kati na juu.
Kuwe na Sera ya Lugha katika nchi za Afrika Mashariki. Kwa kuwa Tamasha la Zinduka hufanyika kila mwaka, kuwe na utaratibu wa kufuatilia kila kinachoamriwa.
Makala zilizowasilishwa katika Tamasha la Zinduka, ziandaliwe kwa ajili ya marejeo.
Chanzo: Mwananchi.co.tz
Labels:
Makala
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment