Sunday, 9 November 2014

MISS TANZANIA AWEZA 'KUFUNGWA' MIAKA 3 JELA

Mshindi wa Redds Miss Tanzania 2014 Sitti Mtemvu (katikati) akiwa na mshindi wa pili Lilian Kamazima pamoja na watatu Jihan Dimachk

Shindano la mlimbwende wa Tanzania maarufu kama Miss Tanzania limetimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, huku likiandika historia mbaya baada ya mrembo wa 2014, Sitti Mtemvu kuvua taji hilo kutokana na kashfa ya kudanganya umri.

Kutokana na uamuzi huo, nafasi ya Sitti sasa itachukuliwa na Miss Arusha, Lilian Kamazima ambaye alishika nafasi ya pili katika Shindano la Redd’s Miss Tanzania 2014, lililofanyika Oktoba 11, mwaka huu katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Kung’oka kwa Sitti katika nafasi yake ya mlimbwende wa Tanzania ni tukio la kwanza tangu kurejeshwa kwa mashindano ya Miss Tanzania 1994.

Miss Tanzania wa 2000, Hoyce Temu akizungumzia hatua ya Sitti jana, alisema amepokea habari hizo kwa masikitiko ingawa ni kitendo ambacho kimerudisha heshima kwa tasnia ya urembo nchini.

“Baada ya hili sakata, kwa kweli tulivunjika moyo sisi warembo, kila tulipopita tulionekana kama watu tusio na maadili, tuliharibiwa jina na ilituvunja moyo, lakini kwa kuwa ameamua kurudisha taji, ameibadilisha Miss Tanzania,” alisema Hoyce.

Katika barua yake ya Novemba 5, mwaka huu kwenda kwa waandaaji wa shindano hilo ambao ni Kampuni ya Lino International Agency Ltd, Sitti alisema amechukua uamuzi huo kwa hiari bila kushawishiwa na mtu ili kulinda heshima yake pamoja na familia yake.


Katika barua hiyo ya ukurasa mmoja, Sitti ambaye ni mtoto wa Mbunge wa Temeke (CCM), Abbas Mtemvu anasema: “Natamka rasmi kuvua taji la urembo la Miss Tanzania 2014…leo nalivua taji nililopewa na binadamu, lakini alilonipa Mwenyezi Mungu bado ninalo.”

Hatua ya mrembo huyo anayedaiwa kwamba ana umri wa miaka 25 na siyo 23 kama anavyodai kwenye fomu za kuwania taji hilo, inahitimisha mjadala mkali ambao takriban mwezi mmoja umetikisa fani ya ulimbwende nchini.

Lundenga

Mkurugenzi Mtendaji, Kampuni ya Lino International Agency Ltd, Hashim Lundenga jana alikutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambako alithibitisha kupokea barua ya Sitti na kwamba sasa nafasi yake itachukuliwa na aliyekuwa mshindi wa pili, Lilian.

“Aliandika barua Novemba 5 mwaka huu na kutufikia sisi, tulikaa na kuitafakari barua hiyo na kutoa uamuzi huu, tumewataarifu Baraza la Sanaa (Basata) na hivyo taarifa hii ni rasmi kwa Watanzania hasa wadau wa mashindano ya urembo,” alisema Lundenga.

Kuhusu zawadi ya Sh18 milioni aliyopewa, Lundenga alisema suala hilo linabaki katika ofisi yao huku akifafanua kuwa Sitti hakuvuliwa taji kutokana na kashfa, bali ameamua kulivua kwa hiari yake.
“Naomba utofautishe kuvuliwa na kuvua mwenyewe, hapo kunakuwa na maamuzi tofauti, ila suala hili ni la kiofisi zaidi,” alisema Lundenga.

Kwa upande wake, Lilian aliyekuwa kwenye mkutano huo jana, alikubali ‘kuvaa’ viatu vya Sitti na kusema kuwa atafanya mambo makubwa katika mashindano ya mrembo wa dunia.

“Nimefurahi kupewa nafasi hii ambayo ni ngumu, ila kwa sababu nina malengo ya kufanya vyema, sidhani kama nitashindwa kufikia huko, nilishindana kwa lengo la kushinda na sasa ndoto yangu ya kuliwakilisha Taifa kimataifa limetimia,” alisema Lilian.

Kauli ya Hoyce

Hoyce alisema uamuzi wa Sitti ni mzuri kwa sababu hata angekwenda kushiriki Miss World, asingekwenda kama Sitti bali kama mrembo kutoka Tanzania.

Hata hivyo, Hoyce alisisitiza kuwa ni vyema Kamati ya Miss Tanzania izingatie kufanya uchunguzi wa kina kwa walimbwende wanaoshiriki ili kujua iwapo wameolewa, wamezaa au wamedanganya umri. “Huu ni wakati ambao Kamati ya Miss Tanzania ijiangalie upya, kama ni nyumba sasa ijengwe upya kwa sababu ile ya zamani imechakaa na inahitaji marekebisho,”alisema Hoyce ambaye sasa ni Mfanyakazi wa Ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) nchini.

Alisema Lundenga anatakiwa ayaangalie mashindano hayo kwa jicho pana zaidi na wasiyachukulie lelemama kama ilivyokuwa zamani na wasiwachague wasichana kutokana na sifa ya uzuri pekee bali kama viongozi wa nchi wanaoipeperusha bendera ya Tanzania.

“Kwa kweli kitendo cha Sitti kitakuwa funzo na kitawekwa kwenye rekodi ya Tanzania kwa muda mrefu. Hii ni nafasi ya pekee na ni mwenendo mpya kwa kamati ya Miss Tanzania,” alisema Hoyce. Alikosoa majaji wa mashindano hayo akisema kosa alilofanya Sitti wakati akijibu maswali kwenye shindano la mwaka huu pale alipojibu maswali kwa lugha ya Kifaransa wakati hakukuwa na uchaguzi wa lugha hiyo, kwamba alistahili kuenguliwa.

“Mimi ningemtoa mapema, kwa sababu ni wangapi wanakifahamu Kifaransa hapa nchini, kwangu mimi hakujibu swali kwa sababu hata alichojibu hakikuwa kimetafsiriwa tutajuaje kama ametutukana?” alihoji.

Alimtaka Sitti kuendelea na shughuli za kijamii kwa sababu tayari amekuwa ni sehemu ya jamii yenye mchango mkubwa.

“Aendelee na kazi za jamii, hata Vanessa William wa Marekani alivuliwa taji, lakini baadaye aliendelea na shughuli nyingine na akawa mwenye mafanikio, sisi dada zake tupo akitaka ushauri atufuate,” alisema Hoyce.


Aweza kufungwa miaka mitatu jela


Wakati mrembo aliyetawazwa kuwa malkia wa ulimbwende wa Tanzania 2014, Sitti Mtemvu akivua taji hilo, yuko katika hatari ya kufungwa miaka mitatu jela ikiwa atabainika kughushi vyeti vya kuzaliwa.

Meneja Mawasiliano na Masoko wa Wakala wa Udhamini na Ufilisi (RITA), Josephat Kimaro alisema jana kuwa, iwapo Sitti atabainika kughushi vyeti vya kuzaliwa anaweza kufungwa jela miaka mitatu kutokana na sheria ya usajili.

Kimaro alisema kifungu namba 28 (3) cha vizazi na vifo kinatoa adhabu hapo hapo kwa kusema uongo na kwa anayebainika kughushi vyeti. Kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Vizazi na Vifo sura ya 108 toleo la mwaka 200, ni kosa la jinai kutoa taarifa za uongo kwa msajili.

Kwa upande wake Msemaji wa Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi, (RITA) Jafari Malema alisema madai ya kughushi vyeti yanayotolewa dhidi ya Sitti ni sehemu ndogo ya changamoto ambazo wakala huo unakumbana nazo kwani wapo wengi wanaofanya hivyo.

Malema alisema RITA imekuwa ikiwachukulia hatua wale wote ambao wanafoji vyeti au kufanya jambo lolote kinyume na taratibu za wakala huo.

“Wapo wengi wanaoghushi vyeti si huyu tu anayetuhumiwa, ingawa sisi hatuna uhakika iwapo ameghushi au la, na iwapo tungethibitisha basi tungemchukulia hatua,” alisema.

Alisema RITA wameshindwa kufanya uamuzi wowote kwa sababu hawajaombwa kulifanyia uchunguzi sakata hilo la Miss Tanzania kudaiwa kughushi vyeti na iwapo wataambiwa basi watalifanyia uchunguzi na kutoa adhabu.

Hata hivyo, Malema alisema suala la Sitti limepelekwa kwa Mkurugenzi wa Rita, Philip Saliboko.

Wakati hayo yakiendelea, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema ikiwa Rita na Kampuni ya Lino International Agency ambao ni waandaaji wa Miss Tanzania wakiamua kumfungulia malalamiko aliyekuwa Miss Tanzania 2014 Sitti, atapandishwa kizimbani kwa kosa la kughushi cheti cha kuzaliwa.

Kova akizungumzia suala hilo jana, aliliambia gazeti hili kuwa Jeshi la Polisi haliwezi kuingia suala hilo mpaka litakapopokea malalamiko kutoka kwa wahusika.

Alisema suala hilo ni nyeti, lakini jeshi hilo haliwezi kuingilia mpaka taratibu hizo zitakapokamilika na iwapo watapewa taarifa rasmi na hapo ndipo watakapolifanyia kazi.

“Tunawasubiri walalamikaji waje kutupatia taarifa kuhusu kughushi na hapo ndipo sheria itachukua mkondo wake, lakini mpaka sasa jeshi la polisi halijapata taarifa zozote kutoka kwao, Rita au Lino Agency wakifungua mashtaka, tutaweza kuyashughulikia, lakini pia itategemea ni malalamiko gani,” alisema Kamanda Kova.

Hata hivyo, uwezekano wa Kampuni ya Lino Agency kufungua mashtaka ni mdogo kwani Mkurugenzi wake, Hashim Lundenga alisema jana kuwa, Sitti hakuvuliwa taji kwa kashfa ya kughushi vyeti bali aliamua kujivua mwenyewe kutokana na kuwapo kwa maneno mengi yanayomshutumu.

Alisema kuwa hali hiyo imemsababishia kukosa amani na kuhatarisha maisha yake na kuamua kuchukua uamuzi huo dhidi ya taji ambalo alishinda kwa kupitia kipaji chake.

Kashfa ya umri

Oktoba 17, 2014 zikiwa zimepita siku sita tu tangu Sitti Mtemvu alipotangazwa mshindi wa taji la Miss Tanzania, yalizuka malalamiko kadhaa kuwa ana umri mkubwa ambao hauendani na kanuni za kushiriki taji la dunia pamoja na kashfa ya kuwa na mtoto.

Hata hivyo, Oktoba 21 mrembo huyo akiwa ameambatana na waandaaji wa shindano hilo walikanusha tuhuma hizo sambamba na kuonyesha cheti cha kuzaliwa ambacho kilimwonyesha kuwa na miaka 23.

Hata hivyo, utata mkubwa ulitokana na tarehe ya kuzaliwa katika cheti hicho ambayo ni Mei 31, 1991, kutofautiana na tarehe ya kuzaliwa ambayo ipo kwenye hati ya kusafiria. Hati hiyo inasomeka kwamba Sitti ambaye pia alikuwa Miss Temeke 2014 alizaliwa 1989.

Baada ya shinikizo la muda mrefu, hatimaye jana, Novemba 8, 2014, ilitangazwa rasmi kwamba Sitti ameamua kuvua taji hilo kwa kuandika barua Novemba 5 mwaka huu, hivyo waandaaji kumvisha aliyekuwa mshindi wa pili, Lilian Kamazima.

Chanzo: Mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment