Wednesday, 19 November 2014

MAJURA: AZALIWA BARA NA KUFA ZANZIBAR

Idrissa Abdallah Majura
Idrisa Abdallah Majura



Siku ya leo, yaani tarehe 19.11. ni siku maalumu na ya kumbukumbu ulimwenguni kote kwa wapenda amani na maendeleo ya jamii, wapigania amani na haki za binadamu.

Ni siku ambayo alizaliwa mwanazuoni Idrissa Abdallah Majura, tarehe 19.11.1938 katika kijiji cha Gera, Mkoani Kagera nchini Tanzania. Ndugu Majura alikuwa miongoni mwa wanafunzi wachache toka Tanganyika wakati huo waliobahatika kupata scholarship ya kwenda masomoni huko Zanzibar.

Baada ya kufuzu masomo yake alitunukiwa shahada ya Elimu na kuwa mwalimu katika shule na vyuo mbalimbali Kisiwani Unguja. Mbali na uwanja wa Elimu Idrissa Majura alikuwa mwana michezo hodari aliyeichezea timu ya Taifa ya Zanzibar akiwa golikeeper mashuhuri wakati huo. Pia alikuwa mwanariadha hodari sana ambaye rekodi zake hazijavunjwa hadi leo!

Idrissa Majura alikuwa mpenzi wa watu wengi huko Kisiwani Unguja. Ingawa hakujihusisha na mambo ya kisiasa, kama wananchi wengine wa Zanzibar aliyaunga mkono mapinduzi yaliyomungòa Sulatani na kuleta uhuru kwa wananchi wote Visiwani. Watu wengi huko Unguja na Pemba walimpenda sana na alifahamiana na watu wa chini na wakuu pia. Ingawa aliishi muda mrefu huko Zanzibar, hakusahau nyumbani kwao huko Bukoba. 

Kila mara alikuwa akija likizo kuwaona wazazi wake, jamaa na ndugu zake. Alitoa misaada mingi kwa kuwasomesha wanafunzi wengi wa Mkoa wa Kagera na Tanzania kwa ujumla. Mnamo mwaka 1969 aliamua kufuta kazi na kurejea nyumbani ili awe karibu na wazazi wake waliokuwa wameanza kuzeeka. Ndipo balaa lilipomkuta muda mfupi baada ya kurejea nyumbani, akakamatwa kwa visingizio kuwa alishiriki kwenye njama za kutaka kuiangusha serikali ya Mapinduzi ya Abedi Amani Karume. 

Kwa sababu ambazo hazieleweki, Serikali ya Muungano ilikubali arejeshwe Zanzibar, ingawa ilijua wazi kuwa kufanya hivyo ilikuwa ni kumweka kitanzi, kama Wazanzibari wengine walivyouawa kwa ukatili wakati huo. Ni wazi kabisa kuwa Idrissa Majura hakuwa mwanasiasa na wala hakujihusisha na madai ya uongo yaliyotolewa kuwa alitaka kuipindua serikali ya mapinduzi. 

Wakati huo wa kutisha huko Visiwani, kila aliyekuwa na Elimu au kutoa kauli yoyote ya kumpinga Karume, hatima yake ilikuwa ni kukiona cha mtema kuni – yaani kifo au kifungo cha maisha. Mpaka leo haijulikani mwanazuoni huyo aliuawa vipi ? na kuzikwa wapi ? kwani hakufikishwa mahakamani ili ajitetee na kuhukumiwa. Vyombo vingi vya kimataifa vimeanza kuulizia suala hili na tuna imani siku itafika ambapo ukweli utajulikana.

Mola aiweke roho yake mahali Pema Peponi - Amin
Chanzo: wavuti.com

No comments:

Post a Comment