Thursday, 20 November 2014
WAANDISHI WA AL JAZEERA KUACHIWA MISRI?
Rais wa Misri amesema kuna uwezekano wa kutoa msamaha wa Rais kwa waandishi wa habari wa Al-Jazeera walioko gerezani tangu mwaka jana.
Abdel Fattah el-Sisi alisema kwenye mahojiano siku ya Alhamis, “ Tukiona kama haitoleta matatizo kwa usalama wa taifa la Misri, basi tutafanya hivyo.”
Msemaji wa Mtandao wa Habari wa Al Jazeera uliopo Doha alisema: "Mamlaka za Misri zina uwezo wa kuwaachia huru waandishi wetu wa habari. Ulimwengu unatarajia kuwa hatua hiyo itafanyika haraka, na kwa wote watatu kuachiwa huru.”
Sisi alitoa amri wiki iliyopita inayomruhusu kuwahamisha wafungwa wa kigeni, ikitoa imani kuwa waandishi hao wataachiwa huru.
Mohamed Fahmy, ambaye ni Mcanada na Mmisri, Peter Greste, raia wa Australia, na Baher Mohamed, raia wa Misri, wamefungwa Misri kwa siku 327, baada ya kutuhumiwa kimakosa na halafu kukutwa na hatia ya kuliunga mkono kundi la Muslim Brotherhood.
Waandishi hao wa habari wamekuwa wakisistiza mara kwa mara kuwa wameadhibiwa kwa kufanya kazi yao.
Chanzo: Al-Jazeera
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment