Wednesday 19 November 2014

'WATOTO' WARUSHIWA MABOMU YA MACHOZI MALAWI



File photo: Peter Mutharika
Peter Mutharika aliwaahidi Wamalawi maisha bora aliposhinda uchaguzi mwezi Mei

Polisi nchini Malawi wamerusha mabomu ya kutoa machozi kutawanya mamia ya wanafunzi wakiandamana kupinga kwa serikali kuchelewa kuwalipa walimu wao mishahara.

Wanafunzi hao, walio na umri kati ya sita na 12, walimimiminika katika mitaa ya mji mkuu, Blantyre.

Takriban walimu 6,500 katika shule za umma hawajalipwa tangu mwezi Mei, na takriban 1,000 wamegoma kuingia madarasani.

Wafadhili wa nchi za kimagharibi walipiga tanji misaada yenye thamani ya takriban dola milioni 150 baada ya serikali ya Malawi kukumbwa na kashfa kubwa ya ufisadi.

Utafiti wa kimahesabu uliofanyika mwaka jana uligundua kwamba takriban dola milioni 60 zilichomolewa kwenye mfuko wa serikali.

Takriban 40% ya bajeti ya Malawi hutoka kwa wafadhili.

"Tunataka rais ajue kuwa tumekasirika. Lazima awalipe walimu wetu ili turejee madarasani,” alisema mwanafunzi mmoja.

"Tunataka kuwa viongozi siku za usoni. Wasiharibu maisha yetu,” mwanafunzi mwengine alisema.

Rais Mutharika alikuwa mjini Zomba, mashariki mwa nchi hiyo akiwatuza stashahada na shahada wahitimu wa chuo kikuu.

Msemaji wa wizara ya Elimu Manfred Ndovi alithibitisha kuwa takriban walimu 6,600 hawakulipwa tangu mwezi Mei.

"Tunaangushwa na mchakato mzima kwani inahusisha ofisi za wilaya, hazina, na wizara yetu,” alieleza.

No comments:

Post a Comment