Saturday, 29 November 2014

MALAWI NA TANZANIA BADO ZAZOZANIA ZIWA NYASA



Kile kilichoonekana kuanza kama mzaha kati ya Tanzania na Malawi kuhusu umiliki wa Ziwa Nyasa, sasa kimeanza kuchukua sura mpya kwa kila nchi kuendelea kutekeleza kitu inachokiamini kuwa ni sahihi.

Baada ya kutokea vuta nikuvute kati ya nchi hizo mbili zilizokuwa marafiki wa miaka mingi, marais wastaafu kutoka Msumbiji, Joaquim Chissano, Festus Mogae wa Bostwana na Thabo Mbeki wa Afrika Kusini walipewa jukumu la kutafuta maridhiano.

Hivi karibuni marais hao walikutana na Rais Peter Mutharika kwa ajili ya kuzungumzia jambo hilo, lakini kwa bahati mbaya walichodhani kuwa ni jambo dogo, kiligeuka kuwa ‘mfupa mgumu’ baada ya rais huyo kusema Tanzania haimiliki hata inchi moja ya Ziwa Nyasa.

Kama hiyo haitoshi, Mutharika anasema kuwa msimamo wake hauwezi kubadilika kwa kuwa mipaka ya nchi hizo mbili iliwekwa na wakoloni na kuipa uhalali Malawi umiliki wa ziwa hilo.

Wakati hayo yakiendelea huko Malawi, hapa nchini Serikali inaendelea na mipango ya kuboresha miundombinu ndani ya ziwa hilo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa meli yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200.


Pia Serikali imeanza maandalizi ya kuweka umeme kwenye Bandari ya Kyela, unaofadhiliwa na Wakala wa Umeme Vijijini (Rea).

Alipotembelea maendeleo ya miradi hiyo hivi karibuni, kiongozi wa timu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Florence Mwanri alisema miradi hiyo itakapokamilika itahudumia wananchi wa Mbeya, mikoa ya jirani na nchi za Malawi, Zambia na Msumbiji.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Gazeti la Nyasa Times la Malawi, wananchi wa nchi hiyo wanatofautiana kuhusu msimamo wa Rais Mutharika kuwa Tanzania inalitumia ziwa hilo kinyume na sheria ya kikoloni iliyoweka mipaka.

Baadhi ya raia wa nchi hiyo wanamwona rais wao kama shujaa anayetetea hadharani maliasili za nchi yao, huku wengine wakiutazama msimamo wa Mutharika kama ni njia ya kuvuruga uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizo.

“Rais Mutharika ameongea sahihi, kwa sababu sheria zilizotumika kugawa mikapa ni za wakati wa ukoloni. Kinachotakiwa kwa Tanzania ni kutambua ukweli huo,” anasema Antipas Massawe.

Mwananchi huyo anaongeza kuwa: “Tanzania na Malawi haziwezi kutatua mgogoro huo kwa sababu wao siyo waliouleta.”

Zabweka Mambo anampongeza Rais Mutharika kwa msimamo wake, huku akiwaambia wananchi kuwa mvutano huo unatokana na Tanzania kutaka kuchimba mafuta kwenye Ziwa Nyasa.

“Tanzania ndiyo nchi pekee yenye Tanzanite duniani, lakini kitu cha ajabu wauzaji wakubwa wa madini hayo ni Afrika Kusini na India, kwa nini wasilalamikie madini yao kwanza?” anauliza Mambo.

Kwa upande wake, Alinane Chisinga amenukuliwa akihoji historia ya Tanzania na Mwalimu Nyerere alisemaje kuhusu mipaka ya nchi hizo mbili, akiamini kuwa jirani yao anajua historia yote kuhusu ziwa hilo.

Hata hivyo, George Lihoma anasema kuwa umefika wakati wa Malawi kuwa na bandari yake kwa kuwa iwapo Tanzania itashindwa kwenye mgogoro huo inaweza kusitisha biashara zinazofanyika baina ya nchi hizo.

Mwananchi aliyejitambulisha kwa jina moja la Kanonono anamuuliza Rais Mutharika harakati za kuchukua Ziwa Nyasa lote zitasaidiaje kuokoa thamani ya fedha yao (kwacha) inayoporomoka na kuifanya nchi kuwa ya tisa duniani kwa umaskini.

“Suala la mpaka litawasaidiaje walimu kuingiziwa fedha zao kwenye akaunti za benki?” anahoji.

Kwa upande wake Rais Mutharika anasema kuwa: “Kesi yetu kuhusu suala hili ipo wazi kabisa kwa mujibu wa Mkutano wa Helgoland wa 1896 na tamko la OAU (Umoja wa Afrika) la 1985.”

Anaongeza: “Nina ujasiri na matumaini kuwa kwa kupitia jitihada za usuluhishi zinazofanywa na Rais Chisano, Mogae na Thabo Mbeki zitasaidia kumalizika kwa suala hili.”

Rais Mutharika anawahakikishia raia wa nchi yake kwamba atarejea kwenye mazungumzo na Tanzania ili kufikia suluhisho kwa njia ya amani kwa faidia ya nchi zote mbili. Juni mwaka huu, rais huyo alimshutumu mtangulizi wake, Joyce Banda kwa madai kuwa alikuwa dhaifu kiasi cha kutoa fursa kwa Tanzania kutumia nafasi hiyo kutaka kupora ziwa lao.

“Ziwa hili letu, ila Tanzania inatumia tu udhaifu wa Serikali iliyopo kwani wenyewe wanajua ndani ya mioyo yao kuwa hawana chochote katika ziwa hilo. Tutakaporejea serikalini mwakani haya mambo yote yasiyo na kichwa tutayamaliza. Nataka niwahakikishie kwamba, tutapeleka meli zaidi kwenye ziwa hili ili kuinua shughuli zetu za kiuchumi na kutengeneza ajira kwa vijana wetu.”

Wakati hayo yakiendelea, wanasheria wa Rais Mutharika wanasema kuwa iwapo marais walioteuliwa kushughulikia suala hilo watashindwa kufikia mwafaka, Malawi inapaswa kuiburuza Tanzania katika Mahakama ya Kimataifa (ICJ).

Chanzo: Mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment