Thursday, 13 November 2014
DEWJI ATAJWA BILIONEA NAMBA MOJA TANZANIA
Ni mfanyabiashara kijana aliyekamata nafasi ya 24 katika orodha ya matajiri 55 wa Afrika.
Mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji (39), ametajwa kuwa ndiyo bilionea namba moja nchini kwa sasa, akifuatiwa na Rostam Aziz (49).
Kwa mujibu wa ripoti ya Jarida la Ventures Afrika lililotolewa jana, wafanyabiashara hao ndiyo Watanzania pekee waliongia kwenye orodha ya mabilionea 55 barani Afrika.
Dewji, ambaye pia ni mbunge wa Singida Mjini kwa tiketi ya CCM, ni mfanyabishara kijana aliyekamata nafasi ya 24 katika orodha hiyo akiwa na utajiri wa Dola 2 bilioni Marekani (Sh3 trilioni).
Nafasi hiyo inamfanya kijana huyo kutambulika kama tajiri namba moja nchini kwa sasa na siyo tena Rostam.
Katika orodha hiyo Dewji amemwacha Rostam kwa nafasi 16. Rostam anashika nafasi ya 40 akiwa na utajiri wa Dola 1.2 bilioni za Marekani.
Mwaka jana, Rostam alitajwa kuwa ndiye tajiri namba moja Tanzania. Hiyo ilikuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na jarida la Marekani la Forbes. Rostam alikamata nafasi hiyo na ya 27 katika Afrika akiwa na utajiri wa Dola 1 bilioni za Marekani (Sh1.6 trilioni).
Katika orodha hiyo, yumo pia Said Bakhresa ambaye aliwahi kutajwa siku za nyuma kuwa mmoja wa mabilionea wa Tanzania na Afrika.
Hata hivyo, ripoti ya jarida hilo ya mwaka 2011, ilimtaja Bakhresa kuwa ndiye aliyekuwa tajiri namba moja wa Tanzania. Bakhressa katika kipindi hicho alikadiriwa kuwa na utajiri wa Dola 620 milioni (Sh971 bilioni) akifuatiwa na Rostam, Mengi na mfanyabiashara mwingine maarufu, Ali Mufuruki.
Mengi alishikilia nafasi ya pili Tanzania na 34 Afrika akiwa na utajiri wa Dola 550 za Marekani (Sh861 bilioni).
Forbes ilionyesha kuwa Bakhresa alifungana na Mo katika nafasi ya tatu ya orodha ya matajiri wa Tanzania na ya 38 kwa Afrika. Wote walikuwa na utajiri wa Dola 500 milioni (Sh783 bilioni). Jarida hilo limemtaja pia tajiri kijana wa Nigeria mwenye umri sawa na Dewji, Igho Sanomi kuwa anashika nafasi ya 30 akimiliki Dola 1.3 bilioni.
Dewji:
Mafanikio yamekuja baada ya kuendeleza mali ya wazazi wake. Anafanya biashara ya nyumba, mazao na viwanda vya mafuta.
Dewji alirejea Tanzania baada ya kumaliza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Georgetown, Marekani na kuendeleza biashara ya maduka ambayo yalianzishwa na baba yake. Alinufaika baada ya kununua viwanda vilivyobinafsishwa na Serikali.
Alivifanya viwanda hivyo kutengeneza faida na kuinyanyua Kampuni ya Mohamed Enterprises (MeTL) kuwa miongoni mwa kampuni zenye mafanikio makubwa Tanzania.
Mo pia anajihusisha na biashara ya usambazaji bidhaa, viwanda vya nguo na kilimo.
Jarida hilo lilipiga hesabu za utajiri wa wafanyabiashara hao kwa kuangalia thamani ya bidhaa zinazouzwa na kampuni zao, mikataba yao na hasa wale walio kwenye sekta ya mafuta na ukubwa wa kampuni zao.
Rostam Aziz
Utajiri wa Rostam unachangiwa zaidi na biashara ya mawasiliano ya simu za mkononi, ujenzi na uchimbaji wa madini.
Anamiliki asilimia 35 ya hisa katika Kampuni ya Simu za mkononi ya Vodacom. Ni kampuni inayoongoza kwa biashara ya simu za mikononi nchini Tanzania ikiwa na wateja zaidi ya milioni 9.5.
Pia anamiliki Kampuni ya Caspian, ambayo inafanya kazi za kuchimba madini katika migodi inayomilikiwa na Kampuni za BHP Billiton na Barrick Gold.
Rostam pia anamiliki hisa katika Kampuni ya Hutchison Wampoa inayofanya kazi za kupakua mizigo bandarini na anamiliki nyumba kadhaa nchini na Afrika Mashariki ya Kati.
Chanzo: Mwananchi.co.tz
Labels:
Makala
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment