Tuesday, 25 November 2014

WAKILI MAARUFU ASIMULIA MKASA WAKE WA 'SUMU'

Mbunge wa Musoma Vijijini na pia wakili maarufu Tanzania, Nimrod Mkono

Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono ambaye hivi karibuni alinusurika kifo akidaiwa kulishwa sumu akiwa London, Uingereza amesimulia jinsi tukio hilo lilivyomkuta.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkono alisema endapo uchunguzi wa suala hilo utakamilika na kuthibitisha kwamba alilishwa sumu, atapambana na wahusika kwa kuwa wamehatarisha maisha yake.

Mkono ambaye pia ni wakili maarufu nchini, alitoa kauli hizo jijini hapa jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuelezea mwenendo wa afya yake.

Alidai kwamba, lengo la kumlisha sumu ni kuharibu figo zake ndani ya saa 72 wakati alipokuwa katika ziara ya nchini humo.

“Niko vizuri na afya njema… kama kuna mtu anawinda jimbo langu mwambieni ameshindwa na wananchi wangu nawaeleza kuwa niko salama wasiwe na hofu. Ninataka kujua nani kanilisha sumu na kwa nini?” alisema Mkono.

Akisimulia tukio hilo alisema, Novemba 11 akiwa miongoni mwa wajumbe 11 wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, walisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Uingereza akiwa salama salimini.


Aliwataja baadhi ya wabunge walioambatana nao kuwa ni William Ngeleja (Mwenyekiti wa kamati hiyo), Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika.

“Tukiwa uwanja wa ndege nilipokea ujumbe mfupi wa maandishi (hakutaka kuuweka wazi kwa sababu upelelezi haujakamilika), ukinitahadharisha kuwa makini, ujumbe ule ulinishtua kwa kweli.”

“Niliwaonyesha wenzangu niliokuwa nao na pale tulikunywa chai kabla ya kuondoka na tulipofika kule mimi nilikaa hoteli yangu na wenzangu wakakaa ya kwao,” alisema.

Huku akisimama na kunyoosha mikono kuonyesha yuko vizuri, Mkono alisema siku iliyofuata ratiba iliwataka kuhudhuria Bunge la Uingereza.

“Niliamka na kwenda Ubalozi wetu na kwa kuwa tulitakiwa kufika bungeni saa 5.00 asubuhi, niliwahi na wenzangu na walipokuja tuliungana… tulipokuwa ndani katika Bunge la Uingereza, ghafla nilianza kujisikia vibaya hali iliyonisababisha nipoteze fahamu kwa saa sita. “Lakini kabla ya kupoteza fahamu niliwaeleza wanipeleke nyumbani (Tanzania), wenzangu wanasema nilikuwa napiga kelele, nirudisheni hawa wanataka kuniua,” alisema Mkono kwa sauti ya chini na kuongeza:

“Hapa nasimuliwa sasa kuwa walinipeleka hospitalini na waliponifikisha madaktari wa pale waliamua kuwasiliana kwanza na Daktari wangu, (Lusangulila Kapitain) ili kujua kama wakati natoka Tanzania nilikuwa na tatizo.”

Alisema, “Kapitain baada ya kuelezwa hali niliyonayo naye aliwaeleza kuwa huyo (Mkono) atakuwa amelishwa sumu kwani wakati anatoka huku alikuwa salama kabisa na akawaomba wanipatie dawa ambazo zilinirejesha katika hali yangu ya kawaida kuanzia saa 12 hadi saa moja jioni.”

Mkono alisema kitu ambacho hadi sasa hajakielewa na anapenda kukifahamu ni kwa nini na malengo yapi akisema kama ni sakata la escrow lilikuwa wazi bila kificho.

“Serikali ilikuwa ni mteja wangu katika kesi kati ya Tanesco na IPTL… nikiwa bungeni siwezi kuongea hadi nipate kibali cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutokana na maadili ya kazi zetu, lakini uchunguzi ukibainika kwamba nililishwa sumu kwa sababu hiyo nitaweka kando maadili ya kazi.”



Chanzo: mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment