Monday, 3 November 2014

UWANJA WA NDEGE WA DAR 'WASHIKA MKIA'

 

Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Moses Malaki amesema uwanja wake umechakaa kiasi cha kukosa sifa za kuwa uwanja wa kisasa barani Afrika na dunia.

Kauli ya Malaki imekuja baada ya ripoti ya matokeo ya utafiti wa mtandao wa Sleeping in Airport uliyofanywa 2014 kuonyesha kuwa JNIA inashika nafasi ya nne kwa viwanja duni Afrika.

“Huo ni ukweli usiopingika kwa sababu uwanja ulijengwa zamani na miundombinu yake haikidhi mahitaji ya sasa…. hali ni mbaya,” alisema Malaki.

“Kiwanja kinakabiliwa na tatizo la miundombinu chakavu, vyoo visivyotosheleza na wakati huohuo kuzidiwa na wingi wa abiria, jambo linalosababisha huduma zake kuwa chini ya kiwango.

“Hatuwezi kuwa bora kwa uwanja huu… hebu fikiria uwanja uliojengwa kuhudumia watu milioni 1.2 kwa mwaka, sasa unahudumia watu 2.5 milioni, hapa lazima huduma zitakuwa chini ya kiwango na msongamo utakuwa mkubwa.”

Alisema katika kukabiliana na changamoto ya msongamano, ofisi yake iko katika hatua za kuongeza vizimba vya kugongea hati za kusafiria kutoka saba vya sasa na kuwa 21.

Alisema tayari wameshazungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani kwa ajili ya kuongeza wafanyakazi, pia kuunganisha na kuwa sehemu moja kwa mlango wa abiria wanaowasili na wa ndani, kazi itakayokamilika wiki mbili zijazo.


Utafiti

Utafiti wa Sleeping in Airport ulitokana na maoni ya wasafiri waliopitia uwanja huo ambao walielezea na kupiga kura kuhusu huduma, miundombinu na uwezo wa viwanja hivyo kutumika kama eneo la kulala wasafiri inapobidi.

Nafasi ya kwanza kwa uduni ilishikwa na uwanja wa kimataifa wa Khartoum, Sudan ukifuatiwa na N’dijili, Kinshasa DRC na Tripoli Libya nafasi ya tatu.

Katika taarifa yake, mtandao huo ulisema Afrika ina sifa ya kuwa na viwanja vingi vyenye sifa mbaya duniani, ikiwemo uchafu wa sakafu, vyoo, vitendo vya rushwa, ukosefu wa viyoyozi licha ya joto kali, migahawa ya kawaida lakini ghali na michakato ya usalama inayotia shaka.

Chanzo: mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment