Thursday, 2 April 2015

KATIBA MPYA TZ: HAKUNA KURA YA MAONI APRILI 30

Mwenyekiti wa Nec Jaji Mstaafu Damian Lubuva

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imekubali kuahirisha upigiaji Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa iliyopangwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu kutokana na kutokamilika kwa uandikishaji wa Daftrai la kudumu la wapiga kura kwa kutumia teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR).

Hatua hiyo inakuja baada ya kuwepo mfululizo wa matamko na ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali wa demokrasia kwamba zoezi hilo lisingewezekana kwa sasa hasa kutokana kusuasua kwa mwenendo wa BVR.

Mwenyekiti wa Nec Jaji Mstaafu Damian Lubuva aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuwa kazi ya uboreshaji daftari la wapiga kura ni ya msingi kabla ya taratibu zote za upigaji kura.

Jaji Lubuva aliyeonekana kuwa mpole zaidi, alisema kwa uzoefu walioupata Njombe, zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura bado halijakamilika katika mkoa huo na mingine iliyosalia.

“Hivyo tume haitaweza kuendelea na zoezi la upigaji kura ya maoni na zoezi hilo lililotangazwa hapo awali kufanyika Aprili 30, 2015 limeahirishwa hadi tarehe itakapotangazwa na Nec baada ya kushauriana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar,” alisema Jaji Lubuva.

Kwa nyakati tofauti, vyama vya siasa, asasi za kiraia, taasisi za kidini na wananchi wamekuwa wakiishauri Nec kuahirisha Kura ya Maoni huku vyama vya siasa vikimtaka Rais Jakaya Kikwete atii makubaliano yaliyofikiwa na Kituo cha Demokrasia (TCD) mwaka jana ya kuahirisha zoezi hilo hadi baada ya Uchaguzi mkuu.

Jaji Lubuva alisema kuwa tume yake inaendelea kuboresha daftari la wapiga kura nchi nzima ambapo wanatarajia kukamilisha ifikapo Julai mwaka huu. Nec ilieleza kuwa baada ya kumaliza uandikishaji mkoani Njombe watahamia mikoa ya Ruvuma, Lindi, Mtwara na Iringa.

Chanzo: mwananchi.co.tz

SHAMBULIO LA CHUO KIKUU KENYA 'LAUA 147'



A Kenyan soldier escorts a woman after she was rescued

Idadi ya watu waliouawa katika shambulio lililofanywa na al-Shabab kwenye chuo kikuu kaskazini-mashariki mwa Kenya imeongezeka kufikia 147, maafisa wa serikali walisema.

Harakati za kijeshi za kudhibiti chuo kikuu cha Garissa sasa zimekwisha, huku washambuliaji wote wanne wakiwa wameuawa, walisema.

Maafisa walisema wanafunzi 587 walitolewa, 79 wakiwa wamejeruhiwa.

Sheria ya kupigwa marufuku kutoka usiku inatekelezwa katika baadhi ya sehemu nchini humo.

Kaunti nne katika mpaka wa Kenya-Somalia, Garissa, Wajir, Mandera na Tana River, wamezuia watu kutoka nje siku nzima.

Wanafunzi tisa waliojeruhiwa vibaya sana walisafirishwa kwa ndege kwenye mji mkuu Nairobi kwa matibabu.

Kwa maelezo zaidi, bonyeza link ifuatayo
http://bbc.in/1DrBXQW

CHUO KIKUU KENYA CHASHAMBULIWA



Map showing Garissa in Kenya

Watu wenye silaha waliovaa barakoa wamevamia chuo kikuu kimoja karibu na mpaka wa Somalia kaskazini-mashariki mwa Kenya, wakiua watu wawili na kujeruhi takriban 30.

Majeshi yamezunguka chuo kikuu cha Garissa na kujaribu kupambana na washambuliaji.

Walioshuhudia walizungumzia watu hao wenye silaha wakifyatua risasi ovyo bila kujali ni nani na hivyo kuhofiwa kuwa idadi ya waliokufa inaweza kuongezeka.

Haiko wazi nani anahusika na shambulio hilo, lakini wapiganaji wa al-Shabab wamekuwa wakiishambulia Kenya mara kwa mara.

Garissa na maeneo mengine ya mpakani yamekuwa yakishambuliwa mara nyingi.