Monday, 8 September 2014

CHANJO YAWAPA NYANI KINGA YA EBOLA




First patient

Nyani waliopewa chanjo wameonekana kuwa na kinga “ya muda mrefu” dhidi vya virusi vya Ebola, ikitoa matumaini ya kuwepo mafanikio akijaribiwa mwanadamu, wanasayansi wanasema.

Majaribio hayo yliyofanywa na Idara za Taifa za Afya za Marekani zimeonyesha kinga hiyo huweza kudumu kwa takriban miezi 10.

Majaribio ya chanjo hiyo kwa binadamu yameanza wiki hii Marekani na itafanyiwa pia Uingereza na barani Afrika.

Shirika la Afya Duniani WHO linasema zaidi ya watu 2,000 sasa wamefariki dunia kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo Afrika magharibi.

Majaribio chungu nzima ya tiba yanafanyiwa kazi kusaidia kuzuia kusambaa kwa Ebola.

Hii ni pamoja na chanjo inayotengenezwa na Idara ya Marekani inayoshughulikia magonjwa ya kuambukiza pamoja na kampuni ya dawa ya GlaxoSmithKline.

Inatumia kirusi kilichotengenezwa kwa asida nasaba za nyani zenye kutoka kwenye wanyama wenye Ebola Zaire, ambayo ndiyo iliyoenea Afrika magharibi, na ile inayojulikana zaidi iitwayo Sudan.

Chanjo ya kirusi hicho haijizalishi ndani ya mwili, lakini matumaini ni kuwa mfumo wa kinga utapambana na virusi vya Ebola ya chanjo hiyo na kujenga kinga.

Chanzo:  BBC
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu

Sunday, 7 September 2014

KENYA YA 4 KWA MAAMBUKIZI YA UKIMWI DUNIANI



Kenya ni nchi ya nne yenye idadi kubwa ya watu walioathirika na virusi vya ukimwi duniani. Kusambaa kwa virusi vya HIV nchini humo imefikia watu milioni 1.6, Wizara ya afya imesema.

Afrika Kusini, inaongoza kwa watu milioni 5.6 walioambukizwa ukimwi, ikifuatiwa na Nigeria (milioni 3.3) na India (milioni 2.4), kulingana na takwimu kutoka UNAIDS na shirika la Afya Duniani (WHO).

Takriban watu 191,840 wanaoishi na virusi vya ukimwi nchini Kenya ni watoto. Inakisiwa watu 58,465 walifariki dunia kutokana na maradhi yanayohusiana na ukimwi mwaka 2013.

Ripoti mpya, ‘The National HIV and Aids Estimates’, iliyozinduliwa hivi karibuni na waziri wa mambo ya afya James Macharia amesema kuna takriban maambukizi mapya 100,000 nchini Kenya kwa mwaka.

Bwana Macharia ametoa wito wa jitihada za ziada, itakayowahusisha wadau wote, ili kupambana na janga hilo.

Kenya itahitaji takriban shilingi trilioni 75 ifikapo 2030 kuzuia takriban maambukizi mapya milioni 1.5, ripoti hiyo inasema.

Wizara ya fedha imeweka shilingi milioni 670 katika Baraza la Taifa la Kudhibiti Ukimwi katika bajeti ya 2014/2015.

Kati ya mwaka 2009 na 2013, matumizi ya kupambana na ukimwi nchini Kenya imeongezeka kutoka shilingi bilioni 63 hadi shilingi bilioni 72.

“Kukiwa na bajeti ya shilingi bilioni 11.7 kwa mwaka, Kenya itapunguza idadi ya maambukizi mapya kwa asilimia 66,” ripoti hiyo inasema.

Ripoti hiyo inapendekeza njia kadhaa za kupunguza maambukzi ikiwepo wanaume kujitolea kutahiriwa, kutumia dawa za kufubaza virusi ARV, kubadili tabia na kusambaza kondomu kwa nia ya kupambana na virusi hivyo.

Imeelezea pia wapenzi ambao mmoja anao na mwengine hana virusi hivyo, machangudoa, wapenzi wa jinsia moja, watumiaji dawa za kulevya, wafungwa, wanajeshi na maaskari, madereva wa malori, miongoni mwao, ndio wapewe kipaumbele katika kupambana na maradhi hayo.

Chanzo: The Citizen, Tanzania
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu

SARAFU YA 500 YAANZA KUTUMIKA OKTOBA TANZANIA

 
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgyS8PeLJN3T7aqfIw73pQG1uECkew4oAzOXFk94XdoSSqpuJqse5bG0i9O8ZScqKhVZ490BbNSD6es1yBty229XcC50z5v0gw_H-2HKzN7xIhAAPZCNpmGs3SBKsHRMOm7PTEZoJHlSG3g/s1600/IMG-20140907-WA0001.jpg 
Benki Kuu ya Tanzania ndiyo chombo chenye jukumu la kutoa sarafu na noti halali (legal tender) zinazotumika nchini. Katika kutekeleza jukumu hili Benki Kuu hutengeneza noti na sarafu zenye uwiano mzuri wa thamani (denominations) unaozingatia uwezekano wa zile zenye thamani kubwa kuweza kugawika katika zile zenye thamani ndogo ndogo.  
Hii hulenga kurahisisha upatikanaji wa chenji na uwezekano wa wahitaji wa viwango mbalimbali vya bidhaa na huduma  kupata katika mafungu yatakayokidhi mahitaji yao.  
 
Katika kutekeleza jukumu hili, Benki Kuu imetoa toleo jipya la Sarafu ya Shilingi 500. Hatua hii imezingatia yafuatayo:  
•  kwamba noti ya shilingi mia tano (500), ndiyo inayotumika zaidi kwenye manunuzi ya kawaida ya kila siku ya wananchi wengi kuliko noti nyingine yoyote. Hivyo noti hiyo hupita kwenye mikono ya watu wengi katika kipindi cha muda mfupi sana na kuchakaa haraka.  
 
•  Noti hizi hukaa katika mzunguko kwa muda mrefu bila kurejeshwa kwenye mabenki kwa wakati muafaka ili zibadilishwe zinapokuwa zimefikia ukomo wake.  
•  Sarafu hukaa kwenye mzunguko kwa miaka mingi zaidi kuliko noti.  
 
Sarafu hii inatambuliwa kwa kuangalia yafuatayo: 
•  Umbo lake ni la duara lenye michirizi pembezoni, kipenyo cha milimita 27.5 na uzito wa gramu 9.5  
•  Ina rangi ya fedha na imetengenezwa kwa madini aina ya chuma (Steel) na “Nickel”  
•  Kwa mbele ina sura ya Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Sheikh Abeid Aman Karume na kwa nyuma ina taswira ya mnyama nyati akiwa mbugani. 
•  Ina alama maalum ya usalama iitwayo “latent image” iliyopo upande wa nyuma  ambayo ni kivuli kilichojificha. Kivuli hiki huonesha thamani ya sarafu ‘500’ au neno ‘BOT’ inapogeuzwa-geuzwa. 
 
Sarafu hii mpya ya shilingi mia tano (500) inatarajiwa kuingizwa kwenye mzunguko kuanzia mwezi  Oktoba 2014.  Sarafu hii, itakuwa ikitumika sambamba na noti zilizopo sasa za shilingi mia tano mpaka hapo noti hizo zitakapokwisha katika mzunguko.  Pamoja na taarifa hii; tunawaomba wananchi kuendelea kufuatilia vipindi mbalimbali vitakavyokuwa vinaeleza jinsi sarafu hii ilivyo na namna ya kutunza noti na sarafu zetu kwa njia salama. 

 
Chanzo: michuzi.blogspot.co.uk

WATOTO KUFIKIA BILIONI 1 AFRIKA IFIKAPO 2050

Itakapotimia karne nyingine, watu wanne kati ya kumi duniani watakuwa Waafrika, Unicef says
Itakapotimia karne nyingine, watu wanne kati ya kumi duniani watakuwa Waafrika, Unicef
Idadi ya Waafrika wa chini ya umri wa miaka 18 itaongezeka kwa robo tatu na kufikia takriban bilioni moja ifikapo mwaka 2050, kulingana na ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa.

Utafiti huo unaonyesha “mabadiliko makubwa katika idadi ya watoto duniani barani Afrika”, inasema ripoti hiyo.

Ugunduzi wake unaonyesha ifikapo 2050, takriban 40% ya watoto wote watatoka Afrika, mpaka 10% mwaka 1950.

Hiyo ni licha ya idadi ya vifo barani Afrika kubaki juu, inasema ripoti hiyo.

Bara hilo kwa sasa linashuhudia karibu nusu ya vifo vya watoto duniani na huenda ikaongezeka kwa 70% ifikapo mwaka 2050, kulingana na ripoti kuhusu Afrika iitwayo Generation 2030 iliyotolewa na shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, Unicef.

Mtikisiko wa takwimu
Hatahivyo, kuongezeka kwa uzazi na ongezeko la idadi ya wanawake walio na uwezo wa kuzaa kunamaanisha katika kipindi cha miaka 35 ijayo, takriban watoto bilioni mbili watazaliwa Afrika na idadi ya watu barani humo itaongezeka mara dufu, inasema ripoti hiyo.

Nchi ya kuangaliwa kwa makini zaidi ni Nigeria. Nchi yenye idadi ya watu wengi zaidi barani Afrika , na ambayo tayari ina idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa, na moja kati ya 10 duniani ifikapo 2050 watazaliwa nchini humo, kulingana na ripoti hiyo.

Nigeria ina idadi ya watu wengi barani Afrika ikikadiriwa kuwa na watu milioni 166.6
Nigeria ina idadi ya watu wengi barani Afrika ikikadiriwa kuwa na watu milioni 166.6


 Idadi ya watu barani Afrika:
  • 1950: 9%
  • 2015: 16%
  • 2050: 25%
  • 2100: 39%
Chanzo: Umoja wa Mataifa

"Ripoti hii lazima iwe chachu ya mjadala duniani, kitaifa na kimataifa juu ya watoto wa Afrika," amesema Leila Gharagozloo-Pakkala, Mkurugenzi wa Unicef wa eneo la mashariki na kusini mwa Afrika.

"Kwa kuwekeza kwa watoto sasa- kwenye afya zao, elimu na usalama – Afrika inatakiwa kutambua faida za kiuchumi walizopata maeneo mengine zilizopitia mabadiliko kama haya,” amesema.

Imetafsiriwa na mwandishi wetu



TOTO TUNDU - KANSIIME

Vimbwanga vya WhatsAapp

TANZANIA YA 8 DUNIANI KWA KUJIUA?


Wakati imethibitishwa kwamba katika kila sekunde 40 mtu mmoja duniani huamua kukatisha maisha yake kwa sababu ambazo zinaweza kuzuilika, Tanzania imeelezwa kuwa ya nane katika orodha ya nchi zinazoongoza kwa watu wake kujiua.

Ingawa Jeshi la Polisi nchini lilipotakiwa kuzungumzia suala hilo lilionekana kuchukua mlolongo mrefu, utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO), umesema tabia ya watu kuficha takwimu na kufuatilia matukio ya vifo inachelewesha uchukuaji hatua wa kudhibiti tabia hiyo ya kujiua.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bukumbi juzi alipotakiwa kuthibitisha kwa takwimu kuhusiana na utafiti
huo wa WHO, sababu za kujiua na hata mikoa inayoongoza kwa matukio ya aina hiyo nchini, alitaka mwandishi wa habari hizi kumtumia maswali ili yafanyiwe kazi kuanzia wiki ijayo.

Utafiti uliofanywa na WHO na kutolewa kama Taarifa na Umoja wa Mataifa juzi, unaonesha kwamba tatizo la kujiua halitiliwi maanani wala kujadiliwa kutokana na kunyanyapaliwa na kuwepo kwa imani potofu zinazohusishwa na vifo hivyo.

Katika utafiti uliotolewa wiki tatu baada ya mmoja wa wakali wa Hollywood Robin Williams kujiua, pia waandishi wa habari wameonywa dhidi ya kuelezea kinagaubaga vifo hivyo kutokana na hatari ya watu wengine kunakili tabia na maamuzi hayo kwa jinsi yalivyoelezwa na vyombo vya habari.

WHO, ambayo imesema kwamba kujitwalia maisha binafsi ni tatizo kubwa la kiafya duniani kwa sasa linalohitaji hatua madhubuti kuchukuliwa dhidi yake imetoa taarifa hiyo baada ya kufanya uchunguzi katika nchi 172 duniani.

Imesema katika mwaka 2012 nchi zenye kipato kikubwa ziliongoza kwa mauaji ya aina hiyo ikiwa na vifo asilimia 12.7 kwa kila watu 100,000 huku nchi za kipato cha chini na kati zikiwa ni asilimia 11.2 kwa kila watu 100,000.

Chanzo: wavuti.com

Saturday, 6 September 2014

AL-SHABAB WATAJA KIONGOZI WAO MPYA



Al-Shabab, kundi la Kisomali, limemtaja Sheikh Ahmad Umar, ambaye pia anajulikana kwa jina la Abu Unaidah, kuwa mrithi wa Ahmed Abdi Godane aliyeuawa na shambulio la ndege siku ya Jumanne.

Kundi hilo siku ya Jumamosi waliahidi kulipiza kisasi kwa mauaji ya miongoni mwa viongozi wao waasisi.

“Kulipiza kisasi kwa vifo vya wasomi na viongozi wetu ni wajibu ambao hatutokata tamaa wala kusahau hata ichukue muda gani,” kundi hilo lilisema katika taarifa waliyoitumia Al Jazeera.

Omar, kiongozi wa tatu wa kundi hilo, anachukua nafasi ya Godane, ambaye alimrithi kamanda Ismail Arale.

Arale alifungwa Guantanamo Bay mwaka 2007.

Kundi hilo pia limethibitisha vifo vya maafisa wengine wawili ambao hawakuwataja majina

Mwaka 2012 Marekani ilitangaza kumzawadia dola za kimarekani milioni 7 kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kumkamata au kumwuua Godane.

Siku ya Ijumaa, Rais Hassan Sheikh Mohamed alitangaza msamaha wa siku 45 kwa wapiganaji ambao wako tayari kuachana na al-Shabab.

Godane, anayejulikana pia kwa jina la Abu Zubeyr, alipanda vyeo vya juu vya kundi hilo linalohusishwa na al-Qaeda mwaka 2008 kufuatia kifo cha mrithi wake Aden Hashi Ayro katika shambulio la anga la Marekani mjini Dhusamareeb kusini mwa nchi hiyo.

Imetafsiriwa na Mwandishi wetu

ZANZIBAR ILIVYOPAKWA MATOPE YA UGAIDI


SIKU hizi Zanzibar inaanza kunuka mbele ya taasisi za kimataifa zenye kushughulika na mambo ya ugaidi.

Hayo ni matokeo ya vitimbi vya duru fulani ndani ya Tanzania kwenyewe vya kuipaka Zanzibar matope kuwa ni visiwa vyenye kuufuga ugaidi wa kimataifa.

Duru hizo zimekuwa mbioni kwa muda sasa zikijaribu “kuthibitisha” kuwa Zanzibar imeingiliwa na magaidi wenye fungamano na mtandao wa kimataifa wa al-Qa’eda.

Hadi sasa jitihada zao hazikufanikiwa na, kwa hakika, kuna wachambuzi wenye kuamini kwamba hakuna cha kuthibitisha.

Hoja yao ni kwamba duru hizo zinaisingizia tu Zanzibar kwa lengo la kisiasa.

Wanasema kwamba lengo lenyewe hasa ni kulitia sumu na hatimaye kuliua lile vuguvugu lenye kuitetea haki ya Zanzibar ya kurejeshewa mamlaka yake kamili ya utawala.

Hoja kama hiyo ilitolewa karibuni kwenye Mahakama ya Kisutu na mmoja wa mashekhe wa Jumuiya ya Uamsho wanaoshtakiwa kwa makosa mbalimbali yenye kuhusika na ugaidi.

Sheikh Farid Hadi Ahmed alidai kwamba sababu iliyowachongea wakamatwe Zanzibar na wapelekwe kushtakiwa Dar es Salaam ni msimamo wao wa kuupinga Muungano wa Tanzania.

Kwa vile kesi hiyo iko mahakamani haitujuzu kusema chochote kuhusu mashtaka ya ugaidi yanayowakabili washtakiwa hao. Sheria lakini haituzuii kukumbusha kwamba ijapokuwa mashtaka ya ugaidi ni nyeti na ingawa wengi wetu tunaupinga na kuulaani ugaidi, hata hivyo, mahakama lazima ihakikishe kwamba washtakiwa wanaokabiliwa na mashtaka kama hayo hawanyimwi haki zao za kisheria na kwamba haki zao za kimsingi hazikiukwi.

Chanzo: Raia Mwema, Tanzania

KWANINI WANAUME HULIPIA NGONO?

pay 4 sex pix

Kuna mtazamo tofauti sana kwa wanaume wanaowafuata machangudoa. Lakini wanajieleza vipi kuhusu kulipa kwasababu ya ngono?

Fred na Laura hufanya matembezi, wakati wa weekend hushinda pamoja, huenda sokoni pamoja na aghlabu hula chakula pamoja.

Watazungumza na kucheka kwa vitu walivyoona kwenye televisheni. Lakini pia hugombana.
Jikoni kwa Fred, wakati anaandaa chakula cha usiku, Laura hukaa na kuchekacheka, akikiri kuwa bora si yeye anapika.

Kama wapendanao wowote, wana siku za raha na za maudhi pia. Lakini hawa si wapendanao wa kawaida.

Fred anamlipa Laura ili ashinde naye, na kufanya naye ngono pia.

Wamekuwa katika mpango huo kwa miaka sita.

Mjadala wa iwapo kuna tatizo kulipia ngono, na je ihalalishwe, bado ni motomoto na hamna jibu kamili.

Pamoja na malumbano hayo, swali moja si kawaida kuulizwa – kitu gani huwavuta wanaume kuwalipa wanawake kulala nao?

“Mara ya kwanza tulikutana kwenye mtandao,” anasema Fred ambaye sasa amestaafu, “na nikamwuuliza kama angependa kuwa nami hotelini usiku mzima.”

Anasema ilikuwa kama wapenzi wakikutana mara ya kwanza, “tulitaka kujuana kwanza.”

“Sasahivi tunajuana sana, yaani mno, kiasi ambacho Fred huingiza tu pesa kwenye akaunti yangu kupitia mtandao kabla sijaenda kumwona,” anasema Laura.

Fred anaishi kijijini na kwa miaka mingi amekuwa akimtunza mama yake. Anasema hakupata nafasi ya kukutana na watu kwahiyo akaamua kulipia ngono.

"Kusema ukweli haikuwa sana kuhusu ngono, zaidi ilikuwa kuwa karibu tu na mwanamke, na kama hutoki ukajichanganya na watu basi ni vigumu sana kufikiria utapataji hayo yote."
Baadhi hutaka tu kuwa karibu na mwanamke na wali si suala la ngono yenyewe
Baadhi hutaka tu kuwa karibu na mwanamke na wala si suala la ngono lenyewe
Robert amekuwa kwenye ndoa kwa miaka mingi.
“Niliishia kuwa mwanamme ninayependa sana kufanya mapenzi ambaye nilioa mwanamke ambaye havutiwi kabisa na hilo – au hata kukumbatiwa, kubusiana na mengineyo.

"Ni mtu mwema, tena mwema sana. Kwa mambo mengine yote tunapatana sana, lakini si kitandani.”

 Robert atadunduliza pesa chungu nzima ili tu aweze kulipia ngono.

“Nilitaka kudumisha ndoa yangu,” anasema, “Nilitaka nifanye yote sahihi kwa mke wangu, kwahiyo suluhu nilioiona ni kulipia ngono.”

Dhana ya kwamba binadamu anaweza kuuzwa kimaadili bado inaleta utata. Wakati machangudoa husema hawauzi miili yao, lakini kama wafanyakazi wengine, wanauza vipaji na ujuzi wao. Wanasema uchangudoa usingekuwa uhalifu na si jambo la kunyanyapaliwa, basi matatizo mengi yangetoweka.

Chanzo: BBC
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu

UNAPOPANDA LIFTI LENYE JENEZA

Vimbwanga vya WhatsApp

MIL 10 KUSAKA AJIRA IFIKAPO 2020, UGANDA

Wengi wasiokuwa na ajira hujikuta hawana la kufanya
Wengi wasiokuwa na ajira hujikuta hawana la kufanya
Idadi ya Waganda wanaotafuta ajira inaweza kuongezeka hadi milioni 10 mwaka 2020, jambo linaloshinikiza kubuniwa kwa ajira mpya na jaribio la kufanikisha usawa kwenye uchumi, kulingana na ripoti ya Benki ya Dunia.
Ripoti hiyo yenye kichwa cha habari Ajira, imeleeza, “Uganda inazidi kukabiliwa na changamoto za kuajiri vijana wake wanaoongezeka na hasa walio mijini, na pia wasomi.

Ripoti hiyo ya Benki ya Dunia inaendana sawia na utafiti wa mwaka 2013 uliofanywa na wizara ya Kazi na Elimu ya nchi hiyo iliyogundua kuwa kati ya wahitimu takriban 400,000 wanaomaliza taasisi za mafunzo kila mwaka, chini ya 100,000 ndio hufanikiwa kupata ajira.

Idadi ya watu kwa sasa Uganda inakadiriwa kufikia milioni 34 ambapo itaongezeka hadi milioni 42 ifikapo mwaka 2020.

Bwana Paul Lukema, Mtafiti kutoka kituo cha Utafiti wa Sera za Kiuchumi, anasema suluhisho la muda mfupi ni kuwekeza zaidi kwenye kilimo lakini wakati huo huo serikali iangalie zaidi namna ya kuendeleza viwanda.

“Uganda inatakiwa kubuni takriban ajira 400,000 kwa mwaka ambapo ni nafasi za ajira milioni 2 kila miaka mitano. Japo kilimo huajiri zaidi ya asilimia 65 ya idadi ya watu wote hapa nchini, kumekuwa na mageuzi ambapo vijana wanahama kutoka vijijini kuelekea mijini hivyo ajira huhama kutoka kilimo kwenda sekta nyingine,” Alisema Bwana Lukema.

Hata hivyo, si habari mbaya tu zilizotolewa kwa nchi hiyo ya Uganda, Benki ya Dunia imeongeza kwenye ripoti yake kuwa marekebisho yanayoendelea katika sekta ya elimu inamaanisha ifikapo mwaka 2020, takriban asilimia 50 ya watu wa Uganda watakuwa angalau wamepata elimu ya msingi.

Chanzo: Sunday Monitor, Uganda
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu

KIONGOZI WA AL-SHABAB, GODANE AUAWA



Ahmed Abdi Godane - undated photo
Mpango wa sheria wa Marekani ulitoa picha hii ya Godane mwaka 2012
 Kiongozi wa kundi la kisomali la al-Shabab, Ahmed Abdi Godane, ameuawa kufuatia shambulio la Marekani wiki hii.

Marekani ilifanya mashambulio ya anga siku ya Jumatatu na kubomoa gari na makazi ya muda kusini mwa mji mkuu wa nchi hiyo.

Rais wa Somalia alitoa taarifa siku ya Ijumaa na kuwasihi wapiganaji kuleta amani baada ya kifo cha kiongozi wao.

Godane alikuwa ni miongoni mwa watu wanaosakwa sana na Marekani.

Ilitangaza kumzawadia dola za kimarekani milioni 7 kwa yeyote atakayempata.

Mchambuzi wa Somalia Nuur Mohamud Sheekh aliiambia BBC, kifo cha Godane “ni pigo kubwa sana kwa kundi hili”.

“Itakuwa na athari kwa maana ya kupunguza ari kwa wapiganaji wa ardhini lakini si mwisho wa al-Shabab kwa kipindi kifupi na wala kirefu.”

Aliongeza kuwa hakuna mrithi anayeonekana kuwepo.

Siku ya Ijumaa, Rais Hassan Sheikh Mohamed alitangaza msamaha wa siku 45 kwa wapiganaji ambao wako tayari kuachana na al-Shabab.


KESI YA KENYATTA ICC KUENDELEA?



Kenya"s President Uhuru Kenyatta stands for Kenya"s national anthem before the Africa Union Peace and Security Council Summit on Terrorism at the Kenyatta International Convention Centre in Nairobi, September 2, 2014
Kesi dhidi ya Uhuru Kenyatta imewakasirisha viongozi wengi wa Afrika
Waendesha mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC wameomba kesi dhidi ya Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta iahirishwe kwa muda usiojulikana.

Mwendesha mashatka mkuu wa ICC Fatou Bensouda amesema bado hana ushahidi wa kutosha kuendelea na kesi hiyo, iliyotarajiwa kuendelea kusikilizwa mwezi ujao.

Kesi hiyo tayari imeshaahirishwa mara chungu nzima, huku mashahidi wakuu wakijitoa.

Bwana Kenyatta anakana kupanga mauaji ya kikabila baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.

Anatuhumiwa kuhusika na uhalifu dhidi ya binadamu baada ya watu 1,200 kuuawa na 600,000 kukimbia makazi yao.



A Kenyan woman cries before a mass funeral for victims of clashes on January 23, 2008 in Nairobi, Kenya
Kenya haijamshtaki yeyote anayehusika na ghasia za 2007 - 2008

Viongozi wa Afrika walipigia debe kesi hiyo ifutiliwe mbali, wakiishutumu ICC kwa kufanyia uchunguzi madai ya ukatili yanayofanyika barani Afrika tu.

Bi Bensouda, raia wa Gambia, amekana hilo, akisema anasimamia haki za walioathirika barani humo.  

Ameishutumu serikali ya Bw Kenyatta kwa kushindwa kutimiza wajibu wake kwa mahakama, akimaanisha kutoa maelezo aliokuwa akihitaji.

Alisema kesi hiyo isogezwe mbele “mpaka serikali ya Kenya itakapotimiza wajibu wake wa kutuma maelezo waliotakiwa.

Mawakili wa Bw Kenyatta wamekuwa wakirudia mara kwa mara kusema kuwa kesi hiyo ifutwe kutokana na kukosa ushahidi.

Wao, pamoja na mawakili wanaowawakilisha waathirika, kwa sasa wana mpaka Septemba 10 kupeleka maelezo yoyote kuhusiana na kuahirishwa kwa kesi hiyo.

Bw Kenyatta alichaguliwa kuwa Rais mwaka 2013, licha ya kukabiliwa na mashtaka hayo.

Chanzo: BBC
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu