Saturday, 6 September 2014

MIL 10 KUSAKA AJIRA IFIKAPO 2020, UGANDA

Wengi wasiokuwa na ajira hujikuta hawana la kufanya
Wengi wasiokuwa na ajira hujikuta hawana la kufanya
Idadi ya Waganda wanaotafuta ajira inaweza kuongezeka hadi milioni 10 mwaka 2020, jambo linaloshinikiza kubuniwa kwa ajira mpya na jaribio la kufanikisha usawa kwenye uchumi, kulingana na ripoti ya Benki ya Dunia.
Ripoti hiyo yenye kichwa cha habari Ajira, imeleeza, “Uganda inazidi kukabiliwa na changamoto za kuajiri vijana wake wanaoongezeka na hasa walio mijini, na pia wasomi.

Ripoti hiyo ya Benki ya Dunia inaendana sawia na utafiti wa mwaka 2013 uliofanywa na wizara ya Kazi na Elimu ya nchi hiyo iliyogundua kuwa kati ya wahitimu takriban 400,000 wanaomaliza taasisi za mafunzo kila mwaka, chini ya 100,000 ndio hufanikiwa kupata ajira.

Idadi ya watu kwa sasa Uganda inakadiriwa kufikia milioni 34 ambapo itaongezeka hadi milioni 42 ifikapo mwaka 2020.

Bwana Paul Lukema, Mtafiti kutoka kituo cha Utafiti wa Sera za Kiuchumi, anasema suluhisho la muda mfupi ni kuwekeza zaidi kwenye kilimo lakini wakati huo huo serikali iangalie zaidi namna ya kuendeleza viwanda.

“Uganda inatakiwa kubuni takriban ajira 400,000 kwa mwaka ambapo ni nafasi za ajira milioni 2 kila miaka mitano. Japo kilimo huajiri zaidi ya asilimia 65 ya idadi ya watu wote hapa nchini, kumekuwa na mageuzi ambapo vijana wanahama kutoka vijijini kuelekea mijini hivyo ajira huhama kutoka kilimo kwenda sekta nyingine,” Alisema Bwana Lukema.

Hata hivyo, si habari mbaya tu zilizotolewa kwa nchi hiyo ya Uganda, Benki ya Dunia imeongeza kwenye ripoti yake kuwa marekebisho yanayoendelea katika sekta ya elimu inamaanisha ifikapo mwaka 2020, takriban asilimia 50 ya watu wa Uganda watakuwa angalau wamepata elimu ya msingi.

Chanzo: Sunday Monitor, Uganda
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu

No comments:

Post a Comment