Saturday, 6 September 2014

ZANZIBAR ILIVYOPAKWA MATOPE YA UGAIDI


SIKU hizi Zanzibar inaanza kunuka mbele ya taasisi za kimataifa zenye kushughulika na mambo ya ugaidi.

Hayo ni matokeo ya vitimbi vya duru fulani ndani ya Tanzania kwenyewe vya kuipaka Zanzibar matope kuwa ni visiwa vyenye kuufuga ugaidi wa kimataifa.

Duru hizo zimekuwa mbioni kwa muda sasa zikijaribu “kuthibitisha” kuwa Zanzibar imeingiliwa na magaidi wenye fungamano na mtandao wa kimataifa wa al-Qa’eda.

Hadi sasa jitihada zao hazikufanikiwa na, kwa hakika, kuna wachambuzi wenye kuamini kwamba hakuna cha kuthibitisha.

Hoja yao ni kwamba duru hizo zinaisingizia tu Zanzibar kwa lengo la kisiasa.

Wanasema kwamba lengo lenyewe hasa ni kulitia sumu na hatimaye kuliua lile vuguvugu lenye kuitetea haki ya Zanzibar ya kurejeshewa mamlaka yake kamili ya utawala.

Hoja kama hiyo ilitolewa karibuni kwenye Mahakama ya Kisutu na mmoja wa mashekhe wa Jumuiya ya Uamsho wanaoshtakiwa kwa makosa mbalimbali yenye kuhusika na ugaidi.

Sheikh Farid Hadi Ahmed alidai kwamba sababu iliyowachongea wakamatwe Zanzibar na wapelekwe kushtakiwa Dar es Salaam ni msimamo wao wa kuupinga Muungano wa Tanzania.

Kwa vile kesi hiyo iko mahakamani haitujuzu kusema chochote kuhusu mashtaka ya ugaidi yanayowakabili washtakiwa hao. Sheria lakini haituzuii kukumbusha kwamba ijapokuwa mashtaka ya ugaidi ni nyeti na ingawa wengi wetu tunaupinga na kuulaani ugaidi, hata hivyo, mahakama lazima ihakikishe kwamba washtakiwa wanaokabiliwa na mashtaka kama hayo hawanyimwi haki zao za kisheria na kwamba haki zao za kimsingi hazikiukwi.

Chanzo: Raia Mwema, Tanzania


No comments:

Post a Comment