Sunday, 7 September 2014

TANZANIA YA 8 DUNIANI KWA KUJIUA?


Wakati imethibitishwa kwamba katika kila sekunde 40 mtu mmoja duniani huamua kukatisha maisha yake kwa sababu ambazo zinaweza kuzuilika, Tanzania imeelezwa kuwa ya nane katika orodha ya nchi zinazoongoza kwa watu wake kujiua.

Ingawa Jeshi la Polisi nchini lilipotakiwa kuzungumzia suala hilo lilionekana kuchukua mlolongo mrefu, utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO), umesema tabia ya watu kuficha takwimu na kufuatilia matukio ya vifo inachelewesha uchukuaji hatua wa kudhibiti tabia hiyo ya kujiua.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bukumbi juzi alipotakiwa kuthibitisha kwa takwimu kuhusiana na utafiti
huo wa WHO, sababu za kujiua na hata mikoa inayoongoza kwa matukio ya aina hiyo nchini, alitaka mwandishi wa habari hizi kumtumia maswali ili yafanyiwe kazi kuanzia wiki ijayo.

Utafiti uliofanywa na WHO na kutolewa kama Taarifa na Umoja wa Mataifa juzi, unaonesha kwamba tatizo la kujiua halitiliwi maanani wala kujadiliwa kutokana na kunyanyapaliwa na kuwepo kwa imani potofu zinazohusishwa na vifo hivyo.

Katika utafiti uliotolewa wiki tatu baada ya mmoja wa wakali wa Hollywood Robin Williams kujiua, pia waandishi wa habari wameonywa dhidi ya kuelezea kinagaubaga vifo hivyo kutokana na hatari ya watu wengine kunakili tabia na maamuzi hayo kwa jinsi yalivyoelezwa na vyombo vya habari.

WHO, ambayo imesema kwamba kujitwalia maisha binafsi ni tatizo kubwa la kiafya duniani kwa sasa linalohitaji hatua madhubuti kuchukuliwa dhidi yake imetoa taarifa hiyo baada ya kufanya uchunguzi katika nchi 172 duniani.

Imesema katika mwaka 2012 nchi zenye kipato kikubwa ziliongoza kwa mauaji ya aina hiyo ikiwa na vifo asilimia 12.7 kwa kila watu 100,000 huku nchi za kipato cha chini na kati zikiwa ni asilimia 11.2 kwa kila watu 100,000.

Chanzo: wavuti.com


No comments:

Post a Comment