Thursday 30 October 2014

BW GOODLUCK AGOMBEA TENA URAIS NIGERIA



Nigerian President Goodluck Jonathan at the World Economic Forum on Africa in Abuja (10 October 2014)

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan amethibitisha kugombea tena urais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Februari, ofisi yake imesema.

Mpaka sasa alikuwa akikataa kuthibitisha nia yake ya kuchuana tena kwenye kinyang’anyiro hicho.

Nia yake hiyo inatangazwa huku akiwa anakosolewa vikali siku hadi siku kutokana na namna anavyoshughulikia suala la wapiganaji wa Boko Haram waliowateka zaidi ya mabinti 200.

Wapiganaji wameripotiwa kudhibiti mji wa Mubi kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo.

Serikali ilitangaza kusimamisha mapigano na Boko Haram mapema mwezi huu ambapo ingetakiwa mabinti hao wanafunzi waachiwe huru.

Maelfu ya watu wamekimbia ngome ya waasi hao iliyopo kaskazini-mashariki wakati wote wa mgogoro huo.

Wednesday 29 October 2014

SHAIRI - UMEPOTEZA MVUTO





TULIVYOKUWA CHUONI, ULIKUWA HUTUONI
UKAWAAMBIA WANDANI, HUNA TIME NA UTANI
KUTUACHA MATAANI, KWENDA NA MAALWATANI
HIYO IMEKULA KWAKO, NA MVUTO UMEPOTEZA
                           
NAMNA ULIVYOTANUA, NA WAZUNGU NA WACHINA
SI TWATAFUNA MIWA, HATUNA HATA ZA HINA
LEO UKO KWENYE NOAH, NA KESHO KWENYE CARINA
HIYO IMEKULA KWAKO, NA MVUTO UMEPOTEZA

UKAJIONA HODARI, MIBUZI ULIVYOCHUNA
WEWE MJINI JABARI, CHUONI HAKUNA MAANA
MWENYEWE NG’ARI NG’ARI, WAKWAMBIE NINI VIJANA
HIYO IMEKULA KWAKO, NA MVUTO UMEPOTEZA

CHUONI UKAFUKUZWA, KWA HIVYO VYAKO VITUKO
MABABU WAKAKUBEZA, KUTAFUTA ZAIDI YAKO
UKABAKI NA KUWAZA , USIJUE HALI YAKO
HIYO IMEKULA KWAKO, NA MVUTO UMEPOTEZA

UNATAKA NINI KWANGU, WEWE MAKHULUKU TABU?
NIMETULIA NA ZANGU, NDANI NIKO NA MUHIBU
JICHO NI KAMA LA KUNGU, KUTULIA NI WAJIBU
HIYO IMEKULA KWAKO, NA MVUTO UMEPOTEZA

Shairi hili limeandikwa na Wazir Khamsin 

RAIS WA ZAMBIA AFARIKI DUNIA LONDON



Rais wa Zambia Micahel Sata afariki dunia akiwa madarakani

Rais wa Zambia Michael Sata amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 77 baada ya kupata matibabu ya ugonjwa ambao haujaelezwa hadharani, serikali imesema.

Rais Sata, ambaye alikuwa akipata matibabu Uingereza, amefariki mjini London katika hospitali ya King Edward VII siku ya Jumanne usiku.

Vyombo vya habari vinasema alifariki dunia baada ya “mapigo ya moyo ghafla kwenda kasi”

Haijawekwa wazi bado nani atamrithi Rais huyo. Uamuzi huo unaweza kuchukuliwa na baraza la mawaziri la Zambia linalokutana Jumatano asubuhi.

“Ni kwa moyo mzito sana natangaza kifo cha rais wetu mpendwa,” kiongozi wa mawaziri Roland Msiska alisema kupitia televisheni ya taifa.

Alisema mke wa Bw Sata na mtoto wake wa kiume walikuwa naye alipofariki dunia.

“Nawasihi nyote muwe na utulivu, umoja na amani wakati wa kipindi hichi kigumu,” Bw Msiska aliongeza.

Kifo cha Rais huyo kinatokea siku chache tu baada ya Zambia kusherehekea maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru kutoka Uingereza.

'Mfalme Cobra'

Mapema mwezi huu ripoti kutoka Zambia zilizema Rais Sata alikwenda nje ya nchi kufanyiwa matibabu huku kukiwa na hisia nzito kuwa anaumwa sana.

Baada ya kuondoka nchini, waziri wa ulinzi Edgar Lungu alitangazwa kuwa kaimu Rais.

Makamu wa Rais Guy Scott amekuwa akishika nafasi hiyo mara kwa mara katika matukio rasmi. Lakini ana asili ya Scotland na wazazi wake hawakuzaliwa Zambia, kwahiyo inaweza ikawa kikwazo kikatiba ya yeye kugombea nafasi hiyo.

Akijulikana kama “King Cobra” kutokana na ulimi wake mkali, Bw Sata alichaguliwa kuwa rais mwaka 2011.

Ilikuwa ni nadra kuonekana hadharani tangu kurejea kwenye mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa mwezi uliopita, ambapo alishindwa kuhutubia kama ratiba ilivyopangwa.

Bw Sata Septemba 2011, alimshinda rais aliyekuwa madarakani Rupiah Banda ambaye chama chake kilikuwa madarakani kwa miaka 20.

Chanzo: BBC                         
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu



Tuesday 28 October 2014

EBOLA: BENKI YA DUNIA YATAKA WATU KUJITOLEA



 Burial in Monrovia, Liberia, 24 Oct

Rais wa Benki ya Dunia ametoa wito kwa maelfu ya wahudumu wa afya kujitolea na kujaribu kusaidia kuzuia kuenea zaidi kwa mlipuko wa Ebola Afrika magharibi.

Jim Yong Kim alisema takriban watabibu 5,000 na wafanyakazi wengine wanahitajika kupambana na ugonjwa huo.

Wengi waliokuwa na sifa stahili wana woga wa kwenda Afrika magharibi, aliongeza.

Mlipuko wa sasa wa Ebola umewaathiri zaidi ya watu 10,000 na kuua takriban watu 5,000.

Mkuu huyo wa Benki ya Dunia Bw Kim aliyasema hayo wakati wa ziara yake nchini Ethiopia, ambapo aliungana na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini-Zuma.

                                                          

RWANDA YAFANYA VYEMA USAWA WA KIJINSIA





Ushiriki wa wanawake zaidi katika siasa na kazi nyingine imepunguza idadi ya utofauti wa kijinsia duniani katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, Jukwaa la Kiuchumi Duniani (WEF) limesema.

Utafiti wa mwaka wa jinsia wa WEF umethibitisha “mabadiliko makubwa” katika nchi nyingi, huku nchi 105 zikiwa na usawa tangu mwaka 2005, mwandishi wa ripoti hiyo amesema.

Iceland ndio inaongoza kwa miaka sita mfululizo, huku Yemen ikishikilia mkia.

WEF imeangazia zaidi uchumi, afya, elimu na ushiriki wa kisiasa katika nchi 142.

Mataifa sita tu - Sri Lanka, Mali, Croatia, Macedonia, Jordan na Tunisia – yameshuhudia usawa wa kijinsia kuongezeka kwa ujumla tangu mwaka 2005, kulingana na WEF.

Moja ya sababu za mafanikio ya Iceland ni idadi ndogo ya watu nchini humo wakati Yemeni ina idadi kubwa ya vifo na watoto wengi wa kike wenye umri wa miaka sita hadi 14 hawajawahi kuhudhuria shule

Rwanda yafanya vyema

Mataifa ya Nordic yanaongoza, huku Finland, Norway na Sweden yanaifuata Iceland katika tano bora.

Uingereza imeshuka kwa nafasi nane duniani na kufikia nafasi ya 26.

Rwanda imeingia katika orodha hiyo kwa mara ya kwanza na kuchukua nafasi ya saba, na kuifanya nchi yenye mafanikio makubwa kiuchumi barani Afrika.

Mwandishi wa ripoti hiyo Saadia Zahidi alisema mafanikio ya Rwanda ni kwasababu kuna karibu idadi sawa ya wanawake na wanaume wenye ajira – na katika ofisi za wizara – na badala yake huduma za afya na elimu zimeimarika.

Mabadiliko ya mapato ya wanawake ndio iliyoiporomosha Uingereza, ilisema WEF.

Msukosuko wa uchumi ndio umesababisha utofauti wa kipato wa kijinsia kuongezeka Uingereza.

Kutaka kujua zaidi na kujua nchi yako iko nafasi ya ngapi, Bonyeza hapa

http://www.bbc.co.uk/news/world-29722848