Thursday, 30 October 2014

MVUTANO ISRAEL NA PALESTINA



 Israeli security forces stand behind a security perimeter outside the Menachem Begin Heritage Centre (29 October 2014)

Msemaji wa kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas ameelezea kufungwa kwa eneo lenye utata la sehemu takatifu la Jerusalem ni “kutangaza vita”.

Hatua hii imekuja baada ya kuwepo mvutano na vurugu kufuatia kupigwa risasi kwa mwanaharakati wa Kiyahudi.

Waziri mkuu wa Israel ametoa wito wa kuwepo utulivu, akisema Bw Abbas anachochea ghasia.

Eneo hilo takatifu litafunguliwa tena Ijumaa, waziri wa uchumi wa Israel alisema.

Yehuda Glick, mwanaharakati wa Wayahudi alijeruhiwa.

Polisi wa Israel baadae walimwuua Mpalestina anayeshukiwa kumpiga risasi mwanaharakati huyo.

Moataz Hejazi, mwenye umri wa miaka 32, alipigwa risasi baada ya kufyatua risasi alipokuta amezingirwa na polisi nyumbani kwake.

Rabbi Glick ni mwanaharakati maarufu, mzaliwa wa Marekani anayeteta haki za Wayahudi kufanya ibada kwenye eneo hilo, ambapo kwa sasa huzuiliwa.

Jengo hilo – linalojulikana kwa Wayahudi kama Temple Mount na Waislamu wanapaita  Haram al-Sharif –, ni sehemu takatifu kwa Wayahudi na pia una msikiti wa al-Aqsa  - eneo takatifu la tatu katika Uislamu.

Katika taarifa nyingine

  • Sweden imekuwa nchi ya kwanza kubwa upande wa Ulaya kuitambua rasmi Palestina kama taifa – Israel imemrejesha balozi wake wa Sweden kutokana na hilo, kulingana na afisa mmoja aliyenukuliwa na shirika la habari la AFP.
  • Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeisihi Israel kusimamisha ujenzi wao wa makazi kwenye ukanda wa Gaza na kuchunguza madai ya ukiukwaji wa sheria unaofanywa na majeshi yake huko Gaza tangu mwaka 2008.
  • Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry alielezea madai ya kutolewa matusi na afisa mwandamizi kutoka Marekani dhidi ya Bw Netanyahu ni jambo la “aibu, lisilokubalika na lenye madhara”
Chanzo: BBC
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu


GRACA ATAKA MWANAMKE KUMRITHI MUSEVENI




Uganda inatakiwa kuwa na rais mwanamke baada ya Rais Yoweri Museveni kustaafu, mke wa aliyekuwa rais wa Afrika kusini alisema.

 Mwanaharakati wa haki za wanawake na watoto, Graca Machel, alisema Uganda ni miongoni mwa nchi za Afrika zenye wanawake hodari ambao wana uwezo wa kuwa rais. 

“Sijui rais Museveni ana mpango wa kustaafu lini, mwaka 2016? Sijui, lakini atakapofanya hivyo, mwanamke lazima ajiandae kuwa Rais. Ntamwambia (Museveni) tutakapokutana,”  aliyasema hayo huku akishangiliwa katika hoteli ya Serena mjini Kampala.

Machel alisikitika alipoarifiwa kuwa Dr. Specioza Wandira Kazibwe hakuwa makamu wa rais tena kwa sasa.

Rais Museveni aliweka historia alipomteua Dr. Kazibwe kuwa makamu wa rais wa kwanza Uganda mwaka 1994.

Alishikilia nafasi hiyo hadi mwaka 2003. Machel ni mjane wa aliyekuwa rais wa Afrika kusini Nelson Mandela.

Chanzo: newvision.co.ug
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu
                                   



BW GOODLUCK AGOMBEA TENA URAIS NIGERIA



Nigerian President Goodluck Jonathan at the World Economic Forum on Africa in Abuja (10 October 2014)

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan amethibitisha kugombea tena urais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Februari, ofisi yake imesema.

Mpaka sasa alikuwa akikataa kuthibitisha nia yake ya kuchuana tena kwenye kinyang’anyiro hicho.

Nia yake hiyo inatangazwa huku akiwa anakosolewa vikali siku hadi siku kutokana na namna anavyoshughulikia suala la wapiganaji wa Boko Haram waliowateka zaidi ya mabinti 200.

Wapiganaji wameripotiwa kudhibiti mji wa Mubi kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo.

Serikali ilitangaza kusimamisha mapigano na Boko Haram mapema mwezi huu ambapo ingetakiwa mabinti hao wanafunzi waachiwe huru.

Maelfu ya watu wamekimbia ngome ya waasi hao iliyopo kaskazini-mashariki wakati wote wa mgogoro huo.

Wednesday, 29 October 2014

SHAIRI - UMEPOTEZA MVUTO





TULIVYOKUWA CHUONI, ULIKUWA HUTUONI
UKAWAAMBIA WANDANI, HUNA TIME NA UTANI
KUTUACHA MATAANI, KWENDA NA MAALWATANI
HIYO IMEKULA KWAKO, NA MVUTO UMEPOTEZA
                           
NAMNA ULIVYOTANUA, NA WAZUNGU NA WACHINA
SI TWATAFUNA MIWA, HATUNA HATA ZA HINA
LEO UKO KWENYE NOAH, NA KESHO KWENYE CARINA
HIYO IMEKULA KWAKO, NA MVUTO UMEPOTEZA

UKAJIONA HODARI, MIBUZI ULIVYOCHUNA
WEWE MJINI JABARI, CHUONI HAKUNA MAANA
MWENYEWE NG’ARI NG’ARI, WAKWAMBIE NINI VIJANA
HIYO IMEKULA KWAKO, NA MVUTO UMEPOTEZA

CHUONI UKAFUKUZWA, KWA HIVYO VYAKO VITUKO
MABABU WAKAKUBEZA, KUTAFUTA ZAIDI YAKO
UKABAKI NA KUWAZA , USIJUE HALI YAKO
HIYO IMEKULA KWAKO, NA MVUTO UMEPOTEZA

UNATAKA NINI KWANGU, WEWE MAKHULUKU TABU?
NIMETULIA NA ZANGU, NDANI NIKO NA MUHIBU
JICHO NI KAMA LA KUNGU, KUTULIA NI WAJIBU
HIYO IMEKULA KWAKO, NA MVUTO UMEPOTEZA

Shairi hili limeandikwa na Wazir Khamsin 

RAIS WA ZAMBIA AFARIKI DUNIA LONDON



Rais wa Zambia Micahel Sata afariki dunia akiwa madarakani

Rais wa Zambia Michael Sata amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 77 baada ya kupata matibabu ya ugonjwa ambao haujaelezwa hadharani, serikali imesema.

Rais Sata, ambaye alikuwa akipata matibabu Uingereza, amefariki mjini London katika hospitali ya King Edward VII siku ya Jumanne usiku.

Vyombo vya habari vinasema alifariki dunia baada ya “mapigo ya moyo ghafla kwenda kasi”

Haijawekwa wazi bado nani atamrithi Rais huyo. Uamuzi huo unaweza kuchukuliwa na baraza la mawaziri la Zambia linalokutana Jumatano asubuhi.

“Ni kwa moyo mzito sana natangaza kifo cha rais wetu mpendwa,” kiongozi wa mawaziri Roland Msiska alisema kupitia televisheni ya taifa.

Alisema mke wa Bw Sata na mtoto wake wa kiume walikuwa naye alipofariki dunia.

“Nawasihi nyote muwe na utulivu, umoja na amani wakati wa kipindi hichi kigumu,” Bw Msiska aliongeza.

Kifo cha Rais huyo kinatokea siku chache tu baada ya Zambia kusherehekea maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru kutoka Uingereza.

'Mfalme Cobra'

Mapema mwezi huu ripoti kutoka Zambia zilizema Rais Sata alikwenda nje ya nchi kufanyiwa matibabu huku kukiwa na hisia nzito kuwa anaumwa sana.

Baada ya kuondoka nchini, waziri wa ulinzi Edgar Lungu alitangazwa kuwa kaimu Rais.

Makamu wa Rais Guy Scott amekuwa akishika nafasi hiyo mara kwa mara katika matukio rasmi. Lakini ana asili ya Scotland na wazazi wake hawakuzaliwa Zambia, kwahiyo inaweza ikawa kikwazo kikatiba ya yeye kugombea nafasi hiyo.

Akijulikana kama “King Cobra” kutokana na ulimi wake mkali, Bw Sata alichaguliwa kuwa rais mwaka 2011.

Ilikuwa ni nadra kuonekana hadharani tangu kurejea kwenye mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa mwezi uliopita, ambapo alishindwa kuhutubia kama ratiba ilivyopangwa.

Bw Sata Septemba 2011, alimshinda rais aliyekuwa madarakani Rupiah Banda ambaye chama chake kilikuwa madarakani kwa miaka 20.

Chanzo: BBC                         
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu