Mtu hufa kwa kujiua kila sekunde 40, kulingana na ripoti iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Imesema kujiua ni “tatizo kubwa la afya kwa umma” ambao kwa muda mrefu umekuwa jambo lisilozungumzika.
WHO limetaka kupunguza idadi ya watu wanaojiua kwa 10% ifikapo mwaka 2020, lakini limeonya kwamba nchi 28 tu ndio zenye mkakati wa taifa wa kuzuia kujiua.
Wanaharakati wamesema kunatakiwa kutolewe elimu zaidi mashuleni.
WHO limekuwa likifanya tathmini kwa miaka 10 juu ya watu kujiua duniani kote.
Limeainisha kuwa:
- Takriban watu 800,000 hujiua kila mwaka
- Ni ya pili kwa sababu za vifo vya vijana wa umri wa miaka 15 hadi 29
- Walio na umri zaidi ya miaka 70 walikuwa na uwezekano mkubwa wa kujiua
- Robo tatu ya vifo hivyo ni katika nchi zenye uchumi wa chini na wa kati
- Katika nchi tajiri, wanaume mara tatu zaidi ya wanawake hujiua
Ripoti hiyo imesema kupungua kwa uwezekano wa kupata silaha na kemikali zenye sumu zimeonyesha kupunguza idadi ya wanaojiua.
Na pia kuanzisha mkakati wa kitaifa wa kupunguza watu wanaojiua ulikuwa unafanya kazi vizuri, lakini umeundwa katika nchi chache.
Mwiko
Dr Margaret Chan, mkurugenzi wa WHO, alisema: “Ripoti hii ni wito wa hatua kuchukuliwa kuelezea tatizo kubwa la kiafya kwa umma, ambao umekuwa mwiko kwa muda mrefu.”
Unyanyapaa wa jamii dhidi ya magonjwa ya akili unaonekana kuzuia watu kutafuta msaada ambapo humsababishia mtu kujiua.
Jonny Benjamin, mwanaharakati wa kuelimisha masuala ya kujiua Uingereza, ameiambia BBC: “Nadhani kunatakiwa kuwa na elimu zaidi kuhusu kujiua na namna ya kuwasaidia watu wenye mawazo ya kufanya hivyo, watu wachache sana wanajua la kufanya wakimwona mtu ambaye yuko hatarini kujiua au mwenye mawazo na hisia hizo.