Sunday, 9 November 2014

WATOTO WA NCHI ZINAZOENDELEA WANA 'RAHA' ZAIDI




Unhappy child 

Watoto wa nchi zinazoendelea wana furaha zaidi na ni wenye kuridhika kuliko watoto wa Uingereza, utafiti mpya umeonyesha.

Ripoti ya The Children's Society's Good Childhood imeipa nafasi ya chini kuliko hata Romania, Brazil na Afrika kusini.

Ni ya tisa kati ya 11 zilizofanyiwa utafiti – kabla ya Korea kusini na Uganda- jinsi watoto walivyo na furaha na maisha yao.

Ripoti hiyo, iliyoangazia utafiti wa watoto 16,000 kutoka nchi hizo, imeonya hali duni ya maisha yao inaweza kuharibu afya ya watoto, elimu na maisha ya familia zao.

Takwimu zaidi kwenye utafiti huo pia zimependekeza kuwa Uingereza kote, nusu milioni ya watoto walikuwa na hali duni ya maisha.

Mkurugenzi mkuu wa Children's Society, Matthew Reed alisema wakati utoto ulikuwa una mwelekeo mzuri “kwa wengi” Uingereza, hali ya kwamba wengi hawakuwa na raha au kutoridhika na maisha yao isipuuzwe.

"Ripoti hii mpya inaonyesha wazi tuko nyuma ya nchi nyingi, zikiwemo nchi zinazoendelea, " Bw Reed alisema.

Kulingana na takwimu ambazo England ilikuwa ikilinganishwa nazo nyingine 10, mtoto mmoja wa Kiingereza kati ya wanane hakuwa na raha na umbile lake.

Ni watoto wa Korea kusini tu miongoni mwa nchi hizo nao walikuwa wana watoto ambao hawakuridhika na maumbo yao.

'Sikiliza kwa makini'         

Watoto England walikuwa wana hisia chanya kuhusu marafiki, nyumbani, pesa na mali, wakiwa nafasi ya sita miongoni mwa nchi 11.

Ripoti hiyo imegundua kuwepo uhusiano baina ya hali halisi ya mtoto na uwezo wa kiuchumi.

Takriban theluthi ya watoto walisema familia zao zimeathirika “kwa kiwango cha kutosha” au “kiwango kikubwa” na msukosuko wa fedha.

Ilisema watoto wanaojihisi maskini wangetarajiwa maradufu kusema kuwa hawana furaha na mara tatu zaidi wangesema wana maisha duni.

"Watoto wanatuambia kuwa hawana raha kuhusu maisha yao ya usoni na maumbile yao, na pia mambo yanayowapa furaha zaidi ni kama kushirikishwa katika shughuli mbalimbali, kuwa na urafiki imara na uwezo wa kuingia kwenye mitandao,” Bw Reed aliongeza.

"Ni muhimu sana kwa sote – kuanzia watunga sera mpaka wazazi na walimu – kuwasikiliza kwa makini wanachotaka kutuambia.”

Nchi 11 zilizofanyiwa utafiti katika ripoti hiyo ni England, Romania, Uhispania, Israel, Brazil, Marekani, Algeria, Afrika kusini, Chile, Korea kusini na Uganda.

Takriban watoto 16,000 walifanyiwa utafiti - 3,000 kutoka England na kutoka darasa la nne, sita na nane.

Chanzo: BBC
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu


      

Saturday, 8 November 2014

WILLIAMS HAKUWA AMETUMIA DAWA ZA KULEVYA



Williams with wife Susan Schneider
Mke wake Susan Schneider ameomba Williams akumbukwe kwa furaha aliyoleta duniani
Robin Williams hakuwa akitumia dawa za kulevya au pombe katika muda aliojiua, mamlaka za California zimesema.

Muigizaji huyo, mwenye umri wa miaka 63, alikutwa nyumbani kwake California Agosti 11 kwa kile ambacho baadae mamlaka husika zilisema alijiua.

Ripoti iliyotolewa na afisa aliyekuwa akichunguza kifo chake siku ya Ijumaa kiligundua kuwa Williams alikufa kwa kukosa pumzi kutokana na kujinyonga.

Williams, aliyepata umaarufu kutokana na uigizaji wake katika filamu kama Mrs Doubtfire na Good Will Hunting, alikuwa akipata matibabu kutokana na maradhi ya msongo wa mawazo.

Mtoa burudani huyo alionekana mara ya mwisho akiwa hai na mke wake Agosti 10, na kukutwa kafariki dunia siku ya pili yake.

Siku mwili wake ulipokutwa, ni msaidizi wake aliamua kufungua mlango baada ya kuona kimya kila alipougonga, mamlaka zimesema.

Msaidizi wake huyo aliingia chumbani na kumkuta Williams akiwa ameshafariki dunia.

 Williams alishinda tuzo ya Academy katika nafasi aliyoigiza kwenye filamu ya Good Will Hunting na pia alikuwa muigizaji mkuu katika filamu kama vile Good Morning Vietnam na Jumanji.


Friday, 7 November 2014

EBOLA YAPUNGUA LIBERIA



 A Liberian woman prays for the end of Ebola in Monrovia, Liberia - 31 October 2014

Liberia imeshuhudia punguzo kubwa la idadi ya wagonjwa wapya walioambukizwa Ebola, shirika la madaktari wasiokuwa na mipaka Medecins Sans Frontieres (MSF) limethibitisha.

Limesema moja ya vituo vyake vinavyotoa matibabu Liberia haina wagonjwa wowote kwa sasa – lakini likaonya bado maambukizi ya Ebola yanaongezeka Guinea na Sierra Leone.

MSF, linaloajiri maelfu ya wafanyakazi Afrika magharibi, linaonekana kuwa shirika bora lenye taarifa sahihi za Ebola.

 Takriban wagonjwa 5,000 kati ya 14,000 wamekufa kutokana na virusi vya ugonjwa huo.

Chris Stokes, Mkuu wa MSF wa masuala ya Ebola, ameiambia BBC kwamba kupungua kwa idadi ya watu walioathirika na virusi vya ugonjwa huo kumetoa fursa kwa wafanyakazi wa afya kuongeza jitihada.

Lakini alisema ugonjwa huo unaweza “kuibuka” tena, akisema Guinea imeanza kuwa na ongezeko la wagonjwa hao tena licha ya maambukizi kutangazwa kudhibitiwa mara mbili.

Ili kudhibiti ugonjwa huo, Bw Stokes aliongeza, inatakiwa idhibitiwe Liberia, Guinea na Sierra Leone kwa mara moja.

UBISHANI: NANI HASA ALIYEMWUUA BIN LADEN?



Retired US Navy Seal Robert O'Neill (file image)
Robert O'Neil anasema yeye ndiye aliyempiga risasiOsama bin Laden  kichwani

Mabishano ya umma yameibuka ya komandoo yupi wa Marekani aliyefyatua risasi iliyomwuua Osama bin Laden, zaidi ya miaka mitatu baada ya kifo cha kiongozi huyo wa al-Qaeda.

Aliyekuwa mwanajeshi wa nchi hiyo Seal Robert O'Neill, mwenye umri wa miaka 38, ameliambia gazeti la the Washington Post katika mahojiano kuwa yeye ndiye aliyefyatua risasi hiyo.

Kauli yake inapingana na ya Matt Bissonnette, mwanajeshi mwengine aliyehusika katika uvamizi, kwenye kitabu chake alichochapisha mwaka 2012.

Kiongozi huyo wa al-Qaeda aliuawa kwenye uvamizi uliofanywa na wanajeshi wa Marekani katika eneo alilokuwa akiishi huko Abbottabad, Pakistan.

Osama bin-Laden addresses a news conference in Afghanistan in this May 26, 1998 file photo.
Osama bin Laden
Aghlabu wanajeshi hao (Navy Seals) hutii sheria ya ukimya linalowakataza kupata sifa yoyote kutoka kwa umma kutokana na hatua walizochukua.

Bw O'Neill, aliyestaafu mwaka 2012, awali alielezea habari yake bila kuonekana sura kwenye jarida la Esquire.

Ilitakiwa ajitambulishe hadharani kwenye mahojiano ya televisheni baadae mwezi huu, lakini taarifa za mahojiano hayo yaliwakasirisha waliokuwa wanajeshi wakati huo.

Bw O'Neill alisema yeye na mwenzake mwengine – ambaye utambulisho wake unabaki kuwa siri – walipanda ngazi mpaka ghorofa ya tatu ya makazi yake Abbottabad, Pakistan, na kumwona Bin Laden akichungulia nje ya mlango mojawapo ya vyumba vya nyumba hiyo.