Watayarishaji wa kipindi
kimoja maarufu cha kijamii cha televisheni nchini Angola wameomba radhi baada
ya kuonyesha wapenzi wa jinsia moja wakibusiana na kusababisha hamaki miongoni
mwa watazamaji.
Televisheni ya taifa ilisema imesimamisha kipindi hicho kiitwacho Jikulumessu kutokana na "sababu za kiufundi ".
Watazamaji wengi wamehisi kipindi hicho kilivuka mipaka kwa kuonyesha wanaume wawili wakibusiana, licha ya kwamba mapenzi ya jinsia moja hayakuharamishwa Angola, waandishi walisema.
Kipindi hicho kilitayarishwa na kampuni inayomilikiwa na mtoto wa kiume wa rais wa nchi hiyo.
Jose Eduardo Paulino dos Santos, muigizaji mkuu ambaye jina lake la uigizaji ni Coreon Du, amekuwa akishutumiwa kuunga mkono wapenzi wa jinsia moja Angola, nchi ambayo wengi wana misimamo mikali ya kidini na maadili tofauti ya kijamii.
Kampuni yake, Semba Productions, ilisema ilikuwa ikitathmini upya kipindi hicho na kuomba radhi kwa lolote baya lililotokea.