Friday, 5 September 2014

1 KATI YA MABINTI 10 HUDHALILISHWA KIJINSIA


A young girl covers her face. File photo

Takriban watoto wa kike milioni 120 duniani –  kama zaidi ya mmoja kwa kila 10 – wamebakwa au kudhalilishwa kijinsia wafikapo umri wa miaka 20, ripoti ya Umoja wa Mataifa imesema.

Shirika la UN linaloshughulikia watoto Unicef pia limesema watoto na vijana 95,000 – wengi wao kutoka visiwa vya Carribean na Marekani ya kusini – waliuawa mwaka 2012 pekee.

Inaonyesha kuwa watoto duniani wanakabiliwa na udhalilishaji mara kwa mara.

Ripoti hiyo ni mkusanyiko wa taarifa kutoka nchi 190.

‘Athari ya milele’       

Unyanyasaji huo “umesambaa mipaka yote ya umri, eneo, dini, kabila na kipato,” Mkurugenzi mkuu wa Unicef Anthony Lake amesema.

Udhalilishaji dhidi ya watoto
  • Mabinti milioni 120 – mmoja kati ya 10 – hubakwa au kudhalilishwa kijinsia afikapo umri wa miaka 20
  • Watoto wa kiume nao hudhalilishwa, lakini kwa kiwango kidogo ukilinganisha na watoto wa kike
  • Udhalilishaji wa kijinsia ulio maarufu kwa wote wa kike na wa kiume ni kupitia mtandao
  • Watoto na vijana 95,000 waliuawa mwaka 2012
  • Takriban zaidi ya mmoja katika ya wanafunzi watatu wenye umri wa miaka 13-15 hufanyiwa ubabe shuleni (bullying)
  • Sita kati ya 10 wenye umri kati ya miwili na 14 hupigwa na wanaowatunza
Chanzo: Ripoti ya Unicef

"Hufanyika maeneo ambapo mtoto anatakiwa kujisikia salama, majumbani, shuleni na kwenye jamii.
“Imeongezeka zaidi kupitia mitandao, na hufanywa na wanafamilia na walimu, majirani na watu usiowafahamu na pia watoto wengine.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa mmoja kati ya watoto watatu, wenye umri kati ya miaka 15 na 19, ambao kwa wakati fulani wamekuwa kwenye mahusiano bila ya ndoa japo husihi pamoja, wengi hujikuta wakidhalilishwa kijinsia na pia kupigwa  na wapenzi wao au waume zao.

Udhalilishaji wa mwenza umeonekana kushamiri sana kwenye nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Uganda, Tanzania na Zimbabwe, kulingana na ripoti.

Miongoni mwa nchi zilizofanyiwa utafiti, takriban nusu ya mabinti kati ya umri wa miaka 15-19 wanaamini mume ana haki ya kumpiga mkewe kutokana na sababu kadhaa, ripoti hiyo imesema.

Chanzo: BBC
                                                   


KIDATO CHA IV KUWA KIGEZO CHA UBUNGE TANZANIA?


 




Pendekezo la Rasimu ya Katiba kuwa wabunge walau wawe na elimu ya kidato cha nne limetupiliwa mbali na wajumbe wa Bunge Maalumu, baada ya Kamati karibu zote kulikataa.

Kamati hizo zimependekeza kigezo cha elimu kuanzia walau kidato cha nne kama sharti muhimu la mtu anayetaka kugombea Ubunge kiondolewe, badala yake mgombea ama ajue tu kusoma na kuandika, au ajue kusoma na kuandika Lugha ya Kiswahili au Kiingereza kama ilivyo kwenye Katiba ya sasa.

Mbali na pendekezo hilo, kamati hizo zimegawanyika kuhusu Ibara ya 129 ya Rasimu ya Katiba inayowapa wananchi nguvu ya kumuondoa mbunge wao madarakani kabla ya miaka mitano kumalizika.

Hayo yalijitokeza bungeni Dodoma jana, wakati kamati hizo zikiwasilisha taarifa zake kuhusu Sura ya 9 na 10 ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Akiwasilisha maoni ya Kamati Namba 10, Mjumbe wa kamati hiyo, Dk Dalaly Kafumu alisema suala la kugombea nafasi yoyote ni la kidemokrasia, hivyo haipaswi mtu yeyote kuzuiwa kwa kigezo cha elimu.

“Haki ya kuamua iwapo mgombea anafaa au hafai ni ya wapigakura. Wasizuiwe kikatiba kutumia haki yao ya msingi ya kuchagua mtu wanayemtaka,”alisema na kuongeza: “Utaratibu huu haupo duniani kote hata nchi zilizo na demokrasia iliyokomaa. Hivyo ibara hiyo isomeke tu ajue kusoma na kuandika na si kiwango cha elimu kama sifa ya msingi.”

Mapendekezo hayo yaliungwa mkono na Kamati Namba 8 kupitia kwa Mjumbe wake, Juma Alawi aliyesema kuweka kiwango cha elimu kwa wagombea ubunge ni ubaguzi.

Kuondolewa kwa kigezo cha elimu ya kidato cha nne pia kumeungwa mkono na kamati namba 10, 4, 12, 9 na 12 za Bunge hilo zilizowasilisha taarifa zake jana asubuhi.

Kamati namba 12 ndiyo iliyokwenda mbali zaidi na kudai kuwa ibara hiyo itasababisha ubaguzi kulingana na elimu wakati kiwango cha chini cha elimu kwa Tanzania Bara ni darasa la saba na Zanzibar ni darasa la 10.

UKRAINE NA URUSI KUKUBALIANA?

Pro-Russian separatists sit on top an armoured personnel carrier near a destroyed tank on a road in the village of Novokaterinovka, some 50km southeast of Donetsk


Rais wa Ukraine Petro Poroshenko ametoa matumaini kuwa wanaweza kufikia muafaka na Urusi wa kusitisha mapigano mashariki mwa nchi yake.

Ukraine, Urusi na waasi wanaoiunga mkono Urusi wanatarajiwa kuanza mazungumzo mchana huko Belarus. Hatahivyo, kuna ripoti za kurushwa kwa makombora karibu na mji wa Mariupol.

Wakati huo huo, nchi za magharibi wanajiandaa kuongeza vikwazo kwa Urusi iwapo mazungumzo hayatofikia popote.

Wanahudhuria siku ya pili ya mkutano wa Nato Newport, Wales.

Nchi za magharibi zinaishutumu Urusi kwa kutuma silaha na majeshi kwa waasi mashariki mwa Ukraine. Moscow imekana hilo.

Zaidi ya watu 2,600 wamefariki dunia wakati wa mapigano hayo yaliyodumu kwa miezi mitano.

Chanzo: BBC
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu

Thursday, 4 September 2014

ROJO APEWA KIBALI CHA KAZI, KUWAVAA QPR


Marcos Rojo amepewa kibali cha kazi na hivyo anatarajiwa kucheza kwa mara ya kwanza dhidi ya QPR.
Marcos Rojo amepewa kibali cha kazi na hivyo anatarajiwa kucheza kwa mara ya kwanza dhidi ya QPR


Kijana mpya wa Manchester United Marcos Rojo ataonekana kwa mara ya kwanza dhidi ya Queens Park Rangers kwenye uwanja wa Old Trafford Septemba 14 baada ya kupewa kibali cha kufanya kazi.


Rojo alikwenda Ureno siku ya Alhamisi kwa ajili ya kukamilisha masuala yanayohusu kibali chake cha kazi.

Uwepo wake utakisaidia kikosi cha Louis van Gaal ambaye amekuwa na tatizo la ulinzi kwenye mechi za kwanza za msimu huu.

Rojo aliruhusiwa kufanya mazoezi Manchester United pamoja na kutokuwa na kibali cha kazi.
Rojo aliruhusiwa kufanya mazoezi Manchester United licha ya kutokuwa na kibali cha kazi

Agosti 30 Sportsmail ilieleza kwamba suala lililokuwa limekwamisha kibali chake cha kazi ni kwamba maafisa wa Ubalozi walikuwa wakichunguza taarifa za tuhuma ya malumbano kati ya Rojo na jirani yake nchini Argentina.

Muargentina huyo, 24, hakuwahi kushtakiwa kwa tukio hilo, ambalo lilitokea mwaka 2010, ila bado lilikuwa likifanyiwa uchunguzi wa kinadharia baada ya kesi kufunguliwa upya mwezi Mei mwaka huu.

Chanzo: taarifa.co.tz

UVUVI WA BARUTI TANZANIA

Ni biashara inayoleta kipato kikubwa, mamilioni ya dola kwa mwaka. Karibu asilimia kumi ya watanzania wanajihusisha na sekta ya uvuvi, kwa njia moja au nyingine, na kwa kutumia njia halali. Huku kukiwa na fedha nyingi, sekta hiyo inamulikwa pia na njia haramu. Moja wapo ni uvuvi wa kutumia baruti, katika kupata samaki kwa njia rahisi. Jambo hilo haliathiri uchumi pekee, bali pia mazingira.Salim Kikeke kutoka BBC ameandaa taarifa hii.

MCHEKESHAJI JOAN RIVERS AFARIKI DUNIA

Joan Rivers



Mchekeshaji na mtangazaji wa kipindi cha televisheni Joan Rivers amefariki dunia, binti yake amesema.

Rivers, mwenye umri wa miaka 81, amekuwa akitumia mashine ya kupumulia katika hospitali ya Mount Sinai tangu kupata maradhi ya moyo mjini New York wiki iliyopita.

Katika taarifa iliyotolewa na binti yake Melissa, amesema amefariki dunia huku akiwa amezungukwa na familia na marafiki, na amewashukuru wafanyakazi wa hospitali kwa “huduma yao isiyo na kifani”.

Pumzi za mchekeshaji huyo aliyejulikana sana kwa kauli zake kali na za kuchoma zilisita wakati wa upasuaji wa mishipa yake ya sauti kwenye zahanati moja siku ya Alhamis.

“Kitu kilichokuwa kikimfurahisha sana mama yangu hapa duniani ni kuchekesha watu,” alisema Melissa Rivers.

"Japo hilo ni vigumu kwa sasa, najua ombi lake la mwisho lingekuwa kurejea kucheka tena haraka tu iwezekanavyo."

Muigizaji huyo anajulikana kwa madhila yaliyomkuta katika maisha yake na hivi karibuni ameanza kuwananga watu mashuhuri wanaohudhuria matamasaha makubwa wanayopita kwa kile kiitwacho ‘red carepet’ kwenye kipindi chake cha Fashion Police.

Alizaliwa kwa jina la Joan Alexandra Molinsky huko Brooklyn, New York, kutoka familia ya wahamiaji wa Kiyahudi waliokimbia mapinduzi ya Urusi.

Alianza kujulikana mwaka 1965 alipotokea kwenye kipindi cha The Tonight Show kikiongozwa na Johnny Carson.

MTOTO AKATAA UTOTO


Vimbwanga vya WhatsApp

RIVERS ATOLEWA CHUMBA CHA WAGONJWA MAHUTUTI



Joan Rivers
Joan Rivers akitangaza kitabu chake cha kumi, Diary of a Mad Diva, mapema mwaka huu


Mchekeshaji na mtangazaji wa televisheni Joan Rivers ametolewa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi na “amewekwa mahala tulivu” katika chumba binafsi hospitalini.


Rivers, mwenye umri wa miaka 81, amekuwa akitumia mashine kupumua akiwa kwenye hospitali ya Mount Sinai tangu kupata maradhi ya moyo mjini New York wiki iliyopita.

Pumzi za mchekeshaji huyo zilisita wakati wa upasuaji wa mishipa yake ya sauti kwenye zahanati moja Alhamis iliyopita.

Binti yake, Melissa Rivers, alitoa taarifa kuthibitisha afya ya mama yake ikiimarika siku ya Jumatano.

“Mama yangu ametolewa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi na kupelekwa chumba binafsi,” ilisema taarifa hiyo kutoka Melissa. “Ahsante kwa nyote mnaoendelea kunipa moyo.”

Joan Rivers amekuwa kwenye mashine za kupumulia kwa zaidi ya wiki moja. Hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa kuhusu afya yake.

Muigizaji na mchekeshaji huyo anajulikana sana kwa kauli zake kali na za kuchoma, na hivi karibuni ameanza kuwananga watu mashuhuri wanohudhuria matamasaha makubwa wanopita kwa kile kiitwacho ‘red carepet’ kwenye kipindi chake cha Fashion Police.

VIFO VYA EBOLA VYAZIDI 1,900 - WHO



A girl walks past a slogan painted on a wall reading "Stop Ebola" in Monrovia - 31 August 2014
Mlipuko wa Ebola umeenea kwenye nchi tano Afrika Magharibi


Zaidi ya watu 1,900 wamefariki dunia Afrika magharibi kutokana na mlipuko wa Ebola, shirika la Afya duniani WHO limesema.


Kumeshathibitishwa kuwepo wagonjwa 3,500 nchini Guinea, Sierra Leone na Liberia

Shirika hilo linakutana Alhamis kutathmini tiba gani bora na namna ya kujadili kufanyika vipimo vya haraka na uzalishaji wa dawa.

Wataalamu wa kudhibiti maradhi, watafiti wa tiba, maafisa kutoka nchi zilizoathirika, watawakilishwa kwenye mkutano Geneva.

Takriban dola za kimarekani milioni 600 zinahitajika kupambana na kirusi hicho, na zaidi ya watu 20,000 wanaweza kuambukizwa kabla ya mlipuko huo kudhibitiwa, WHO imeonya.

Mkuu wa WHO Margaret Chan ameelezea mlipuko huo  “ni mkubwa, hatari na wenye utata mkubwa waliowahi kuuona”.

“Hakuna yeyote, hata wataalamu wa maradhi ya milipuko wenye uzoefu wa tangu mwaka 1976 hadi 1995, watu ambao walihusika moja kwa moja na milipuko hiyo, hakuna aliyeona kitu kama hicho,” alisema

Zaidi ya asilimia 40 ya vifo vimetokea katika kipindi cha wiki tatu kuelekea Septemba 3, WHO, ikiashiria kuwa ugonjwa huo unaongezeka kwa kasi kiasi cha kushindwa kuudhibiti.

Chanzo: BBC

Imetafsiriwa na Mwandishi wetu

Wednesday, 3 September 2014

GARI LA RAIS WA KENYA LAPATIKANA UGANDA



Kenyan presidential security escort President Uhuru Kenyatta's car - March 2013
Magari ya msafara wa Rais yanatakiwa kuwa na ulinzi wa hali ya juu


Gari lililotekwa ambalo ni mali ya idara ya usalama ya Rais wa Kenya limepatikana nchini Uganda.

Gari hilo aina ya BMW lilitekwa Jumatano iliyopita mjini Nairobi huku watekaji wakimtishia dereva kumpiga risasi.

Mkurugenzi wa Interpol Uganda, Assan Kasingye, ameaimbia BBC gari hilo litarejeshwa Nairobi.

Takwimu za hivi karibuni za polisi nchini Kenya zinaonyesha kuwa takriban matukio matatu ya utekaji magari hutokea kwenye mji mkuu wa nchi hiyo.

Mwandishi wa BBC Paul Nabiswa amesema taarifa za tukio hilo zilisambaa kwenye vyombo mbalimbali vya habari nchini Kenya, licha ya msemaji wa Rais Uhuru Kenyatta kujaribu kupunguza makali.

Msemaji huyo alisema gari hilo halikuwa katika msafara wa Rais kwa wakati huo na lilikuwa tu gari la polisi.

Lakini magazeti ya Kenya yameeleza kuwa lilikuwa likiendeshwa na Inspekta wa polisi ambaye ni miongoni mwa maafisa wa usalama wa Rais, amesema mwandishi wa BBC.

Inspekta huyo alivamiwa na watu wanne wenye silaha ambao walimlazimisha kukaa nyuma ya gari na kutimka nalo, gazeti la Kenya Nation lilisema.

Aliachwa nje ya taasisi ya mafunzo ya polisi kwenye wilaya moja mashariki mwa Nairobi saa sita baadae, inaeleza.

Vyombo vya habari vya Kenya vilisema takriban watu watatu wameshakamatwa wakihusishwa na wizi huo Nairobi, kaskazini- magharibi mwa mji mkuu wa nchi hiyo, na Bungoma, mji ulio mpakani na Uganda.


MWANAMKE WA KWANZA KUTANGAZA BBC DIRA YA DUNIA TV

Mtangazaji wa BBC Idhaa ya Kiswahili Zuhura Yunus amekuwa mwanamke wa kwanza kutangaza kipindi cha BBC Dira ya Dunia Tv kinachorusha matangazo yake kutoka jijini London.

Kipindi cha Dira ya Dunia ya BBC kilianzishwa miaka miwili iliyopita na watazamaji wake wakizoea kutazama sura za watangazaji wa kiume kama Salim Kikeke, Charles Hillary, Peter Musembi na Kassim Kayira .

 Lakini, Septemba 1, 2014, Zuhura Yunus alitangaza kwa mara ya kwanza kwenye kipindi hicho maarufu Afrika Mashariki na wazungumzaji wa Kiswahili duniani kote.

Bi Yunus ambaye ni mtangazaji wa BBC Swahili kwa muda mrefu sasa, ameungana na wafanyakazi wenzake kurusha matangazo ya Dira ya Dunia.

Hongera Bi Zuhura Yunus.

Chanzo: taarifa.co.tz