Tuesday, 9 September 2014

DENZEL AKUMBUKA MACHUNGU YA KUBAGULIWA



Muigizaji maarufu Denzel Washington na mkewe Pauletta Washington


 Wakati wa kutayarisha filamu mpya iitwayo The Equalizer mjini Boston, Marekani, Denzel Washington aliibua kumbukumbu za ubaguzi alizokabiliana nazo zaidi ya miaka 30 iliyopita.

Washington alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika tamasha la Filamu la Toronto, ndipo lilipoibuka swali kuhusu kuigiza filamu hiyo Boston na kauli aliyoitoa kuhusu mke wake ndiyo iliyoleta hisia zisizotarajiwa.

Washington alieleza wakati alipokuwa Boston miongo mitatu iliyopita pamoja na mkewe Pauletta Learson Washington, aliyekuwa naye akiigiza, baadhi ya watu wakadhani yeye ni kuwadi, na mkewe ni changudoa. Walinzi waliitwa, na ghasia zikaanza.

“Nilikuwa sijui kupigana, lakini nilijua namna ya kushinda,” Washington aliwaambia waandishi wa habari.

Pia anakumbuka namna alivyokwenda kumtazama mkewe akiigiza usiku mmoja na kuitwa kwa jina la N (ambalo halifai kulitaja)

 “‘Hey n—, n—, n—, n—, hey boy.’ Nikasema Nini?.’  Hiyo ndio kumbukumbu niliyonayo ya Boston ,” alisema.

Halafu akaelezea mara ya kwanza alipoitwa kwa jina hilo linaloanzia N alipokuwa Florida, alikuwa amekaa kwenye veranda akiwa kama na umri wa miaka tisa. Aliitwa jina hilo lenye dharau na kundi la watoto ambapo alirudi nyumbani na kumwuuliza mama yake kwanini wanamwita hivyo.

 “Akasema, Ah, huyo ni mtu tu anaogopa utachukua nafasi yake.’ Ilikuwa kama kaa chini ya mtungi. Na kusinimagharibi mwa Boston, ilikuwa kawaida ,” alisema, akimaanisha nyumba kwenye maeneo yenye umaskini ambazo zimebanana. “Wao wako chini. Kwahiyo ilikuwa kama kusema, ‘Sisi bora kuliko wewe.’ Ndio, kwahiyo nimekuja Boston na kumbukumbu kama hizo.”

The Equalizer itaanza kuonyeshwa Marekani Sepembat 26.

Chanzo: uk/yahoo.com
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu


ISRAEL 'YAWATISHIA' WAHAMIAJI KUONDOKA



African migrants stand inside the Holot facility in Israel's Negev desert (17 February 2014)

Mamia ya wahamiaji WaEritrea na WaSudan wapo kwenye eneo maalum la jangwa la Negev, Israel




Israel inatumia nguvu na vitisho kinyume na sheria kwa takriban raia 7,000 kutoka Eritrea na Sudan kuondoka nchini, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema.

Wamenyimwa haki ya kupewa fursa ya kufuata mchakato ulio bora wa kuomba hifadhi na kuwekwa kizuizini, ripoti mpya imesema.

Mapema mwaka huu, waliyoomba hifadhi kutoka barani Afrika huko Israel walifanya maandamano makubwa kulalamikia namna wanavyochukuliwa.

Israel ilisema sera zake kwa wahamiaji waliopo kinyume cha sheria na wakimbizi zinaendana na sheria za kimataifa.

Nchi hiyo inasistiza Waafrika si waombaji hifadhi lakini wahamiaji wa kiuchumi wanaoona Israel kama mahala panapovutia kwasababu ni nchi iliyoendelea iliyo karibu wanapoweza kutafuta ajira.

Chanzo: BBC
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu







MTOTO WA OBASANJO APIGWA RISASI, NIGERIA



Former President Olusegun Obasanjo (March 20110
Aliyekuwa Rais Olusegun Obasanjo alipigana katika vita vya wenyewe kwa wenyewe Nigeria 1967-1970
Mtoto wa kiume wa aliyekuwa Rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo amepigwa risasi na kujeruhiwa katika mapambano na wapiganaji, msaidizi wa Bw Obasanjo  alisema.

Lt  Kanali Adeboye Obasanjo  alijeruhiwa wakati  jeshi  lilipojaribu kudhibiti upya miji kaskazini-mashariki mwa jimbo la Adamawa kutoka kwa Boko Haram, Muhammad Keffi ameiambia BBC.

“Idadi kubwa ya wapiganaji” pia waliuawa katika mapambano hayo, jeshi lilisema.

Mwezi uliopita, Boko Haram walitangaza kuwepo na taifa la Kiislamu katika maeneo wanayodhibiti kaskazini-mashariki mwa Nigeria.

Wataalamu walionyesha wasiwasi kuwa Nigeria, nchi yenye idadi ya watu wengi zaidi barani Afrika, inaweza kugawanyika kama ilivyo Iraq na Syria ambapo kundi la wapiganaji la IS limetangaza kuwa Taifa la Kiislamu.

Wapiganaji wa Boko Haram wameteka Michika na Bazza, miji miwili karibu na mji ulio maarufu kibiashara wa Mubi, katika siku za hivi karibuni.

APPLE YAZINDUA iPHONE YENYE UKUBWA ZAIDI



Apple iPhones

Kampuni ya Apple imetoa simu za kisasa aina mbili – iPhone 6 na aina nyingine kubwa zaidi, iPhone 6 Plus.

Zote mbili ni kubwa kuliko toleo za mwanzo – huku skrini zikiwa na ukubwa wa sentimita 11.9 na 14.0.

Pia ni takriban nusu ya milimita kwa wembamba.

Imeimarisha muonekano wake kwa kile walichoita “retina HD”, ambapo itakuwa inapakua taarifa kwa kasi zaidi na kuahidi bateri kudumu kwa muda mrefu zaidi.

Apple ilishuhudia mauzo yake ya simu za kisasa kushuka duniani kutoka 13% hadi 11.7% kati ya mwaka 2013 mwishoni na mwaka 2014, kulingana na utafiti wa kampuni ya IDC.

Hata hivyo, mauzo ya Android yaliongezeka kutoka 79.6% hadi 84.7% katika kipindi hicho hicho cha Aprili hadi Juni, huku Samsung ikiwa na mauzo zaidi na kampuni ya Huawei na Lenovo za China ambazo zinaonekana kushamiri kwa kasi.

“Faida kubwa ya Apple ya kutengeneza skrini kubwa zaidi si kwamba inataka kuvutia watu wanunue simu zao, lakini kuzuia wateja wake kukimbia, hasa kukimbilia Samsung Galaxy Note,” alisema John Delany, mkuu wa timu ya Ulaya ya IDC.

“Liko wazi kuwa wateja wengi wa soko la Apple wanataka simu yenye ukubwa zaidi, alisema

Chanzo: BBC
 Imetafsiriwa na Mwandishi wetu









SHAIRI - MADAFU



Unapokunywa ni raha,         Wasifia ihsani
Wajipa nawe furaha,            Tena isiyo kifani
Ila kuna na karaha,               Kawaulize wandani
Ukiyapenda madafu,             Ujifunze na kukweya

Mbona hukwenda Kiunga,    Kama umkwezi kweli
Au ukapita Tanga,                 Kuangua yalo mali
Umeng'ang'ana Ukonga,        Kwenye madafu mawili
Ukiyapenda madafu,              Ujifunze na kukweya

Ukwezi sharti ujuzi,               Na jitihada muruwa
Hautaki mtu `lazy’,                Asiyejituma sawa
Hebu tizama wakwezi,          Namna wanavyopagawa
Ukiyapenda madafu,             Ujifunze na kukweya 

Si lazima uwe kipa,               Kwa mnazi kuukweya
Pengine ukala papa,              Kidhani tasaidiya
Mabingwa hutoka kapa,       Mchovu yu kidedea
Ukiyapenda madafu ,           Ujifunze na kukweya    

Unafurahia ladha,                 Na kiu kuondokewa
Kujiona wewe ‘father’,        Baada ya kukamuwa
Hayaokotwi ‘brother’,         Mnazini metolewa
Ukiyapenda madafu,            Ujifunze na kukweya  

Mashairi yana ladha yake na hasa yakiandikwa kwa lugha fasaha na aina yake.
Shairi hili limeandikwa na Wazir Khamsin