Sunday, 26 October 2014
CHAMA TAWALA BOTSWANA KUSHINDA UCHAGUZI
Chama tawala cha Botswana Democratic (BDP) kimeshinda uchaguzi mkuu katika nchi inayozalisha almasi kwa wingi zaidi duniani.
Imepata takriban viti 33 miongoni mwa 57 vya ubunge, tume ya uchaguzi ya taifa imesema.
Chama kinahitaji viti 29 kuchukua madaraka. Kundi la upinzani la Umbrella for Democratic Change limepata viti 14.
Chama cha BDP cha Rais Ian Khama kimekuwa madarakani tangu Botswana ilipopata uhuru mwaka 1966.
Lakini kimekuwa kikipambana kuungwa mkono maeneo ya mijini ambapo vyama vya upinzani hivi karibuni vimeonekana kufanya vizuri.
Botswana inaonekana ni miongoni mwa nchi zenye utulivu na demokrasia barani Afrika.
Nchi hiyo bado haina mgawanyiko sawa wa mali, umaskini wa hali ya juu, ukosefu wa ajira na HIV, kulingana na Benki ya Maendeleo ya Afrika ADB.
Ukosefu wa kiwango cha ajira umefikia 17.8% na ina watu wenye maambukizi ya virusi vya HIV kwa 23.4%.
Utafiti uliofanyika mwezi huu na shirika la utafiti la Afrobarometer limeripoti 58% ya watu wa Botswana wanaona ukosefu wa ajira kama tatizo kubwa linaloikumba nchi yao ya Botswana.
BI OBAMA AZUNGUMZIA WANAWAKE NA WANAUME
WhatsAapp
MKIMBIAJI WA AFRIKA KUSINI AFARIKI DUNIA
Aliyekuwa mshindi wa dunia wa mbio za mita 800 Mbulaeni Mulaudzi amefariki dunia katika ajali ya gari nchini mwake Afrika kusini.
Mulaudzi alishinda dhahabu katika mashindano ya dunia ya mwaka 2009 katika mita 800 mjini Berlin na kushinda fedha katika mashindano ya Olimpiki mwaka 2004 mjini Athens.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 34, aliyebeba bendera ya nchi yake katika sherehe za ufunguzi mjini Athens, alistaafu mwaka 2013.
"Bw Mulaudzi kwa hakika alikuwa miongoni mwa wakimbiaji bora Afrika kusini iliyowahi kushuhudia,” alisema Peet van Zyl
Chanzo: BBC
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu
CHID BENZ ANASWA NA DAWA ZA KULEVYA
Msanii wa muziki wa Hiphop nchini Rashid Makwiro maarufu ‘Chid Benz’, jana alasiri alikamatwa na dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwananchi, Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege, ACP Hamis Selemani, alithibitisha kukamatwa kwa Chid Benz na kwamba bado anaendelea kushikiliwa na polisi.
“Msanii huyu tumemkamata hapa airport akijaribu kuvuka na dawa za kulevya kinyume cha sheria akielekea jijini Mbeya. Alikuwa katika hatua za ukaguzi kwa ajili ya kupanda ndege ya Fastjet kuelekea Mbeya akiwa na wenzake,” alisema.
Akivitaja vitu alivyokamatwa navyo, ACP Selemani alisema msanii huyu amekutwa na kete 14 zinazodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya na mpaka sasa bado wanaendelea uchunguzi kubaini ni aina gani za dawa hizo.
“Mtuhumiwa huyu tumemkamata na kete 14 pamoja na misokoto miwili ya bangi, ambayo alikuwa ameiweka katika mfuko wa shati alilokuwa amevaa. Aidha, tumemkuta na kigae kidogo cha chungu pamoja na kijiko, vitu vya maandalizi ya kutumia dawa hizo na hivi vyote vimekutwa katika begi lake,” alisema.
Alisema hivi sasa msanii huyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi, “Bado tunaendelea kumshikilia na tutahakikisha sheria inafuatwa kama inavyokuwa kwa watuhumiwa wengine wanapokamatwa na vitu kama hivi,” alisema kamanda huyo.
Msanii huyo alikuwa anakwenda jijini Mbeya, kwa ajili ya kushiriki onyesho la ‘Instagram Party’ linalotarajiwa kufanyika leo jijini humo.
Chidi Benz alikuwa ameongozana na msanii mwenzake Nurdin Bilal maarufu ‘Shetta’, baada ya kukamatwa na polisi, Shetta aliendelea na ukaguzi kwa ajili ya kupanda ndege kuelekea Mbeya.
Julai mwaka jana wasanii wawili Melisa Edward na mwenzake Agnes Gerald ‘Masogange’ walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oriver Tambo nchini Afrika Kusini, wakiwa na dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine takriban kilo 150, zilizokuwa na thamani ya Sh6.8 bilioni.
Saturday, 25 October 2014
GIBNEY, AFUMWA KUOA MKE WA PILI FACEBOOK
Maurice Gibney, Yvonne Gibney (juu kulia) na Suzanne Prudhoe (chini kushoto) |
Kama wanandoa wengine wote, Yvonne na Maurice Gibney walikuwa na misukosuko kwenye ndoa yao.
Aliwahi kusoma kuhusu tetesi za uwezekano wa mumewe kutoka nje ya ndoa kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook, lakini akawa na imani kuwa ilikuwa ni uzushi tu na hawezi kumwendea kinyume wakati alipokuwa akifanya kazi Oman.
Wazo hilo lilibaki mpaka alipogundua picha ya mume wake huyo mwenye watoto wawili akiwa anamwoa mwanamke mwengine kwenye ufukwe wa bahari katika taifa hilo la Kiarabu.
Bila kujua Bi Gibney, mwenye umri wa miaka 55, mumewe anayefanya kazi kwenye kampuni ya mafuta amekuwa akiishi maisha mengine na mwalimu Suzanne Prudhoe, mwenye umri wa miaka 46.
Baadae ilikuja kujulikana wawili hao walikuwa wapenzi kwa takriban miezi 18 kabla ya kufanya sherehe baharini yenye kugharimu £45,000 kwenye ubalozi wa Uingereza, mwezi Machi mwaka jana.
Baada ya kukasirishwa sana kwa kuendewa kinyume, Bi Gibney, mhudumu wa afya, akageuka kuwa mchunguzi na kugundua mumewe alimdanganya mpaka mama yake mwenyewe, ambaye alihudhuria harusi hiyo ya pili pamoja na mtoto wa kambo, ili kuwashawishi kwamba tayari walishatalakiana.
Bi Gibney alizungumzia ‘uchungu’ alioupata baada ya mume huyo walioachana, ambaye ana kipato cha paundi 85,000 kwa mwaka bila kukatwa kodi, alipoondoka mahakamani baada ya kukiri kuwa na wake wawili. Badala ya kumfunga jela jaji amemtoza faini ya paundi 85.
‘Wakati akioa mke mwengine tulikuwa tumeoana miaka 17,’ alisema. ‘Niliithamini ndoa yangu na nilimpa heshima, imani, mapenzi na kila kitu.
Mahakamani ilijulikana kuwa Bi Gibney aligundua kuhusu siri hiyo nzito Februari mwaka jana.
Baada ya kuona watu wakitoa maoni yao Facebook, alishtuka alipobonyeza ukurasa wa Bi Prudhoe na kukuta picha za mumewe, mwenye umri wa miaka 49, aliyevaa suti ya rangi ya maziwa, akimbusu na kumtazama machoni kwa mahaba mke wake mpya.
Chanzo: Dailymail.co.uk
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu
Friday, 24 October 2014
WANAWAKE 'WAGOMA' KUFANYA MAPENZI, SUDAN K
Kuna zaidi ya wakimbizi wa ndani milioni 1.4 Sudan kusini |
Wanaharakati wa kuleta amani wanawake Sudan Kusini wamependekeza kuwe na mgomo wa kitaifa wa kutofanya mapenzi ili kusimamisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Wanaharakati hao wanataka wanawake wawaunge mkono kwa matumaini ya kuwa itawashawishi wanaume kutafuta suluhu ya amani kutokana na mgogoro uliopo.
Gazeti la Sudan Tribune limeripoti kuwa wazo hilo lilitolewa katika mkutano wa zaidi ya wanaharakati wa kike 90, wakiwemo wabunge, katika mji mkuu wa Sudan kusini, Juba.
Waandalizi wa mkutano huo walisema, “Pendekezo kuu ni kuwashawishi wanawake wa Sudan kusini kuwanyima haki ya kufanya mapenzi waume zao mpaka amani irejee nchini”.
Serikali ya Sudan kusini imekuwa ikipigana na waasi tangu Desemba 2013.
Maelfu ya watu wamekimbilia nchi jirani, na watu milioni 1.4 ni wakimbizi wa ndani kutokana na mgogoro huo, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Chanzo: BBC
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu
Subscribe to:
Posts (Atom)