Sunday, 26 October 2014

CHID BENZ ANASWA NA DAWA ZA KULEVYA



Msanii wa muziki wa Hiphop nchini Rashid Makwiro maarufu ‘Chid Benz’, jana alasiri alikamatwa na dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi, Kamanda wa Polisi  wa Viwanja vya Ndege, ACP Hamis Selemani, alithibitisha kukamatwa kwa Chid Benz na kwamba bado anaendelea kushikiliwa na polisi.

“Msanii huyu tumemkamata hapa airport akijaribu kuvuka na dawa za kulevya kinyume cha sheria  akielekea jijini Mbeya. Alikuwa katika hatua za ukaguzi kwa ajili ya kupanda ndege ya Fastjet kuelekea Mbeya akiwa na wenzake,” alisema.

Akivitaja vitu alivyokamatwa navyo, ACP Selemani alisema msanii huyu amekutwa na kete 14 zinazodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya na mpaka sasa bado wanaendelea uchunguzi kubaini ni aina gani za dawa hizo.

“Mtuhumiwa huyu tumemkamata na kete 14 pamoja na misokoto miwili ya bangi, ambayo alikuwa ameiweka katika mfuko wa shati alilokuwa amevaa. Aidha, tumemkuta na kigae kidogo cha chungu pamoja na kijiko, vitu vya maandalizi ya kutumia dawa hizo na hivi vyote vimekutwa katika begi lake,” alisema.

Alisema hivi sasa msanii huyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi, “Bado tunaendelea kumshikilia na tutahakikisha sheria inafuatwa kama inavyokuwa kwa watuhumiwa wengine wanapokamatwa na vitu kama hivi,” alisema kamanda huyo.

Msanii huyo alikuwa anakwenda jijini Mbeya,  kwa ajili ya kushiriki onyesho la ‘Instagram Party’ linalotarajiwa kufanyika leo jijini humo.

Chidi Benz alikuwa ameongozana na msanii mwenzake Nurdin Bilal maarufu ‘Shetta’, baada ya kukamatwa na polisi, Shetta aliendelea na ukaguzi kwa ajili ya kupanda ndege kuelekea Mbeya.

Julai mwaka jana wasanii wawili Melisa Edward na mwenzake Agnes Gerald ‘Masogange’  walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oriver Tambo nchini Afrika Kusini, wakiwa na dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine takriban kilo 150, zilizokuwa na thamani ya Sh6.8 bilioni.

No comments:

Post a Comment