Friday, 24 October 2014
RAIS KIKWETE: KAZI YA URAIS SI MASKHARA
Rais Jakaya Kikwete amesema kazi ya urais ni ngumu na anatamani amalize kipindi chake ili awe mtu huru kufanya mambo yake, ikiwamo kilimo, huku akiamini atapatikana Rais bora kuiongoza vizuri zaidi Tanzania kuliko yeye.
Rais Kikwete alisema hayo Beijing alipokuwa akizungumza na mabalozi wa Afrika wanaowakilisha mataifa yao nchini China.
Kwenye mkutano huo uliofanyika kwenye Nyumba ya Wageni wa Serikali ya China ya Diaoyutai, Rais Kikwete katika shughuli yake ya kwanza ya ziara rasmi ya siku sita kwa mwaliko wa mwenyeji wake, Rais Xi Jinping.
“Ni kweli naona kama muda hauendi kwa kasi ya kutosha ili niweze kuwa raia wa kawaida na nipate muda wa kuchunga ng’ombe na mbuzi wangu, nilime mananasi yangu kwa nafasi ya kutosha,” alisema Rais Kikwete kwenye mkutano huo baada ya naibu balozi wa Nigeria, Sola Onadipe kuelezea kushangazwa na kauli yake ya kutamani muda wake wa uongozi ufike ili apumzike.
“Kwanza utaratibu huu wa miaka mitano au miaka 10 ni wa kikatiba, ni jambo lililoko katika Katiba yetu na hatuna kishawishi cha kulibadilisha.
“Pili, kazi hii ya urais ni ngumu sana. Kwa hakika nawaonea gere sana wenye nguvu na ubavu wa kutaka kubakia kwenye kazi hii kwa miaka mingi. Pengine wana nguvu zaidi kuliko mimi,” alisema Rais Kikwete.
“Lakini pia kuna uzuri katika mfumo huu wa kwetu kwa sababu kila baada ya miaka mitano na hata kama ni baada ya kila miaka 10, anaingia mtu mwingine madarakani akiwa na fikra mpya na mawazo mapya.”
Rais Kikwete alisema mfumo huo unamridhisha na hakuna kinachomshawishi abakie madarakani zaidi ya muda wa kikatiba.
Chanzo: mwananchi.co.tz
“Nina hakika, nchi yetu itapata kiongozi mwingine, bora kuliko hata mimi, kuongoza vizuri nchi yetu,” alisema Rais Kikwete ambaye aligombea urais kwa mara ya kwanza mwaka 1995, lakini akashindwa kwenye kura ya maoni ndani ya CCM.
Awali Balozi Onadipe alisema kuwa lingekuwa jambo la maana kwa Afrika kama viongozi wengine wangekuwa na mawazo ya namna hiyo ya kuheshimu Katiba za nchi zao na kung’atuka kwenye uongozi muda wao unapowadia.
Rais Kikwete pia alisema siyo busara kwa kiongozi kuwasikiliza wale wanaoshauri wakisema kuwa akiondoka madarakani nchi itavurugika.
“Hawa wanatetea masilahi yao tu wakisema kuwa ukiondoka wewe madarakani, wao hawatakuwa tena mabalozi au mawaziri au nafasi nyingine yoyote.”
Utawala bora
Akizungumzia utawala bora katika Afrika, Rais Kikwete alisema ni jambo la kusikitisha kuwa katika enzi za sasa za utawala bora, baadhi ya Serikali na viongozi wa Afrika bado wanaua na kutesa raia wao kwa kisingizio kuwa utawala bora siyo mfumo wa Kiafrika.
Rais Kikwete alisema mpango wa nchi za Afrika Kujithamini Kuhusu Utawala Bora (APRM) ni mfumo mzuri ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza kiwango cha udikteta.
“APRM ni chombo murua. Kimesaidia kuboresha mifumo yetu ya utawala bora, hata kama bado wapo watu wanaosema kuwa APRM na falsafa yake ni jambo la Wazungu jambo ambalo siyo la kweli kwa kutilia maanani faida za mfumo huu wa kujithamini wenyewe,” alisema Rais Kikwete.
“Hivi tunahitaji wazungu kuja kutufundisha kuwa ni jambo baya kuua raia wako? Unahitaji mzungu aje kukwambia kuwa ni jambo baya kuwafanyia ukatili na unyama wananchi wako?”
Rais Kikwete alisema kuwa mageuzi na mabadiliko ya kidemokrasia katika nchi za Afrika ni jambo zuri na la lazima na kuwa viongozi wa Afrika lazima waendelee kukumbatia, kulea na kuendelea kujenga demokrasia.
Wanasiasa wamkosoa
Akizungumzia kauli ya Rais Kikwete kwamba anatamani kumpumzika, naibu katibu mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika alisema Rais alipaswa kuwa na hamu ya kupumzika tangu uchaguzi wa mwaka 2010 badala ya kusema hayo sasa wakati amefika kikomo cha kugombea.
“Kusema ana hamu ya kupumzika sasa ni kuwapaka Watanzania mafuta kwa mgongo wa chupa,” alisema Mnyika, ambaye pia ni mbunge wa Ubungo.
Alisema Rais Kikwete ameiacha nchi katika utata mkubwa wa Katiba na sasa muda umekwisha anadai kuwa ana hamu ya kuondoka Ikulu.
“Nimtakie heri kama kiongozi wangu, lakini ajue kuwa udhaifu wake ndiyo ulioifikisha nchi hapa ilipo,” alisema Mnyika.
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila alimshauri Rais Kikwete afanye mihadhara ya kitaaluma ili arithishe ujuzi wake kwa wengine baada ya kumaliza muda wake badala ya kurudi kijijini kulea wajukuu na mifugo pekee.
“Ingawa ana hamu ya kustaafu, lakini yapo mengi ambayo hajayatimiza kiasi ambacho hata nchi wahisani wanamlaumu,” alisema.
Kafulila alisema Rais ameshindwa kutimiza ahadi ya maisha bora kwa kila Mtanzania, elimu, utawala bora na ufisadi.
Naibu katibu mkuu wa CUF (Bara), Magdalena Sakaya alisema kauli ya Rais kwamba ana hamu ya kumaliza muda wake inaonyesha kuwa hakuwa na malengo ya kuibadili nchi.
Sakaya alisema Watanzania wameshuhudia maisha duni kuliko ilivyowahi kutokea katika uongozi wowote ule kwa kuwa Rais Kikwete ameshindwa kusimamia mtiririko wa fedha na rasilimali.
“Ugumu wa maisha upo palepale. Hakuna alichobadili zaidi ya safari za nje ya nchi zisizokuwa na msingi,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitengo cha siasa, Dk Benson Bana aliusifu uongozi wa Kikwete na kusema kuwa amefanya mambo mengi kulingana na uwezo wa nchi na rasilimali ilizonazo.
“Amepanua uhuru wa demokrasia na amekuza miundombinu na hata suala la usalama alilizingatia kwa sababu ujambazi umepungua kwa kiasi kikubwa,” alisema.
Dk Bana alisema, Rais ana haki ya kusema kuwa ana hamu ya kupumzika kwani amefanya kazi yake na kuimaliza.
Wanaharakati wamkosoa
Mkurugenzi mstaafu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake, (Tamwa), Ananilea Nkya alisema Rais Kikwete anaiacha nchi katika mpasuko mkubwa baada ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa isiyokuwa na maridhiano.
“Sitaki kuwa mnafiki kwa Rais Kikwete, hata akilima mananasi hayatamsaidia kwa sababu ameiacha nchi katika mpasuko, Katiba Inayopendekezwa haina maridhiano,” alisema.
Nkya alisema Rasimu ya Tume ya Mabadiliko, ilipendekeza mambo makubwa, lakini mchakato huo uliharibika na Katiba Inayopendekezwa ikapitishwa kichama na kiushkaji.
“Angeacha Katiba bora, ingemsaidia hata yeye atakapokuwa amestaafu na kuwa mkulima,” alisema.
Labels:
Habari
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment