Tuesday, 28 October 2014
EBOLA: BENKI YA DUNIA YATAKA WATU KUJITOLEA
Rais wa Benki ya Dunia ametoa wito kwa maelfu ya wahudumu wa afya kujitolea na kujaribu kusaidia kuzuia kuenea zaidi kwa mlipuko wa Ebola Afrika magharibi.
Jim Yong Kim alisema takriban watabibu 5,000 na wafanyakazi wengine wanahitajika kupambana na ugonjwa huo.
Wengi waliokuwa na sifa stahili wana woga wa kwenda Afrika magharibi, aliongeza.
Mlipuko wa sasa wa Ebola umewaathiri zaidi ya watu 10,000 na kuua takriban watu 5,000.
Mkuu huyo wa Benki ya Dunia Bw Kim aliyasema hayo wakati wa ziara yake nchini Ethiopia, ambapo aliungana na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini-Zuma.
RWANDA YAFANYA VYEMA USAWA WA KIJINSIA
Ushiriki wa wanawake zaidi katika siasa na kazi nyingine imepunguza idadi ya utofauti wa kijinsia duniani katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, Jukwaa la Kiuchumi Duniani (WEF) limesema.
Utafiti wa mwaka wa jinsia wa WEF umethibitisha “mabadiliko makubwa” katika nchi nyingi, huku nchi 105 zikiwa na usawa tangu mwaka 2005, mwandishi wa ripoti hiyo amesema.
Iceland ndio inaongoza kwa miaka sita mfululizo, huku Yemen ikishikilia mkia.
WEF imeangazia zaidi uchumi, afya, elimu na ushiriki wa kisiasa katika nchi 142.
Mataifa sita tu - Sri Lanka, Mali, Croatia, Macedonia, Jordan na Tunisia – yameshuhudia usawa wa kijinsia kuongezeka kwa ujumla tangu mwaka 2005, kulingana na WEF.
Moja ya sababu za mafanikio ya Iceland ni idadi ndogo ya watu nchini humo wakati Yemeni ina idadi kubwa ya vifo na watoto wengi wa kike wenye umri wa miaka sita hadi 14 hawajawahi kuhudhuria shule
Rwanda yafanya vyema
Mataifa ya Nordic yanaongoza, huku Finland, Norway na Sweden yanaifuata Iceland katika tano bora.
Uingereza imeshuka kwa nafasi nane duniani na kufikia nafasi ya 26.
Rwanda imeingia katika orodha hiyo kwa mara ya kwanza na kuchukua nafasi ya saba, na kuifanya nchi yenye mafanikio makubwa kiuchumi barani Afrika.
Mwandishi wa ripoti hiyo Saadia Zahidi alisema mafanikio ya Rwanda ni kwasababu kuna karibu idadi sawa ya wanawake na wanaume wenye ajira – na katika ofisi za wizara – na badala yake huduma za afya na elimu zimeimarika.
Mabadiliko ya mapato ya wanawake ndio iliyoiporomosha Uingereza, ilisema WEF.
Msukosuko wa uchumi ndio umesababisha utofauti wa kipato wa kijinsia kuongezeka Uingereza.
Kutaka kujua zaidi na kujua nchi yako iko nafasi ya ngapi, Bonyeza hapa
http://www.bbc.co.uk/news/world-29722848
Monday, 27 October 2014
BINTI AJIRUSHA GHOROFANI BAADA YA KUTAPELIWA
Workers House nchini Uganda |
Mwanamke mmoja amejirusha kutoka ghorofa ya 14 katika jumba liitwalo Workers House nchini Uganda na kufa baada ya kugundua ‘kaingizwa mjini’ alipokuwa akipeleka pesa nyumbani wakati akifanya kazi Dubai.
Annet Ashaba, mwenye umri wa miaka 26, kutoka wilaya ya Sembabule, alirejea Oktoba 16 na kugundua alitapeliwa fedha zake alizotuma kwa ndugu yake Uganda kumjengea nyumba.
“...ndugu zake walituambia alituma pesa kwa shemeji yake mmoja kumnunulia kiwanja na baadae akatuma ziada kwaajili ya ujenzi. Lakini Ashaba aliporejea alikuta kiwanja kimenunuliwa lakini nyumba iliyojengwa siyo aliyotegemea,” alisema msemaji wa polisi wa Kampala Patrick Onyango.
Alisema ndugu zake Ashaba aliwaonya kuwa jambo baya linaweza kumtokea.
“Alipofika ghorofa ya 14, alifunga mdomo wake kwa kitambaa halafu akaruka,” Bw Onyango alisema.
Ashaba si wa kwanza kujirusha kutoka Workers House. Septemba 2009, Baker Kilenzi, mwenye umri wa miaka 23, alikata shingo yake mwenyewe kwenye ghorofa ya nane baada ya kuachana na mpenzi wake.
Wiki hiyohiyo, Moses Siraji, mwenye miaka 24, akifanya kazi kwenye kampuni ya mafuta, alijirusha kutoka ghorofa ya 14 na kufa.
Mwaka 2012, binti mmoja aliyehitimu chuo kikuu alijirusha na kufariki dunia baada ya miaka mingi ya kusaka ajira bila mafanikio.
Chanzo: monitor.co.ug
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu
MLINDA MLANGO WA AFRIKA KUSINI AUAWA
Msako mkali unafanyika
kutafua wauaji wa Kapteni wa soka wa
Afrika kusini Senzo Meyiwa, polisi wamesema.
Wametangaza kutoa
zawadi ya rand 250,000 (£14,100;
$22,800) kwa taarifa zozote zitakazosaidia kukamatwa kwa wanaoshutumiwa kuwa
wezi waliompiga risasi na kumwuua.
Imeripotiwa alishambuliwa
baada ya wanaume wawili kuingia kwenye nyumba ya mpenzi wake huko Vosloorus,
kusini mwa Johannesburg.
Watu
hao waliingia na kutaka watoe simu zao za mkononi na mali nyingine. Mwanamme
mwengine wa tatu alibaki nje.
Mmoja
miongoni mwa wawili hao ameelezewa na polisi kuwa mrefu, mweusi, mwembamba na
mwenye rasta, na mwengine ni mfupi, mweusi na mkuza.
Rais Jacob Zuma alitoa
salaam za rambirambi kwa mlinda mlango huyo, akisema, “hakuna maneno yanayoweza
kuelezea mshtuko taifa limepata kutokana na kifo hicho”.
Wakala wake amemwelezea
kuwa mtu asiyekuwa na makuu, aliyetoka katika maisha magumu na kufanikiwa kuwa “shujaa
katika jicho la kila mmoja”.
Kijana huyo mwenye
umri wa miaka 27 alikuwa mlinda mlango wa Orlando Pirates na aliichezea Afrika
kusini katika mashindano manne ya mwisho ya mechi za kufuzu kombe la Mataifa
Afrika.
Siku ya Jumamosi,
alikuwa na klabu yake, walipovuka nusu fainali ya kombe la Ligi la Afrika
kusini, baada ya kuinyuka Ajax Cape mabao 4 -1.
QATAR YAKANA KUWAFADHILI IS
Maafisa waandamizi kutoka Qatar wamekana vikali madai kuwa nchi hiyo inaunga mkono makundi ya kigaidi nchini Syria kama vile kundi linalojiita Islamic State IS.
Wameiambia BBC kwamba Qatar ilitoa misaada kwa wapiganaji wa wastani tu, wakishirikiana na shirika la kijasusi la Marekani CIA, na mashirikia mengine ya kijasusi ya Kiarabu na nchi za magharibi.
Udhibiti mkali wa fedha nao umewekwa, waliongeza.
Kauli hizo zimetolewa kabla ya ziara ya kiongozi wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani nchini Uingereza wiki hii.
Mapema mwezi huu iliripotiwa kuwa wabunge kadhaa walihoji ukaribu wa Uingereza na Qatar, huku kukiwa na madai kuwa wana uhusiano na kundi la IS.
Mwandishi wa ulinzi wa BBC alisema Qatar, mwekezaji mkuu wa Uingereza, ameshtushwa sana na madai hayo.
UPINZANI WAANDIKA HISTORIA TANZANIA
Sehemu ya wanachama wa NCCR - Mageuzi, CUF, NLD na Chadema wakionyesha alama ya vidole vitatu wakati wa utiaji saini makubaliano ya ushirikiano baina ya vyama hivyo jana kwenye viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam. |
Vyama vya upinzani vimeandika historia mpya tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, baada ya vyama vinne vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kutiliana saini makubaliano saba ya ushirikiano, kubwa ikiwa kusimamisha mgombea mmoja katika kila ngazi ya uchaguzi kuanzia sasa.
Tukio hilo lilifanywa na viongozi wakuu wa NCCR-Mageuzi, Chadema, CUF na NLD jana katika Viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi, wakiwamo viongozi wa dini na taasisi mbalimbali.
Akisoma makubaliano hayo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alianza kwa kueleza historia ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba ya Tanganyika na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ilitengenezwa kwa muundo wa chama kimoja cha siasa (CCM)... “ilifanyiwa marekebisho mwaka 1992 baada ya kuanza mfumo wa vyama vingi.
Mwaka 2011 tulianza mchakato wa kuandika Katiba Mpya, ilipatikana Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya wananchi lakini maoni hayo yameondolewa katika Katiba Inayopendekezwa.”
Alisema kitendo cha kuachwa kwa maoni ya wananchi yaliyokuwa katika Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba, kimesababisha athari katika matukio muhimu ya kidemokrasia.
Akitaja makubaliano hayo, saba aliyosema yana lengo la kuzaa Tanzania Mpya, Dk Slaa alisema, “Jambo la kwanza ni kuhusisha sera za vyama vyetu na kuchukua yale yote yanayofanana ili tumwe na kauli zinazolingana na kufanana kwa Watanzania.”
Sunday, 26 October 2014
HUKUMU YA KIFO YA BI JABBARI YATEKELEZWA
Bi Jabbari alitengwa kwa miezi miwili baada ya kukamatwa na kesi yake kuanza mwaka 2008 |
Iran imeendelea na kutekeleza hukumu ya kifo kwa mwanamke mmoja licha ya kampeni ya kimataifa ya kusihi hatua hiyo isitishwe.
Reyhaneh Jabbari, mwenye umri wa miaka 26, aliuliwa kwa kunyongwa kwenye gereza la Tehran siku ya Jumamosi asubuhi.
Alitiwa hatiani kwa kumwuua mwanamme mmoja ambaye alisema alikuwa akijaribu kumdhalilisha kijinsia.
Jabbari alikamtwa mwaka 2007 kwa mauaji ya Morteza Abdolali Sarbandi, aliyekuwa mfanyakazi wa wizara ya masuala ya kijasusi.
Mama yake Bi Jabbari's, Shole Pakravan, aliiambia BBC alimtembelea binti yake muda kidogo kabla ya hukumu hiyo kutekelezwa.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani na Uingereza zote zimelaani mauaji hayo.
"Umoja wa Mataifa umesema kutiwa kwake hatiani kulitokana na madai aliyoyatoa baada ya kupewa vitisho. Ninasihi Iran kuahirisha hukumu zote za kifo," alisema waziri wa mambo ya nje wa Uingereza.
Kampeni ya kutoa wito wa kusitisha mauaji hayo yalianzishwa katika mitandao ya kijamii ya Facebook na Twitter mwezi uliopita na ilionekana iliweza kusimamisha kifo hicho kwa muda tu.
Hatahivyo, shirika la habari la serikali Tasnim lilisema Jumamosi kuwa hukumu hiyo ya kifo kwa Jabbari ilitekelezwa baada ya ndugu zake kushindwa kupata msamaha kutoka kwa familia ya Morteza.
Lilisema madai yake ya kumwuua kwa minajil ya kujilinda haikuweza kuthibitishwa mahakamani.
Ukurasa wa Facebook ulioanzishwa sasa unasema “Mungu amlaze pahala pema”.
Subscribe to:
Posts (Atom)