Serikali ya China inachunguza kutoweka kwa zaidi ya
wanawake 100 wa Vietnam katika jimbo la Hebei kaskazini mwa nchi hiyo, vyombo
vya habari nchini humo vimesema.
Wanawake hao waliozeshwa kupitia mtu anayewaunganisha na
wanaume ‘matchmaker’ wanaoishi vijijini karibu na Handan, lakini alitoweka
mwezi Novemba, ripoti hiyo ilisema.
Mwuunganishaji huyo, mwanamke wa Vietnam anayeishi China,
naye ameingia mitini.
Uwiano wa wanawake na wanaume China mara nyingine
husababisha wanaume makapera walio maskini kutafuta maharusi kutoka nchi za
kusini mashariki mwa Asia.
Makapera hao kila mmoja amelipa maelfu ya yuan kwa mwuunganishaji huyo wa Vietnam, ambaye anajulikana kwa jina la Wu Meiyu, aliyekuwa akiishi Hebei kwa zaidi ya miaka 20.
Mapema mwaka huu alitembelea vijiji mbalimbali huko Hebei akitafuta wateja, akiwaahidi kuwapa mke kutoka Vietnam kwa malipo ya yuan 115,000 ($18,600; £11,800), ripoti hiyo ilisema.
Novemba 20, wake waliwaambia waume zao kuwa walikuwa wanaenda kula chakula na maharusi wengine wa Vietnam
Ghafla wakawa hawapatikani.
Waume hao walipoenda nyumbani kwa Bi Wu kukabiliana naye, waligundua aliondoka siku chache zilizopita.