Huduma za reli baina ya Tanzania na Zambia zimesita
kutokana na mgomo wa zaidi ya wafanyakazi 1,500 kutoka Tanzania.
Afisa mmoja wa umoja wa wafanyakazi alisema wafanyakazi hao hawajalipwa kwa
miezi mitano na serikali ya Tanzania kutokana na mgogoro wa fedha katika
mamlaka hizo za reli.
Serikali bado haijatoa kauli yoyote kuhusiana na tukio hilo.
China imefadhili ujenzi wa reli hiyo, ambayo ina kilomita 1,860 (1,155 maili
), katika miaka ya 70 kwa nia ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo jirani.
Iliwapa serikali ya nchi hizo mbili mkopo usio na riba wa dola za kimarekani
milioni 500 kila mmoja, kwa ajili ya mradi huo.
Hatahivyo, Mamlaka za Reli ya Tanzania- Zambia, iliyoundwa na serikali hizo
mbili, inaendesha shughuli zake kwa hasara, alisema mwandishi wa BBC aliyopo
mjini Dar es Salaam.
Mamlaka hiyo inamsaka mwekezaji kwa udi na uvumba kuinusuru, kwani serikali
za Tanzania na Zambia zinasita kuendelea kuifadhili reli hiyo, aliongeza.
Watu wa vijijini aghlabu hutumia huduma hizo za reli. Na pia hutumiwa
kusafirisha mizigo, hasa shaba na mbao, kutoka Zambia kuelekea Tanzania,
alisema mwandishi huyo.
Afisa wa Jumuiya ya Wafanyakazi wa Reli Tanzania Erastus Kihwele ameiambia
BBC Focus on Africa kuwa serikali hizo mbili zingetafuta “fedha za dharura”
kulipa wafanyakazi.
Alisema wengi wao hawana pesa za kulipa kodi
za nyumba au ada za shule kwa ajili ya watoto wao kwasababu hawajalipwa
mshahara kwa miezi mitano.
Mgomo huo unatarajiwa kudumu kwa wiki moja, lakini unaweza kuendelea zaidi
kama matakwa yao hayakutekelezwa, Bw Kihwele aliongeza.