 |
| Waandamanaji wakiwa kituo cha televisheni cha taifa wakitarajia upinzani kutangaza lolote |
Televisheni ya taifa ya Burkina Faso imetolewa hewani, muda
mchache baada ya askari kufyatua risasi kwenye makao yake makuu, na kuwalazimisha
waandamanaji na waandishi wa habari kutawanyika.
Wakati huo huo kwenye mji mkuu, Ouagadougou askari
waliwatawanya maelfu ya waandamanaji na kuweka vizuizi eneo hilo.
Askari walishika madaraka siku ya Ijumaa baada ya
kiongozi wa muda mrefu Blaise Compaore kuachia ngazi kufuatia maandamano ya
siku kadhaa.
Umoja wa Mataifa umelaani jeshi kuchukua hatamu na kutishia kuweka vikwazo.
Mjumbe wa Afrika magharibi Mohamed Ibn Chambas alisema jeshi lazima liruhusu
uongozi wa kiraia.
Jeshi lilimtangaza Lt Kanali Isaac Zida kuwa kiongozi wa serikali ya mpito
siku ya Jumamosi.
Maelfu ya waandamanaji walikusanyika maeneo mbalimbali mjini Ouagadougou siku
ya Jumapili kulipinga jeshi.
 |
| Kiongozi wa upinzani Saran Sereme alipofika kituo cha televisheni cha taifa kabla tu risasi kufyatuliwa |
Kulikuwa na tafrani wakati kiongozi wa upinzani Saran Sereme na aliyekuwa
waziri wa ulinzi Kwame Lougue walipowasili kwenye makao makuu ya televisheni
hiyo ya taifa.
Watu hao waliokusanyika waliamini Be Sereme alikuwa anatarajia kutangaza kuongoza
serikali hiyo ya mpito, mwandishi wa BBC aliyopo Ouagadougou Laeila Adjovi aliripoti.
Taarifa zinasema Jenerali mstaafu Lougue naye alikusudia kutangaza kutaka
kuongoza nchi hiyo wakati huo pia.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya kuwasili, risasi zikaanza kurushwa hivyo
wafanyakazi na waandamanaji wakaanza kukimbia.