Friday, 9 January 2015
MTOTO WA JACKIE CHAN AFUNGWA JELA
Jaycee Chan, mtoto wa kiume wa muigizaji nyota Jackie Chan, amefungwa jela miezi sita kwa kosa linalohusiana na dawa za kulevya.
Chan, mwenye umri wa miaka 32, alikiri kosa kwenye mahakama ya wilaya ya Dongcheng, Beijing kwa “kuhifadhi watu wengine kutumia dawa za kulevya.”
Polisi walivamia nyumbani kwake mwezi Agosti na kukuta zaidi ya gramu 100 za marijuana.
Alikabiliwa na kifungo cha miaka mitatu.
Kukamatwa kwake kulifanyika wakati wa msako mkali wa dawa za kulevya China ambapo watu maarufu kadhaa walijikuta wakikamatwa.
Juni 2014, Rais Xi Jinping walimwamuru polisi kutumia hatua kali kuzuia matumizi ya dawa za kulevya.
Kukiri kwa mtoto wa mmoja wa waigizaji maarufu China kunatoa ujumbe muhimu kutoka serikali ya China: hakuna mwenye kinga ya kukamatwa inapokuja suala la dawa za kulevya.
YAYA TOURE: MCHEZAJI BORA AFRIKA
Kiungo wa Manchester City Yaya Toure amekuwa mchezaji wa kwanza kutajwa kuwa mshindi wa tuzo ya CAF wa mchezaji bora wa Afrika kwa miaka minne mfululizo.
Toure, mwenye umri wa miaka 31, alitajwa kuwania tuzo hiyo baada ya kuchangia kwa kiasi kikubwa kushinda Ligi Kuu ya England na Kombe la Ligi.
Pia aliisaidia Ivory Coast kufuzu kucheza kwa Kombe la Mataifa ya Afrika 2015.
Toure ameweza kuwashinda mshambuliaji wa Gabon Pierre-Emerick Aubameyang na mlinda mlango wa Nigeria Vincent Enyeama.
Kiungo Toure alitajwa miongoni mwa wachezaji wa kuwania tuzo ya Ballon D’Or 2014 ya Fifa mwezi Oktoba.
VIONGOZI WA DINI YA KIISLAM 'WATOWEKA' UGANDA
Viongozi wanne wa Kiislamu katika mji mkuu wa Uganda, Kampala wametoweka baada ya kuchukuliwa na watu wasioweza kutambuliwa, kiongozi wa jumuiya alisema.
Mkuu wa kundi la Kiiislamu la Tabliq aliiambia BBC “walitekwa” kutoka nyumbani kwao au sehemu za kazi.
Polisi bado hawajaanza kufanya uchunguzi kwani bado haijaripotiwa rasmi kuwa wametoweka, msemaji aliiambia BBC.
Haiko wazi kama kutoweka kwao kuna uhusiano na kupigwa risasi kwa viongozi wawili wa Kiislamu mwezi Desemba.
Mmoja alikuwa mkuu wa jumuiya ya Kishia ya Uganda, ambaye alipigwa risasi mashariki mwa Uganda na watu walio kwenye pikipiki Desemba 25, mwengine alikuwa kiongozi wa Tabliq aliyepigwa risasi kwenye gari lake Desemba 28 mjini Kampala.
Polisi wamenyooshea kidole mauaji hayo kwa waliobaki katika kundi la Allied Democratic Forces (ADF), kundi la waasi la Uganda lenye makao yake makuu nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kundi hilo linaongozwa na Jamil Mukulu, ambaye kabla ya kuanza vuguvugu hilo, alikuwa kiongozi mwenye msimamo mkali ndani ya kundi la Tabliq katika miaka ya 90.
Mwandishi wa BBC alisema kumekuwa na mgongano wa uongozi ndani ya jumuiya ya Tabliq.
Viongozi wa Tabliq ambao hawajulikani walipo:
Yusuf Kakande, Siraj Kawooya , Twaha Ssekitto na Abdul Salam Sekayengo
Viongozi waliouawa mwezi Desemba:
Abdu Kadir Muwaya, kiongozi wa Kishia – aliipinga ADF
Sheikh Mustafa Bahiga, kiongozi wa Tabliq – aliyekuwa polisi na kuhusishwa katika mzozo wa uongozi ndani ya kundi hilo.
Thursday, 8 January 2015
KENGE 140 WANASWA WAKITOROSHWA NJE YA NCHI
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl Julius Nyerere |
Jeshi la Polisi la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)linamshikilia raia wa Kuwait kwa tuhuma za kukutwa na viumbe hai aina ya Kenge 149 wenye thamani ya Sh 6.3 milioni.
Kamanda wa Polisi wa JNIA, Khamis Suleiman alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Hussain Ahmed Ally Mansour(34), raia wa Kuwait ambaye alikamatwa uwanjani hapo jana majira ya saa 5 usiku wakati akijiandaa na safari ya kuelekea nchini Kuwait kupitia Dubai na Shirika la Ndege la Emirates .
Kamanda Selemani alisema Mansour alikamatwa na wanyama hao ambao aliwahifadhi kwenye mifuko midogo midogo ilivyowekwa katika begi kubwa lenye rangi nyeusi.
“Kenge waliwekwa kwenye mifuko midogo midogo 15 na kila mmoja kuna kenge 15 na mifuko mingine walikaa wawili,”alisema kamanda Selemani.
Alisema kati ya Kenge hao, 15 walikufa na walio hai walikuwa 134 ambao walikuwa wamefichwa kwenye mifuko hiyo.
AL-SHABAB YAUA 'MASHUSHUSHU WA CIA NA ETHIOPIA'
Kundi la wapiganaji la Somalia al-Shabab limewaua kwa kuwamiminia risasi watu wanne wanaoshutumiwa kuwa ‘mashushushu’ wa shirika la Marekani CIA na mashirika mengine ya kijasusi.
Watu hao, wakiwemo wanajeshi wawili wa serikali, walipigwa risasi mbele ya mkusanyiko wa watu wengi katika mji wa Bardhere kusini mwa nchi hiyo, walioshuhudia walisema.
Mahakama inayoendeshwa na al-Shabab awali iliwatia hatiani kwa kufanya uchunguzi kwa niaba ya CIA, Ethiopia na serikali ya Somalia.
Mashambulio ya anga ya Marekani yameua makamanda wawili waandamizi wa al-Shabab katika miezi ya hivi karibuni.
Wednesday, 7 January 2015
JINO LA MTU KUKUTWA KWENYE CHIPSI McDONALD
McDonald imeomba radhi baada ya jino la binadamu kukutwa
kwenye chipsi za mteja mmoja nchini Japan mwaka jana.
Mteja mmoja alitoa malalamiko baada ya kugundua hilo
Agosti mwaka jana.
McDonald imesema uchunguzi huru uligundua kuwa ni jino la
binadamu.
Kampuni hiyo pia imekiri kuwepo na plastiki ndani ya malai ‘ice-cream’ na ngozi ya plastiki ya kutengeneza mikoba ilikutwa kwenye kuku.
Wakurugenzi wa McDonald walisema watalifanyia kazi suala hilo ili matukio kama hayo yasitokee tena.
McDonald imekabiliwa na matatizo mengi Japan katika siku za karibuni, ikiwemo upungufu wa chipsi ambapo iliwalazimu kuagiza kutoka Marekani.
Katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumatano, wakurugenzi hao walisema uchunguzi ulionyesha jino hilo halikupikwa.
“Hatujafanikiwa kugundua jino hilo liliingia vipi kwenye chakula," alisema.
Mwanamke aliyekuta jino awali alidai mfanyakazi mmoja alimwambia jino hilo lilikaangwa.
Chanzo: dailymail.co.uk
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu
MUHAMMAD ALI ATOLEWA HOSPITALI
Picha imepigwa 2006 |
Bondia wa mabondia Muhammad Ali ametolewa hospitalini
baada ya kulazwa mwezi uliopita alipopatwa na maambukizi katika njia ya mkojo.
Aliyekuwa bingwa mara tatu wa uzani wa juu wa masumbwi duniani, amerejea nyumbani baada ya kutolewa siku ya Jumanne, msemaji wa familia alisema.
Bob Gunnell alisema Ali mwenye umri wa miaka 72 amepona kabisa na familia yake inamshukuru kila mmoja kwa sala zao.
Ali alitambuliwa kuwa na ugonjwa wa kutetemeka ‘Parkinsons’ mwaka 1984 baada ya kustaafu ndondi.
Alionekana hadharani mwezi Septemba, eneo alipokuzwa Louisville katika sherehe za kutoa Tuzo za Kutetea Haki za Binadamu za Muhammad Ali.
Jina la hospitali ambapo Ali alitibiwa halijatolewa.
Chanzo:AP
Subscribe to:
Posts (Atom)