Thursday, 8 January 2015
AL-SHABAB YAUA 'MASHUSHUSHU WA CIA NA ETHIOPIA'
Kundi la wapiganaji la Somalia al-Shabab limewaua kwa kuwamiminia risasi watu wanne wanaoshutumiwa kuwa ‘mashushushu’ wa shirika la Marekani CIA na mashirika mengine ya kijasusi.
Watu hao, wakiwemo wanajeshi wawili wa serikali, walipigwa risasi mbele ya mkusanyiko wa watu wengi katika mji wa Bardhere kusini mwa nchi hiyo, walioshuhudia walisema.
Mahakama inayoendeshwa na al-Shabab awali iliwatia hatiani kwa kufanya uchunguzi kwa niaba ya CIA, Ethiopia na serikali ya Somalia.
Mashambulio ya anga ya Marekani yameua makamanda wawili waandamizi wa al-Shabab katika miezi ya hivi karibuni.
Wednesday, 7 January 2015
JINO LA MTU KUKUTWA KWENYE CHIPSI McDONALD
McDonald imeomba radhi baada ya jino la binadamu kukutwa
kwenye chipsi za mteja mmoja nchini Japan mwaka jana.
Mteja mmoja alitoa malalamiko baada ya kugundua hilo
Agosti mwaka jana.
McDonald imesema uchunguzi huru uligundua kuwa ni jino la
binadamu.
Kampuni hiyo pia imekiri kuwepo na plastiki ndani ya malai ‘ice-cream’ na ngozi ya plastiki ya kutengeneza mikoba ilikutwa kwenye kuku.
Wakurugenzi wa McDonald walisema watalifanyia kazi suala hilo ili matukio kama hayo yasitokee tena.
McDonald imekabiliwa na matatizo mengi Japan katika siku za karibuni, ikiwemo upungufu wa chipsi ambapo iliwalazimu kuagiza kutoka Marekani.
Katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumatano, wakurugenzi hao walisema uchunguzi ulionyesha jino hilo halikupikwa.
“Hatujafanikiwa kugundua jino hilo liliingia vipi kwenye chakula," alisema.
Mwanamke aliyekuta jino awali alidai mfanyakazi mmoja alimwambia jino hilo lilikaangwa.
Chanzo: dailymail.co.uk
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu
MUHAMMAD ALI ATOLEWA HOSPITALI
Picha imepigwa 2006 |
Bondia wa mabondia Muhammad Ali ametolewa hospitalini
baada ya kulazwa mwezi uliopita alipopatwa na maambukizi katika njia ya mkojo.
Aliyekuwa bingwa mara tatu wa uzani wa juu wa masumbwi duniani, amerejea nyumbani baada ya kutolewa siku ya Jumanne, msemaji wa familia alisema.
Bob Gunnell alisema Ali mwenye umri wa miaka 72 amepona kabisa na familia yake inamshukuru kila mmoja kwa sala zao.
Ali alitambuliwa kuwa na ugonjwa wa kutetemeka ‘Parkinsons’ mwaka 1984 baada ya kustaafu ndondi.
Alionekana hadharani mwezi Septemba, eneo alipokuzwa Louisville katika sherehe za kutoa Tuzo za Kutetea Haki za Binadamu za Muhammad Ali.
Jina la hospitali ambapo Ali alitibiwa halijatolewa.
Chanzo:AP
'KAMANDA' WA LRA AJISALIMISHA CAR
Ongwen, picha ya mwaka 2008, inasemekana alichukuliwa kuwa jeshi la LRA tangu akiwa mtoto |
Mtu mmoja anayedai kuwa kamanda mwandamizi katika kundi kubwa la waasi la Lord's Resistance Army (LRA) ametiwa kizuizini na jeshi la Marekani.
Mtu huyo, aliyejitambulisha kama Dominic Ongwen,alisalimu amri Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilisema.
Ongwen anasakwa na Mahakama ya Uhalifu wa Kivita akishutumiwa kuhusika na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.
Anadhaniwa na baadhi ya watu kuwa naibu kamanda wa kiongozi wa LRA Joseph Kony.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Jen Psaki alisema mtu huyo alidai kuwa ameasi kundi hilo la LRA.
Joseph Kony, kiongozi wa LRA wamekuwa vitani nchini Uganda na eneo zima kwa zaidi ya miongo miwili.
Chanzo: BBC
Imetafsiriwa na mwandishi wetu
Tuesday, 6 January 2015
UJAUZITO: MBINU YA KUPITISHA DAWA ZA KULEVYA
Baadhi ya wanawake wa Kitanzania waliofungwa katika magereza ya China na Hong Kong, walishika ujauzito kama moja ya mbinu ya kupitisha dawa za kulevya bila kugundulika kwenye viwanja vya ndege na mipaka mingine ya kimataifa. Mwananchi limebaini.
Watanzania wanne walio katika magereza ya China na Hong Kong walijifungua watoto kwa nyakati tofauti wakiwa wanatumikia vifungo na wamekiri kuwa walibeba ujauzito kama mbinu ya kupitisha dawa hizo bila kukaguliwa.
Watoto wanaozaliwa magereza baada ya kufikisha mwaka mmoja hupelekwa katika vituo vya watoto yatima na kusomeshwa na Serikali ya China hadi pale wazazi wao watakapomaliza adhabu.
Imebainika kuwa watoto wawili wapo katika vituo hivyo, mmoja tayari yupo Tanzania baada ya bibi yake kumrejesha na mwingine bado yupo gerezani na mama yake.
Wanawake hao ambao wote wana umri wa kati ya miaka 20 na 30 walieleza masikitiko yao jinsi ambavyo wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya wanavyowarubuni ili kubeba dawa hizo kwa ahadi za kuwapa fedha nyingi.
Monday, 5 January 2015
NEPAL YAANZISHA MABASI YA WANAWAKE TU
Huduma ya basi ya wanawake pekee imeanzishwa kwenye mji mkuu wa Nepal, Kathmandu kupunguza kudhalilishwa kijinsia katika mji wenye njia zilizojaa watu wengi.
Mwenyekiti wa kampuni hiyo alisema nia ni kufanya wanawake wajisikie raha na salama.
Magari manne yenye viti 17 kila mmoja yatafanya safari zake kwenye barabara kuu muda wa shughuli nyingi.
Takriban robo ya mabinti wamedhalilishwa kijinsia katika usafiri wa umma, kulingana na utafiti wa Benki ya Dunia ya mwaka 2013.
Lengo mwishowe ni wafanyakazi wote wa mabasi hayo wawe wanawake |
Mabasi yote Kathmandu hutakiwa kuachia idadi kadhaa ya viti kwa „wanawake tu” kisheria, lakini wakosoaji wanasema sheria hiyo haitekelezwi.
Kwa sasa kuna kondakata mmoja tu mwanamke katika kampuni hiyo lakini Bw Bharat Nepal, mkuu wa jumuiya ya usafiri alisema nia mwisho ni wanawake tu ndio waweze kuiendesha kampuni hiyo.
KAMPUNI YA POMBE KUTUMIA PICHA YA GANDHI
Kampuni moja ya pombe ya Marekani imeomba radhi kwa kutumia picha ya shujaa wa uhuru wa India Mahatma Gandhi kwenye maokpo yake ya bia, taarifa zinasema.
Hatua hiyo ya kampuni ya New England imefanyika baada ya kesi kufunguliwa kwenye mahakama ya India ikisema hatua hiyo “imemdhalilisha” kiongozi huyo.
Gandhi aliongoza mapambano bila vurugu dhidi ya utawala wa Kiingereza nchini India.
Aliuawa Januari,1948, miezi kadhaa baada ya India kupata uhuru.
Pombe hiyo yenye picha ya kiongozi huyo inaitwa Gandhi-Bot.
Katika mtandao wake kampuni hiyo inasema bia hiyo ni “ni namna ya kujitakasa na kusaka ukweli na mapenzi".
Wakili mmoja amefungua kesi mjini Hyderabad, kusini mwa India, akidai kutumia picha ya Ghandi kwenye makopo ya pombe ni “la kulaaniwa” na la kuadhibiwa kutokana na sheria za India.
Kampuni hiyo ilisema inaomba radhi kwa yeyote waliyemwuudhi. Na hakuna dalili zozote za kampuni hiyo kuondosha picha hiyo.
Matt Westfall, mkuu wa kampuni hiyo alisema "wajukuu wa Ghandi wameiona picha hiyo na wameonyesha kuvutiwa nayo” Haikuwa wazi ni ndugu gani kampuni hiyo ilikuwa ikiwazungumzia hasa.
Alisema ana matumaini bidhaa hiyo itawavutia watu “kujifunza zaidi kuhusu Mahatma Gandhi na mbinu zake za kutotumia vurugu. Wahindi wengi hapa Marekani wameridhishwa na hatua hiyo.
Chanzo: BBC
Imetafsiriwa na mwandishi wetu
Sunday, 4 January 2015
MSHUKIWA WA MAUAJI AHISIWA KUWA TANZANIA
Almahri anasakwa kwa kuhusika na kifo cha Nadine |
Msako wa kimataifa unafanyika baada ya mwanamke mmoja kukutwa amekufa kwenye chumba cha hoteli.
Mwili wa Nadine Aburas, mwenye umri wa miaka 28, ulikutwa na wafanyakazi katika hoteli ya Future Inn hotel huko Cardiff siku ya mwaka mpya.
Polisi wa South Wales walisema wanaichukulia kesi hiyo kuwa ya mauaji na wanataka kumsaka mshukiwa Sammy Almahri, raia wa Marekani kutoka mjini New York.
Almahri, mwenye umri wa miaka 44, ambaye ana majeraha yanayoonekana usoni, alikuwa na “urafiki” na Bi Aburas na inaaminiwa kwamba sasa yupo Tanzania, jeshi hilo la polisi limesema.
Mshukiwa huyo aliingia katika hoteli hiyo ya Future Inn hotel huko Cardiff Bay, Desemba 30 kabla Bi Aburas kuwasili kwenye saa tatu usiku.
Halafu aliondoka kwenye hoteli hiyo kwenye saa 9 alfajir siku ya Mwaka mpya na kusafiri kwa ndege kutoka uwanja wa ndege wa Heathrow, Uingereza na kuelekea Bahrain saa nne unusu asubuhi.
Mpelelezi wa polisi Paul Hurley alisema Almahri anachukuliwa kuwa mtu "hatari" na "mwenye mengi" alipozungumza na umma kusaidia kumpata.
Alisema: "Hoteli ilikuwa imeshughulika na watu waliokuwa wakisherehekea Krismasi na Mwaka Mpya. Watakuwepo watu waliowaona pamoja, au peke yao, na ninawasihi wajitokeze.
"Wakati bado hatujakamata mtu yeyote, tuna maafisa wanaojaribu kumsaka Sammy Almahri, ambapo sasa tunaamini yupo nchini Tanzania.
"Tumekuwa tukifanya kazi kwa karibu na wafanyakazi wenzetu wa Marekani na maafisa polisi wa Tanzania.
Kutokana na uchunguzi wetu tumegundua Almahri ni mtu anayejiweza sana na uwezo wa kupata fedha nyingi, ambayo inaweza kumsaidia kukwepa mkono wa sheria.
Uchunguzi wa mwili wa marehemu umekamilika lakini sababu ya kifo chake bado hakijathibitishwa.
Familia ya Bi Aburas imetoa rambirambi kwake kwa kusema "mzuri, mchangamfu, wa kipekee na mwenye kipaji".
Katika taarifa walisema: "Alikuwa anapenda sana kusaidia watu na kila mtu alimpenda. Ameacha pengo kubwa kwenye familia yetu na kila mmoja anampenda. Familia imeomba waachwe waomboleze kimya kimya.”
Chanzo: www.uk.news.yahoo.com
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu
Subscribe to:
Posts (Atom)