Friday, 20 February 2015

KIMA ATARAJIWA KUACHIWA URITHI WOTE



Shabista with Chunmun

Wanandoa wa India waliotengwa baada ya familia zao kutoridhishwa na ndoa yao wameamua kuacha mali zao zote kwa kima wao.

Brajesh Srivastava na mkewe Shabista waliiambia idhaa ya Hindi ya BBC kuwa walikuwa "wapweke kwa miaka mingi" kabla ya kumnunua kima huyo aitwaye Chunmun, mwaka 2005 kwa rupia 500 yaani dola 8.

Wanandoa hao, ambao hawana watoto, wanasema wamemlea kama mtoto wao.

Bw Srivastava ni Hindu na mkewe Mwislamu, na ndoa za imani tofauti bado zina utata katika baadhi ya maeneo India.

Brajesh Srivastava and wife Shabista
Bi Srivastava alisema familia zao zote mbili ziliwatenga baada ya ndoa yao na walikuwa wapweke mpaka walipomnunua Chunmun.

"Wakati huo alikuwa mtoto, alikuwa chini ya umri wa mwezi mmoja, na mama yake alikufa kutokana na umeme," alisema.

Humnywisha Chunmun maziwa, matunda na chakula chochote anachopika. Chumba chake kina feni ambacho hutumika wakati wa joto na ‘heater’ wakati wa baridi.

Wednesday, 18 February 2015

BI HARUSI AOLEWA NA MGENI MWALIKWA KWA HASIRA


 Indian bride

Bi harusi mmoja wa India ameolewa na mmoja wa waalikwa katika harusi yake baada ya bwana harusi mtarajiwa kupatwa na kifafa na kuzimia.

Ripoti zilisema bwana harusi huyo mtarajiwa, Jugal Kishore, alikuwa na kifafa na hakumwambia mtarajiwa wake, Indira na familia ya binti huyo.

Wakati Bw Kishore alipopelekwa hospitali, bi harusi huyo mwenye hasira aliamua kutafuta  mume mbadala.

Alimwomba mmoja wa upande wa familia ya shemeji yake, aliyekuwa mwalikwa, kumwoa badala ya mtarajiwa wake. Jambo alilokubali.

Tukio hilo lilitokea mjini Rampur katika jimbo lililo kaskazini mwa India Uttar Pradesh.

Kulingana na gazeti la The Time la India, Bw Kishore, mwenye umri wa miaka 25, alianguka chini mbele ya wageni waalikwa alipotaka tu kumkamata mkono bi harusi wake Indira.

Aliporejea hospitalini, Bw Kishore alimwomba Indira abadili mawazo, akimwambia atabezwa na marafiki na ndugu zake akirudi bila mke, lakini bi harusi huyo alikataa.

Afisa polisi Ram Khiladi aliiambia BBC kuwa awali Bw Kishore na familia yake walikasirishwa na kupeleka malalamiko polisi.

"Lakini kwa kuwa bi harusi huyo kashaolewa, utafanya nini? Familia hizo zimeshatafuta suluhu na wamefuta malalamiko," aliongeza.

Tuesday, 17 February 2015

MTOTO ALBINO AKUTWA KAKATWA MIGUU TANZANIA



Albino boys in Tanzania

Mtoto mdogo albino ambaye hakujulikana alipo tangu siku ya Jumapili amepatikana kaskazini mwa Tanzania, huku miguu yake yote miwili ikiwa imekatwa.

Watu wawili wamekamatwa wakihusishwa na kifo chake.

Awali kulikuwa na hofu kuwa huenda ameuliwa na waganga wa kienyeji wanaopiga ramli.

Polisi walisema Yohana Bahati mwenye umri wa mwaka mmoja alichukuliwa na watu waliovamia nyumba ya mama yake, na kumpiga na panga.

Viungo vya albino, husakwa na waganga wa kienyeji wanaopiga ramli nchini Tanzania.

Nchi hiyo ilipiga marufuku waganga wa kienyeji kuendeleza shughuli zao mwezi Desemba katika jaribio la kuzuia mashambulio na utekajinyara.

Baba wa mtoto huyo, aliyekuwa karibu wakati wa shambulio hilo, anahojiwa, mkuu wa polisi wa kanda hiyo Joseph Konyo aliliambia shirika la habari la AFP.




OBASANJO WA NIGERIA ANG'ATUKA CHAMANI



Former Nigerian president Olusegun Obasanjo

Aliyekuwa rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo ameng’atuka kutoka chama tawala cha People's Democratic Party (PDP) kabla ya uchaguzi wa Machi 28, akirarua kadi yake ya chama hadharani.

Bw Obasanjo alikuwa mkosoaji mkali wa Rais Goodluck Jonathan, anayetaka kugombea tena kwenye uchaguzi kupitia chama cha PDP.

Bw Jonathan anakabiliwa na changamoto kubwa kutoka mgombea wa upinzani Muhammadu Buhari.

Uchaguzi huo, uliotakiwa kufanyika Februari 14, uliahirishwa kutokana na sababu za kiusalama.

Mchambuzi wa BBC Nigeria alisema uamuzi wa Bw Obasanjo ni pigo kubwa kwa chama cha PDP, ikionyesha mgawanyiko ulioukikumba chama hicho huku ikipambana kuongeza muda wake wa uongozi wa miaka 15.

Monday, 16 February 2015

WASHTAKIWA KWA MAUAJI YA COPENHAGEN



 

Polisi wa Denmark imewashutumu watu wawili kwa kuwasaidia watu wenye silaha walioua watu wawili katika mashambulio tofauti Copenhagen.

Mshukiwa huyo mwenye silaha, aliyetajwa na vyombo vya habari vya Denmark kuwa Omar El-Hussein, alipigwa risasi na polisi na kufa baada ya kushambulia mjadala wa uhuru wa kusema na sinagogi.

Mkurugenzi wa filamu na mlinzi wa sinagogi waliuawa huku watano wakijeruhiwa.

Watu hao wawili wanashtakiwa kwa kutoa na kutupa silaha, na pia kuwasaidia watu hao wenye silaha kujificha.

Wakili wa upande wa utetezi alisema watu hao wamekana mashtaka hayo.

Sunday, 15 February 2015

LADY JAYDEE AFUNGUKA, AVUNJA NDOA NA GADNER

 

Mwanamuziki nyota wa kike nchini, Lady Jaydee jana aliamua kuwaburudisha mashabiki wake kwa staili ya kipekee; kuzungumzia kuvunjika kwa ndoa yake na Gadner Habash.

Kwa muda mrefu kumekuwa na minong’ono kuwa wawili hao wametengana, lakini hakuna aliyekuwa tayari kuweka wazi kuhusu suala hilo.

Hata hivyo, jana, Jaydee, ambaye jina lake halisi ni Judith Wambura aliamua kutoa ya moyoni, akisema kuwa kwa sasa ametengana rasmi na mtangazaji wa kituo cha redio cha E-fm cha jijini Dar es Salaam.

Jaydee ambaye wakati mwingine huitwa ‘Jide’, kwa wiki moja sasa ameamua kujibu maswali mbalimbali kutoka kwa mashabiki wake kwenye mitandao ya kijamii.

Kati ya maswali aliyoulizwa na mashabiki wake ni kama ni kweli ametengana na mumewe na ni sababu za kutengana.

Kupitia ukurasa wake wa instagram, mwanadada huyo alisema: “Nimemvumilia vya kutosha, kuhusiana na tabia zisizokuwa na nidhamu wala heshima ya ndoa na sasa imefika kikomo.”

Friday, 13 February 2015

MADEREVA WANAWAKE SAUDIA 'WAACHIWA HURU'



Loujain al-Hathloul at wheel of her car

Wanawake wawili kutoka Saudi Arabia waliotiwa kizuizini kwa kukiuka amri ya ufalme wa nchi hiyo kwa kuwepo madereva wanawake wameachiliwa huru baada ya zaidi ya siku 70, ripoti zinasema.

Loujain al-Hathloul, mwenye umri wa miaka 25, alikamatwa baada ya kufanya kampeni ya amri hiyo kupunguzwa makali.

Rafiki yake Maysa al-Amoudi, mwenye umri wa miaka 33, alitiwa kizuizini alipoenda kumsaidia.

Wasiwasi mkubwa uliibuka baada ya kutolewa ripoti kuwa kesi yao itahamishwa katika mahakama ya kigaidi.

Saudi Arabia ni nchi pekee kukataza wanawake kuendesha gari.

Japo si kinyume cha sheria kwa mwanamke kuendesha, ni wanaume tu wanaopewa leseni ya udereva – na wanawake wanaoendesha gari hadharani wako hatarini kupewa faini na kukamatwa na polisi.

Wanawake wa Saudi Arabia walianzisha mfululizo wa kampeni – ikiwemo kwenye mitandao ya kijamii – wakitaka sheria hiyo ilegezwe.

Bi Hathloul alikamatwa Desemba 1 baada ya kujaribu kuendesha gari ndani ya ufalme huo kutoka nchi jirani ya United Arab Emirates (UAE).

Bi al-Amoudi, mwandishi wa habari wa UAE, naye pia alikamatwa alipowasili mpakani kumwuunga mkono Bi Hathloul.