Sunday, 15 February 2015

LADY JAYDEE AFUNGUKA, AVUNJA NDOA NA GADNER

 

Mwanamuziki nyota wa kike nchini, Lady Jaydee jana aliamua kuwaburudisha mashabiki wake kwa staili ya kipekee; kuzungumzia kuvunjika kwa ndoa yake na Gadner Habash.

Kwa muda mrefu kumekuwa na minong’ono kuwa wawili hao wametengana, lakini hakuna aliyekuwa tayari kuweka wazi kuhusu suala hilo.

Hata hivyo, jana, Jaydee, ambaye jina lake halisi ni Judith Wambura aliamua kutoa ya moyoni, akisema kuwa kwa sasa ametengana rasmi na mtangazaji wa kituo cha redio cha E-fm cha jijini Dar es Salaam.

Jaydee ambaye wakati mwingine huitwa ‘Jide’, kwa wiki moja sasa ameamua kujibu maswali mbalimbali kutoka kwa mashabiki wake kwenye mitandao ya kijamii.

Kati ya maswali aliyoulizwa na mashabiki wake ni kama ni kweli ametengana na mumewe na ni sababu za kutengana.

Kupitia ukurasa wake wa instagram, mwanadada huyo alisema: “Nimemvumilia vya kutosha, kuhusiana na tabia zisizokuwa na nidhamu wala heshima ya ndoa na sasa imefika kikomo.”


Msanii huyo anayemiliki Machozi Band, alibadili picha ya wasifu ya mtandao huo na kuweka jicho linalotoa machozi na kidole kikivuja damu.

Alisema kuwa yeye na Gadner hawajaachana kama ambavyo watu wanasema isipokuwa yeye ndiye aliyeamua kumuacha mwanamume huyo.

Hata hivyo, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Gadner alisema: “Sina comment katika hilo.”

Aliongeza kusema: “Aliyezungumza ni mtu mzima na amefanya juhudi kuzungumza alichozungumza. Ku-comment kwa kupinga au kukubali ni kuzidharau juhudi zake.”

Meneja wa mwanamuziki huyo maarufu kama Rapa Wakazi, alisema kuwa kilichozungumzwa na kuandikwa na mwanamuziki huyo ni kati ya mwimbaji huyo na mashabiki wake, hivyo hakuna cha kuongeza.

Meneja huyo alisema ingawa mwanamuziki huyo hakuhusisha uongozi wakati anaandika, lakini hayo ni mawazo yake na yabaki kuwa hivyo.

Wakati Habash akisema hayo, Jide aliamua kufunguka na kusisitiza kuwa hatarudi nyuma kwa uamuzi aliouchukua. Na hii ni sehemu ya majibu yake:

Swali: Tumesikia umeachana na mumeo kweli au si kweli?

Jide: Hatujaachana, nimemuacha.

Swali: Kwa nini umeachana/ umemuacha mumeo?

Jide: Nimeamua kutokana na kuwa ndoa inatakiwa iwe na maelewano, furaha, amani na upendo… ila kwa bahati mbaya vyote hivyo havikuwepo, sikuwa tayari kuendelea kuishi kwa maumivu huku nikipretend (kwa maigizo), ili kuridhisha jamii.

Swali: Huoni kama umejishushia heshima kuachana na mumeo?

Jide: Sioni hivyo ila naona nilikuwa najishushia heshima zaidi kuishi na mume asiye na heshima… amekuwa akiwapa mademu (vimada) magari yangu na kuyagonga wakati nipo safari, ukiachilia mbali vipigo. Kifupi ilikuwa ndoa ya mateso.

Swali: Baada ya kuachana unatarajia kuolewa tena?

Jide: Ni mapema kujihakikishia kuolewa na mwingine, ila haimaanishi kuwa sitopenda tena. Nahitaji kuwa makini zaidi kuchagua mtu sahihi wa kumpa moyo wangu.

Swali: Uliwezaje kuishi na mume mlevi namna ile?

Jide: Nilidhani angebadilika, nilikuwa natoa nafasi, iliposhindikana nikaona isiwe tabu, kila mtu aubebe mzigo wake. Ukizingatia ananizidi umri miaka mingi, alitakiwa yeye anielekeze zaidi kuliko mimi kumwelekeza maisha mtu mzima.

Swali: Uliwezaje kuondoka? 
Jide: Nilipoamua iwe basi, niliondoka bila kubeba kitu, nikasafiri kwenda Marekani, nikakaa huko mwezi mzima kurefresh (kujiliwaza) na kujipima kama ninaweza kumove on (kuendelea)? Niliporudi Tanzania sikukanyaga tena nyumbani mpaka muda huu ninatype (kuandika) na kupost (kutuma) majibu haya.

Kwa kifupi niliondoka bila kuaga sikuona sababu ya kuaga. Ahsanteni jamani, nafikiri nimejibu yote.

Jay Dee alichomoza kwenye anga za muziki baada ya kurudia kibao cha mwanamuziki nguli, Marijani Shabani cha “Zuwena” ambacho kilimpa umaarufu mkubwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz
 

No comments:

Post a Comment