Saturday, 7 February 2015

ALI KIBA AZUNGUMZIA BIFU LAKE NA DIAMOND



Hatimaye staa wa Bongofleva Ali Kiba amekiri kuwa yuko katika bifu na mwanamuziki mwenzie Diamond Platnumz kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.

Kauli hiyo ya Ali Kiba inapingana na ile ya hivi karibuni iliyowahi kutolewa na Mwenyekiti wa Kamati za bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe alisisitiza kuwa wanamuziki hao hawana tofauti zozote na kwamba ni watu tu ndio wanakuza suala hilo.

Hata hivyo, juzi Ali Kiba aliliambia gazeti hili kuwa ni kweli kuna ugomvi baina yao, huku akisisitiza kwamba tofauti yao ilianza mwaka 2012. Wakati Ali Kiba akifunguka kuhusu bifu hilo hali imekuwa tofauti kwa Diamond ambapo amekaririwa mara kadhaa kuwa hana tofauti yeyote na mwanamuzi huyo ambaye wanatoka mkoa mmoja wa Kigoma na kuunganisha Kundi la Kigoma All Stars. Akizungumza wakati akijibu maswali mbalimbali katika mahojiano maalumu, mwanamuziki huyo pia alielezea mambo mengi kuhusu muziki wake na hii ni sehemu ya mahojiano hayo;

Swali: Nini chanzo cha bifu lako na Diamond?

Ali Kiba: Hakuna kiini kwa sababu nadhani hayo mimi aaah.…Kiukweli haya tuliyamalizaga muda mrefu …Labda watu wahisi kwamba kipindi kile alichonifuta katika wimbo wake (alisema bila kufafanua jina la wimbo) na yeye alivyosema kwamba nimemfuta katika wimbo wangu ‘Single Boy’, mimi sijawahi kurekodi na Diamond katika wimbo wangu hata mmoja na huo niliimba na Lady Jaydee.

Yeye ndiye aliyesema kwamba nilimfuta katika wimbo ule, ila ukweli ni kwamba hatukuwahi kuingia pamoja studio, nilimshauri tufanye wimbo mwingine lakini siyo ule kwa sababu nimeshaimba na Lady Jay Dee.

Swali: Umeshawahi kuwa karibu na Diamond?


Ali Kiba: Hapana yeye ndiyo alishawahi kuwa na ukaribu na mimi.

Swali: Unaweza kufanya kolabo na Diamond?

Ali Kiba: Ngoja nikwambie ukweli, sidhani kama ninaweza kuja kufanya kolabo na Diamond, ila nikipata wimbo ambao nadhani kwamba anastahili kuwapo, kiukweli nitamshirikisha lakini kama hastahili haitawezekana.

Kwa sababu kila wimbo unajielezea, kwa mfano kama mtu anataka kufanya Zouk akimtafuta Stara Thomas itawezekana kwani hayo ndiyo mambo yake, kwa hiyo kama nikitaka kufanya naye wimbo ambao nitaona kwamba unafaa nitamfuata na nitamweleza.

Swali: Utofauti kati yako na Diamond ni upi? 
Ali Kiba: Mimi naimba muziki mzuri na nina ‘hit song’, naye Diamond anaimba ‘hit song’, unaposema mimi sina hit song wakati mimi nina nyimbo nyingi kushinda yeye unakuwa unakosea, tangu nimeanza kuimba ni nyimbo mbili tu hazijawahi kuwa hit ikiwamo ‘My Everything’ na ‘Mali Yangu’ lakini nyingine zote zilivuma tangu nianze kufanya muziki.

Swali: Inasemekana katika Tamasha la TigoMusic kuna hirizi zilionekana Uwanja wa Leaders na wewe na Diamond mnatuhumiwa kuhusika, unalizungumziaje?

Ali Kiba: Yaani Mungu mmoja sina imani hiyo kabisa na mimi naamini Mungu na mambo ya hirizi na mimi ni tofauti. Nadhani watu wanasema hivyo kwa sababu wanadhani kwamba kuna bifu. Binafsi sina bifu na msanii yeyote labda kama wanaweza kuwa na bifu na mimi binafsi simchukii msanii yeyote na sina bifu na yeyote.

Swali: Video yako ya Mwana imezungumziwa na mashabiki kuwa haikuwa na uhalisia. Pia ilikuwa ya kawaida sana, wewe binafsi unalichukuliaje?

Ali Kiba: Video ilivyokuwa ndivyo ilipangwa iwe kwa sababu kila mtu alikuwa amejenga picha itakuwaje kwa hiyo ililazimika kufanya vile kwa kuwa watu walishapanga mpaka gharama kwa kuwa nilikaa muda mrefu pasipo kufanya. Ningefanya kitu ambacho watu walikifikiria kiukweli ingekuwa karaha, nilichozingatia mimi ni kuimba vizuri na kuonyesha fikra za wimbo husika.

Swali: Vipi uliandaa ‘skripti’ ya video au aliamua GodFather kuifanya vile ilivyotengenezwa?

Kiba: Tulikuwa na ‘script’ yetu pia waongozaji wa video walikuwa na yao ambayo walitupatia. Hivyo tukakubaliana nao kwa sababu tulitaka kuleta utofauti na kila kitu kikakaa sawa.

Swali: Ni kweli kwamba una mpango wa kufanya kolabo na Chris Brown?

Ali Kiba: Uwezekano wa kufanya upo kwa sababu kila kitu ni mipango kwa hiyo naweza kufanya kolabo na wasanii wa kimataifa na mashabiki watarajie kufanya hivyo.

Swali: Kwa nini haujafanya video ya Kimasomaso na ulisema video ya Mwana ingefanyika Dar es Salaam kwa nini ulitengenezea Afrika Kusini?

Ali Kiba: Video ya ‘Kimasomaso’ ilishindikana kutokana na muda ulikuwa hautoshi, nilijikuta niko katika mambo mengi sana kwani nilikuwa nimeegemea katika video ya Mwana kwa hiyo nilipokuja kugeuka ikawa ni vigumu.

Nilisema kwamba nyingine ningefanya nje ya hapa lakini kwa ‘Mwana’ sijaelewa kwanini nifanye hapa, tofauti na hiyo nyimbo haikuwa na maana ya Dar es Salaam, maana yake ni mwanamke na mwanamume sikuona sababu ya kufanyia hapa jijini.

Ukitumia neno la Dar es Salaam ni kwa sababu ni jiji lenye changamoto kwa hiyo unapozungumzia hilo ina maana kwamba ni Joharnesburg, Nairobi, Kampala, London majiji ambayo yana changamoto mfano video ya Macmuga nilifanyia Marekani.



Chanzo: mwananchi.co.tz
 

No comments:

Post a Comment