Wednesday, 11 February 2015

WANAWAKE VINARA USAFIRI WA BODABODA



Zinaitwa bodaboda, kule Nigeria wanaziita okadas kwa jina jingine ni pikipiki. Hiki ni chombo cha usafiri ambacho katika miaka ya hivi karibuni kimeiteka miji mingi ya Afrika ikiwamo Tanzania.

Licha ya kutumika katika uhalifu, kusababisha vifo kwa kiasi kikubwa, utafiti  uliofanywa na gazeti hili  katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam ambako kuna matumizi makubwa ya bodaboda ulibaini kuwa usafiri huu unapendwa zaidi na wanawake.

 Dereva wa bodaboda katika maeneo ya Tabata Relini, Ayubu Msigala anasema idadi kubwa ya abiria wake ni wanawake. Anasema wanawake wajawazito pia wanatumia usafiri huo kwa kiasi kikubwa.

“Zamani wanawake walikuwa wanaogopa bodaboda, lakini sasa  hata wajawazito wanatumia zaidi, hawaogopi kama ilivyokuwa zamani,” anasema Msigalla.

 Akizungumzia suala la wanawake kupenda bodaboda, Msigala anasema wanawake waliokuwa wakiziogopa bodaboda sasa ndiyo wanaozipanda kwa wingi huku wanawake wajasiriamali wakiongoza kuzitumia.

Anasema mamalishe, wauza nguo, vocha, hata wafanyakazi wa maofisini wamekuwa wapandaji wakubwa wa bodaboda.


“Hata akina mama wanaokwenda hospitali kupeleka watoto hutumia zaidi usafiri huu ili kuwahi, wakati mwingine naweza kumpakia mama na watoto wake wawili na mzigo,” anasema.

 Hata wajawazito wenye kipato cha chini wameelezwa kuzitumia pindi inapowabidi na wengine zimekuwa zikiwapeka kujifungua.

Hata hivyo, idadi kubwa ya majeruhi katika wodi za MOI na Sewahaji ni wanaume jambo lililozua maswali.

 Suria Mungi, mkazi wa Bunju anasema analazimika kupanda usafiri huo ili kurahisisha shughuli zake.

“Sina uwezo wa kukodi teksi halafu hapohapo nataka kuwahi kazini inanibidi nichukue bodaboda. Cha muhimu namdhibiti asikimbize,” anasema Suria.

Zimegeuka mabasi ya shule

Kutokana na shida ya usafiri, baadhi ya wazazi wameona kuwa usafiri rahisi kwa ajili ya watoto wanaokwenda shule ni bodaboda

 “Hali ya hatari zaidi inayotuogopesha hata sisi waendesha bodaboda wenyewe, ni pale mzazi anapokodi bodaboda kuwapeleka shule watoto wake watatu, kila siku asubuhi na jioni,” anasema  Masawe Mkandemia.

 Zinawadanganya wanafunzi

 Kati ya waendesha bodaboda 10 waliohojiwa, sita kati yao walikiri kuwa wanafunzi wanadanganyika kiurahisi na madereva hao.

“Kwanza unaweza kumpeleka shule bure na kwa fedha tunayopata  ni rahisi kumhonga na akadanganyika,” anasema Mwika Marwa.

Wengine walikiri kuwa sasa wanafunzi wanazitumia ili kuepuka manyanyaso katika mabasi ya abiria.

Bodaboda hazikwepeki

 Tatizo kubwa madereva wengi wana elimu ndogo kwani wengi wao wameishia darasa la saba.

 Kwa mfano, utafiti uliofanywa na  Emmanuel Mwakapasa wakati wa kutimiza taratibu za Shahada ya Uzamili ya Unesi mwaka 2011 katika Chuo cha Sayansi ya Afya na Tiba Muhimbili (Muhas), ilibainika kuwa asilimia 64.8 ya madereva 273 waliohojiwa jijini Dar es Salaam, walikuwa wana elimu ya msingi na wote walikuwa wanaume.

Utafiti huo ulioitwa ‘Mtazamo juu ya matumizi ya kofia ngumu miongoni mwa waendesha bodaboda za biashara jijini Dar es Salaam’ ulibainisha kuwa kundi kubwa la madereva hao ni lile lenye umri kati ya miaka 18 hadi 24.

Kundi hilo ni miongoni mwa asilimia 54 ya watu wasio na ajira nchini wenye umri chini ya miaka 25 katika taifa la 10 duniani kuwa na kundi kubwa la vijana, taasisi isiyo ya kiserikali ya Restless Development, yenye makao yake nchini Uingereza, imebainisha.

Mwananchi lilizungumza na wakazi wa Dar es Salaam ambao ni watumiaji wakubwa wa usafiri huo, pamoja na madereva wa bodaboda. Wengi walikiri kuwa bodaboda ina sura nyingi za kimanufaa kwao licha ya kuwa na upungufu pia.
Kwanza, wasafiri  walisema ni mbadala wa mabasi ya abiria na teksi kutokana na unafuu na uharaka wake wakati madereva walikiri kuwa ni ajira tosha.

Hapo zamani, bodaboda ilitumiwa kama usafiri binafsi, kwa wengine ulitumika kama sehemu ya starehe lakini kwa sasa ongezeko la matumizi ya bodaboda  unatajwa   kusababishwa na kukithiri kwa foleni, ubovu wa barabara na uhaba wa mabasi ya abiria.

Hapa nchini, bodaboda zimekuwa kimbilio  la watu wa aina zote kuanzia wenye kipato cha kati, cha chini, jinsi na rika zote.  Lakini pamoja na hayo, bodaboda zimekuwa kinara wa ajali za barabarani.

 Akitoa taswira halisi ya ajali za bodaboda, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga anasema ajali hizo ni nyingi.

 Kwa mfano, takwimu za mwaka 2008 hadi Oktoba 2014 zinaonyesha kuwa ajali zilizosababishwa na bodaboda zilikuwa 31,498  na katika kipindi hicho hicho vifo 5266 vilitokea.

“Kwa idadi ya ajali hadi Oktoba  mwaka huu tunakwenda vizuri lakini kwa madhara ya vifo na majeruhi bado hali siyo nzuri sana,” anasema Kamanda Mpinga.

 Kwa mfano, kutoka Januari mwaka huu hadi Oktoba, tayari kuna vifo 799 vilivyosababishwa na usafiri huo.

 Mwaka uliokumbwa na jinamizi la bodaboda kwa kiasi kikubwa ni 2013 ambapo vifo 1,098 vilitokea na ajali 6,831.

 Msemaji wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Patrick Mvungi anasema asilimia 55 ya majeruhi katika wodi za MOI na Sewahaji ni za watu waliopata ajali za pikipiki.

 Mwananchi ilifika hadi katika wodi  ya Sewahaji na  kushuhudia wagonjwa wakiwa wamefurika hadi katika korido karibu kabisa na mlango wa kuingilia.

Umaarufu wa bodaboda waongezeka

Licha ya ajali hizo, idadi ya pikipiki zinazosajiliwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga na Majini,(Sumatra),  inaendelea kuongezeka na msemaji wa mamlaka hiyo, David Mziray anasema  idadi ya pikipiki zilizosajiliwa kwa mwaka 2013 hadi Juni 30, 2014 ni 2,254. Pia katika kipindi hicho, zilisajiliwa bajaji 5,041.
Hata hivyo utengenezaji wa bodaboda na uingizaji nchini umefanya vifaa hivyo kuongezeka na hivi karibuni gazeti dada la The Citizen lilibainisha kuwa hadi mwishoni mwa mwaka jana kulikuwa na bodaboda 589, 936 huku asilimia 70 zikisemekana kuwapo Dar es Salaam pekee.

Pia, gazeti hilo lilibainisha kuwa kutoka Januari hadi Oktoba mwaka jana zilikuwapo bodaboda 118, 047 na bajaji 27,000 karibu mara tatu ya usafiri wa daladala.

Uhalisia mwingine unaonyesha kuwa umaarufu wa vyombo hivyo unaendelea kuongezeka na ni bahati nasibu ambazo mara nyingi zinatoa zawadi ya bodaboda.

Kwa mfano Promosheni ya Jishindie Bodaboda kutoka kampuni ya simu za mkononi ya  Vodacom,  Promosheni ya  Weka na Ushinde ambapo washindi walijipatia bodaboda, baiskeli na bajaji kutoka Benki ya NMB na NBC.

Katika Barabara ya Mandela zilizopo ofisi za gazeti hili, ajali tano za bodaboda hutokea kila siku na kati ya hizo, majeruhi hupatikana na wengine kufariki dunia.

 Askari wa Usalama Barabarani kituo cha Tabata Relini, Jackson Watalima anasema ajali za bodaboda  ni nyingi katika eneo hilo na kila siku idadi inaongezeka hasa nyakati za usiku.

 Wauzaji wavuna faida

Kutokana na kukua kwa biashara ya usafiri wa bodaboda wauzaji pia wanazidi kuvuna faida baada ya bei ya vifaa hivyo kupaa licha ya kuongezeka kwa ushindani.

Mfanyabiashara wa pikipiki eneo la Kariakoo, Mussa Mtenguka anasema kuwa biashara kwa sasa imekuwa ya wastani kutokana na kuongezeka kwa wauzaji japo ina faida kubwa kama awali.

“Hizi pikipiki za Kichina tunaziuza kati ya Sh 1.65 milioni hadi Sh1.7 milioni wakati hizi Boxer za India ni Sh2 milioni. Hata hivyo hizi bei ziliongezeka miaka miwili iliyopita kutokana mahitaji kuongezeka, bei hazikuwa hivi,” anasema Mtenguka.

Kwa mujibu wa tovuti ya kampuni ya kutengeneza pikipiki nchini Cruiser Motors Tanzania, ili kutimiza mahitaji yaliyopo mijini na vijijini, wanatarajia kuanzisha uundaji wa vifaa hivyo vyenye asili ya Tanzania ambavyo vitakuwa vikisambazwa ndani ya Kanda ya Afrika Mashariki na Kati.

“Kwa sasa kampuni inazalisha pikipiki 10,000 kwa mwaka na tunaratajia kuongeza uzalishaji huo hadi pikipiki 50, 000,” ilieleza sehemu ya taarifa ya kampuni hiyo yenye kiwanda chake Kiwalani, jijini Dar es Salaam.
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Prosper Ngowi anasema kwa mtazamo wa haraka bodaboda zimesaidia kuongeza ajira, kupunguza upotevu wa muda na vitendo vya wizi miongoni mwa vijana.

Hata hivyo, anasema serikali imechelewa kufanya utafiti wa kina wa kubaini faida na hasara zinazoletwa na bodaboda kabla ya kuendelea kuchochea sera za usafiri huo.

“Mapema tu baada ya usafiri huo kukua kwa kasi na kuanza kuleta ajali nyingi, serikali ilibidi ikae chini na kufanya utafiti, je gharama za kupoteza watu na kuwatibu majeruhi wa ajali za bodaboda zinaendana na faida.

“Hii pia ingesaidia kufahamu kama asilimia kubwa ya bodaboda zinamilikiwa na vijana wenyewe au mapebari wengine ili kutambua ufanisi wa kuwasemehe kodi…serikali haina budi kufanya utafiti huo sasa,” anasema Dk Ngowi.

Dk Ngowi anasema hata kama itabainika zimeleta hasara, serikali haitakiwi kuzizuia na zaidi zifanyike juhudi za kuwaelimisha zaidi madereva hao kufuata sheria na kuwa wastaraabu.

Iwapo utaboreshwa, alisema bodaboda ni usafiri mzuri utakaokuza uchumi mara dufu kwa kuokoa muda na fedha zinazopotea kutokana na foleni.

 Usafiri ghali kwa kilomita

Pamoja na ukweli kwamba bodaboda zinaonekana kurahisisha usafiri jijini hapa na maeneo mengine yasiyofikika na usafiri wa umma nchini, bado bodaboda ni usafiri ghali kwa kilomita kuliko daladala katika barabara zenye usafiri wa uhakika.

Utafiti mdogo uliofanywa na gazeti hili katika mitaa mbalimbali jijini Dar es Salaam ni kwamba kama unatokea External barabara ya Mandela kuelekea Ubungo unahitajika ulipe Sh1,500 hadi Sh2,000 kwa bodaboda wakati kwa daladala ni Sh400 na ni ndani ya kilomita moja na nusu.

Afya

 Katika siku za hivi karibuni, madereva wengi wa bodaboda wameonekana kuvaa miwani za jua na makoti. Ukweli ni kuwa wanaathiriwa kwa kiasi kikubwa na upepo na vumbi.

 Daktari wa Macho katika Hospitali ya Mwananyamala, Agusta Sintale anasema, vumbi na upepo huharibu macho kwa kiasi kikubwa na hasa iwapo dereva wa bodaboda ataendesha kwa miaka miwili mfululizo.
 
Ajira

 Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka anasema hawezi kuzungumza kuhusu pikipiki katika kuzalisha ajira bali alidai kuwa suala hilo ni la kiuchumi zaidi.

Ripoti ya hivi karibuni iliyoandikwa na Benki ya Dunia,(WB) iliweka bayana kuwa usafiri wa bodaboda unarahisisha biashara na ni msaada mkubwa kwa wakazi wanaoishi katika miji yenye msongamano katika nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Hata hivyo, Januari mwaka huu, aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe,  aliiagiza Sumatra kuandaa mikakati ya kuanzishwa kwa benki ya bodaboda ili kuwasaidia wapate mikopo kuboresha uchumi.

“Biashara ya bodaboda  nchini imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika kurahihisha usafirishaji maeneo ya vijijini na kwenye majiji yenye misongamano ya karibu kila kitu” anasema Dk Mwakyembe.

Dk Mwakyembe anasema kutokana na ukweli huo,upo umuhimu mkubwa kuanzisha benki itakayosaidia kutoa mikopo kwa madereva wa boda boda,ili waweze kuboresha uchumi wao.

Chanzo: mwananchi.co.tz



 

No comments:

Post a Comment