Monday, 9 February 2015

MAMBO 5 YANAYOKWAMISHA BIASHARA



Wafanyabiashara wengi hukumbwa na changamoto nyingi katika uendeshaji wa shughuli zao za biashara. Changamoto hizi ndizo zinaweza pia kuwa utofauti wa biashara zinazokua na zile zinazokufa.

Makala hii inachambua mambo muhimu ambayo huwa ni mzigo mzito kwa wajasiriamali hata kufikia hatua ya kuathiri biashara zao, na pia makala hii inaonyesha baadhi ya njia za kukabiliana na changamoto hizo.

1. Mtaji

Kikwazo hiki hujitokeza katika mitazamo mitatu, kwanza wakati wa kutaka kuanzisha biashara, pili wakati biashara imeshaanza ila fedha hazitoshi kuendesha vema, na tatu pale mfanyabiashara anapokusudia kupanua biashara yake. Ili kukabiliana na kikwazo cha mtaji yafuatayo yanaweza kusaidia:-

Kuanza biashara kidogo kidogo: Hii namaanisha kuwa kufikiria namna ambazo unaweza kuanzisha biashara kwa mtaji mdogo na wakati huo huo ukafanya kwa ufanisi. Hii inaweza kwa kuchunguza kwa umakini gharama zisizo za lazima, mambo ambayo unaweza fanya wewe mwenyewe au kusaidia na watu wengine bila kuajiri, pia chunguza aina ya bidhaa ambazo kweli ni za lazima kuanza nazo. Kutunza taarifa za biashara yako kwa ufasaha na kuwa na muundo bora wa uongozi, hii itakusaidia kuwa kutimiza masharti ya benki, na wadau mbalimbali wa sekta ya fedha ambao wanaweza kukuongezea mtaji.

Zingatia pia kuwa na mali zisizohamishika, na pia kuna na mahusiano mazuri na wadau mbalimbali kwani wao wanaweza kuwa vyanzo vya kukupatia mtaji.

2. Muundo wa biashara


Hili limekuwa ni tatizo kwa watu wengi hususani wafanyabiashara wadogo na wa kati. Ni tatizo zaidi kwa kuwa wafanyabiashara wenyewe wengi hawaoni kama ni tatizo, wakitoa visingizio kuwa eti uendeshaji wao wa biashara ndio muundo bora zaidi . Hapa nazungumzia kuwa na biashara ambayo haina mgawanyiko wa majukumu, haina mchanganuo wa biashara, haina utunzaji sahihi wa taarifa, na wala haifuati taratibu za kisheria kama usajili, kuwasilisha taarifa za fedha , kulipa kodi, kuwa na akaunti benki, n.k. Hili ni tatizo kwa kuwa biashara hizo hazijaandaliwa kukua, na hata zinapofanikiwa kukua zinakumbana na ugumu wa kuwa endelevu. Hivyo kuleta ugumu wa kuongeza mtaji kupitia mikopo ya benki na asasi nyingine, ugumu wa kuendeshwa kitaalamu zaidi kwani madaraka yameshikiliwa na mtu mmoja, na ugumu wa kupanua fursa za kibishara kama vile kushirikiana na biashara kubwa zaidi , kushiriki katika kuomba Tenda, n.k.

Na mbaya zaidi inapotokea mmiliki au mmoja wa wamiliki kufariki au kushindwa kuendelea kuendesha biashara, biashara huyumba na hatimaye kufa kwakuwa hakukuwa na muundo unaoeleweka wa uendeshaji wa biashara husika.

Kama haufahamu jinsi ya kuunda muundo imara wa biashara yako, mtafute mtu anayeweza akufanyie kazi hiyo, au jifunze ili uweze kufahamu namna ya kuweka muundo vema. Heshimu taaluma za watu, na omba ushauri inapobidi. Fanya bidii uzungukwe na wafanyakazi unaowaamini na wenye uzoefu na ujuzi wa kile wanachokifanya. Jifunze mambo mengi zaidi kuhusu usimamizi wa biashara, na kuwa macho na changamoto unazokumbana nazo kwani hizo zinakupa mafundisho ya kuboresha biashara yako.

3. Usimamizi wa wafanyakazi

Mambo magumu yanayojitokeza katika usimamizi wa wafanyakazi ni wafanyakazi kukosa uaminifu na kuwa na ufanisi wa chini ya kiwango. Usipoangalia utapata hasara, na hata kupoteza wateja kwani wateja kwa ujumla huja kufuata bidhaa na huduma zako ambazo zinatolewa na hao wafanyakazi.

Kuna namna kadhaa za kupambana na tatizo hili. Hatua ya kwanza ni wewe mwenyewe kujenga muundo mzuri wa biashara yako ikiwa pamoja na mpango bora wa kifedha ili uweze kulipa wafanyakazi kwa kiwango cha kuridhisha. Ukishakuwa na mpango mzuri wa kifedha maana yake utaweza pia kuajiri watu wanaokidhi kiwango cha kazi unachotaka wafanye, na sio basi tuu ili mradi watu. Kingine unachoweza kufanya ni kuweka muundo maalum wa utendaji katika biashara yako ili kila mfanyakazi afahamu majukumu yake, anaripoti kwa nani, anahitajika kufanya nini, na kwa kiwango gani. Fungua mianya ya mawasiliano ili kujua matatizo wanayokumbana nayo watendaji wako.

Zaidi sana hakikisha watendaji wanao ujuzi na vifaa vinavyoendana na kazi wafanyayo na ufanisi unaotakikana.

Tumia muda kujua tabia za watu unaotaka kuwaajiri, na endelea kuwa karibu nao na kujifunza kuhusu wao ili uweze kujua namna ya kuwachochea pia utendaji wao. Je, unafanya nini kuwachochea waonyeshe bidii na ubunifu. Je, unaruhusu ubunifu ? Je unawaheshimu na kuwathamini watendaji wako?

4. Ubia

Mara nyingi imekuwa ni ngumu kwa watu wengi kufanya biashara kwa kushirikiana na watu wengine, hususani katika hatua za mwanzo za uanzishwaji wa biashara. Vikwazo vinavyojitokeza katika kufanya ubia na watu wengine ni vingi kama vile : Kutokupata watu waaminifu, Kupata watu wasio na moyo wa kujitolea kufanya shughuli za biashara yenu, kupata watu wanaokuwa wagumu kujitolea mtaji wa kutosha kufanya biashara yenu, na zaidi sana, kupata watu wasio na mwelekeo au mtazamo wa mbali wa kijasiriamali, yaani wao wanawaza faida ya haraka haraka, na kwamba kwao biashara ni sehemu ya kuingiza fedha ya ziada tuu ya leo au kesho.

Usiwe na haraka ya kufanya ubia na mtu, msome tabia yake vema. Jifunze pia kuhusu mtazamo wake wa maisha, na biashara, fahamu kuhusu familia yake na majukumu yake ya kijamii. Kisha pima uone kama majukumu yake, tabia yake, mtazamo wake , na imani yake vinaendana na biashara mnayotaka kuanzisha au malengo na mtazamo wako wa baadae wa biashara husika. Chunguza vyote kwa umakini, na usijidanganye, kumbuka dalili ya mvua ni mawingu, waweza jua mapema kama mtu atakuwa mshirika bora kwako mapema kabla hamjaanza kufanya biashara pamoja.

Usichanganye urafiki, udugu au kujuana kwa namna nyingine na biashara yako. Anaweza kweli kuwa rafiki mzuri kwako, lakini biashara yenu inahitaji mtaji wa kutosha na kujituma kwa mhusika, kitu ambacho huyo rafiki yako hatoweza kufanya kutokana na majukumu yake ya kifamilia.

5. Ushindani wa kibiashara

Kikwazo hiki kinajitokeza kwa namna nyingi ikiwa ni pamoja na uwezekano mkubwa wa kuigwa na watu wengine. Ni kawaida watu kutaka kuiga kama ufanyavyo hasa pale unapoonekana kufanikiwa. Kikwazo hiki hujitokeza pia katika namna ya bidhaa mpya zinazokuja kuwa mbadala wa bidhaa yako, na hata kuwa katika bei ya chini zaidi. Kumbuka siku hizi wateja wengi wana mianya mingi ya kupata taarifa za bidhaa mbalimbali na bei zake toka kwa wauzaji mbalimbali. Hivyo kufanya biashara kwa mazoea tuu kwakuwa una 'jina' kubwa haitoshi.

Jifunze kusoma alama za nyakati, kwa kufuatilia habari zaidi zinazohusiana na aina ya biashara unayofanya, wafahamu wapinzani wako vema, soma taarifa pia za mambo ya kijamii, kimataifa, siasa na hata burudani, vyote hivi vinaweza kukupa mwelekeo wa mambo katika jamii hivyo kujituma zaidi na wewe kubadilika. Kujifunza kwako kuhusu wapinzani au wafanyabiashara wengine hakutokuwa na maana kama hautokuwa na muundo imara wa uendeshaji wa biashara yako, na pia ukaboresha ufanisi wako siku hadi siku.

Pia jitahidi kujenga uwezo wa kuitofautisha biashara yako na biashara nyingine , na kuwa na kitu cha kipekee ambacho wengi hawawezi kuiga, na hata kama wataiga, hawatoweza kufikia kiwango chako.

Tunakutakia mafanikio makubwa kupitia biashara yako.

Chanzo: wavuti.com

No comments:

Post a Comment