Saturday, 13 September 2014

SHAIRI - TAHADHARI NA MATONGE

 
HUONI WANAVYOKULA,       KWA UKWASI NA MADAHA
KWAO NI KAMA KULALA,     HAWAIPENDI KARAHA
SIWAONE NI MAFALA,          NI WENYE NYINGI STAHA
NA UNAPOKULA NAO,         JIKANYE HAYO MATONGE 

SIJIONE UMJUZI,                   KWA MATONGEYO MAKUBWA
UKADHANI HAWAWEZI,        KULA NA WAO UBWABWA 
WASTAHABU ULEZI,             LAINI USIO MWIBA
NA UNAPOKULA NAO,         JIKANYE HAYO MATONGE

VIJITI YAO ASILI,                     HUKO WALIKOZALIWA
WALA NAVYO KWELI KWELI, KAMA KUTAFUNA MIWA
WAVITUMIA KWA WALI,         NA HATA KWENYE HALUWA
NA UNAPOKULA NAO,           JIKANYE HAYO MATONGE

VIMACHO VYAO VIDOGO,     NDIVYO MNAVYOWASEMA
HAWAUONI MUHOGO,            NA WAKILA WANAHEMA
MAMBO MDOGO MDOGO,     NDIYO UFIKE SALAMA
NA UNAPOKULA NAO,           JIKANYE HAYO MATONGE
Shairi hili limeandikwa na Wazir Khamsin

IMANI ZAIDI KWA BI KENYATTA KULIKO WANASIASA

Bi Margaret Kenyatta, mke wa Rais Uhuru Kenyatta

Wakenya wana imani zaidi na mke wa Rais wao (First Lady) Margaret Kenyatta kuliko mtu yeyote anayejulikana nchini Kenya, kulingana na utafiti mpya uliofanywa na Ipsos Synovate.

Umma nao unamwamini zaidi kuliko bunge, mahakama, baraza la mawaziri na serikali za mitaa.

Asilimia 39 ya walioulizwa kwenye utafiti huo uliofanywa mwezi Agosti na kutolewa siku ya Alhamis wameelezea “kuwa na imani sana” na mama huyo, asilimia 73 wakiwa wanavutiwa naye huku 15% tu wakiwa na hisia hasi dhidi yake.

Idadi ya Wakenya walioonyesha kutovutiwa na Bi Kenyatta pia ni ndogo kuliko utafiti wowote aliofanyiwa mtu maarufu.

Rais Uhuru Kenyatta ameongoza miongoni mwa wanasiasa, asilimia 43 ya waliohojiwa wakionyesha kuwa na imani naye.

Hata hivyo idadi hiyo imeshuka kwa 10 kutoka Novemba mwaka jana alipokuwa na asilimia 53 ya walio na imani naye.

Imani kwa Naibu Rais nayo imeshuka kutoka asilimia 48 hadi 38 katika kipindi sawa na Rais Kenyatta.

Asilimia 28 imeonyesha kuwa na imani na kiongozi wa Cord, Raila Odinga na 20% kwa mkuu wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka
Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Cord Raila Odinga


Tom Wolf ambaye alikusanya maoni ya watu kutoka Ipsos Synovate alisema kushuka kwa asilimia za Rais na Naibu wake ni kupungua kwa mcheche wa baada ya uchaguzi.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wamehoji takwimu hizo, wakisema mfumo uliotumika hauna uwiano.

“Nafasi ya Rais na naibu wake kwa sasa haziwezi kulinganishwa. Rais hapa Kenya bila shaka ataongoza tu akishindanishwa na wapinzani au wenzake, “ alisema Prof Fredrick Wanyama.

Aliongeza kuwa maoni ya watu “yalikusudia kuonyesha kuwa viongozi wa upinzani hawawajibiki”.

Dr Adams Oloo alisema utafiti huo uliofanywa ni sawa na kulinganisha tufani na chungwa.

Chanzo: Daily Nation, Kenya                 
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu


WANAOWAHUDUMIA WAGONJWA WA EBOLA WAGOMA




Wafanyakazi wa hospitali wameanza mgomo kwenye wodi ya Ebola ilojazana katika hospitali kuu ya wilaya mashariki mwa Sierra Leone palipoathirika zaidi na ugonjwa huo kwa madai kuwa serikali inashindwa kuwalipa.

Hadi wafanyakazi 80 walijazana kwenye mlango wa kuingilia wa hospitali hiyo siku ya Ijumaa, na kusabababisha shughuli zote kusimama.

Wafanyakazi hao walifanya mgomo kwa amani lakini walikuwa tafrani.

Tukio hilo limetokea baada ya migomo mengine kufanyika kwenye hospitali hiyohiyo kwa madai ya mazingira mabovu ya kufanyia kazi, maambukizi miongoni mwao na malipo wanayopewa haiendani na hatari wanayokabiliana nayo.

Wafanyakazi hao waliajiriwa kitaifa kuongeza idadi yao katika hospitali ya serikali ya Kenema, ambapo wanafanyia kazi kwenye hema ‘maalum lililotengwa’ wakati wauguzi na wafanyakazi wengine wakiwa na kazi ya kutibu wagonjwa, kusafisha vyombo vilivyochafuka, kusafisha vinyesi, matapishi, damu na kuondosha pamoja na kuzika maiti.

"Nilianza kufanya kazi hapa mwezi mmoja uliopita na hatujalipwa kitu wiki ya pili sasa," Umaru, anayeshughulika na usafi, aliiambia Al Jazeera. "Tumemwambia kila mmoja agome mpaka tulipwe marupurupu yetu."

Vifo vya wafanyakazi                              

Wafanyakazi waliobaki walisema zaidi ya wauguzi 38 na madaktari wameambukizwa na kufariki dunia katika eneo hilo tangu mlipuko wa ugonjwa huo kutokea, miongoni mwao ni daktari maarufu Sheik Umar Khan.

Wafanyakazi wanaosaidia kuhudumia wagonjwa wa Ebola wanatakiwa kulipwa dola 110 kwa wiki lakini wamekuwa wakifanya kazi bure huko Kenema katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Eneo hilo maalum la kuhudumia wagonjwa wa Ebola limezidiwa likiwa na takriban wagonjwa 80 wakitibiwa na wapya wakiwasili kila siku.


ARSENAL Vs MAN CITY: VIKOSI KAMILI NA REKODI ZAO

Straika aliyekosa namba katika kikosi cha Van Gaal kwa msimu huu, Danny Welbeck, anajiandaa kucheza mechi yake ya kwanza ya ligi kuu chini ya mzee Arsene Wenger pale The Gunners watakapoikaribisha Man City katika uwanja wa Emirates.


Staa huyo mwenye umri wa miaka 23 alijiunga na klabu ya Arsenal akitokea katika kikosi cha Man U kwa ada ya uhamisho wa euro milioni 20 (Tsh bil 44), katika tarehe ya mwisho wa dirisha la usajili wa majira ya joto na upo uwezekano mkubwa wa kupewa nafasi ya kikosi cha kwanza mara baada ya Giroud kuumia.

baadhi ya mastaa wa The Gunners watakaocheza katika mechi dhidi ya Man City
Baadhi ya mastaa wa The Gunners watakaocheza katika mechi dhidi ya Man City

Wakati huohuo kiungo wao, Aaron Ramsey anasumbuliwa na majeraha ya kifundo cha mguu ‘ankle’ aliyoyapata akiwa na kikosi cha timu ya taifa cha Wales katika mechi dhidi ya Andorra Jumanne iliyopita hivyo hatokuwepo katika mechi ya ligi kuu siku ya Jumamosi dhidi ya Man City.

'Possible line up' baada ya usajili wa Alex Sanchez
‘Possible line up’ baada ya usajili wa Alex Sanchez

Mastaa wengine wa The Gunners wanaotarajiwa kucheza dhidi ya Man City baada ya kutoka katika majeraha ni pamoja na Abou Diaby, Kieran Gibbs, Mikel Arteta, na Mesut Ozil.

Kwa upande wa Man City, Straika msumbufu , Stevan Jovetic anasumbuliwa na maumivu ya misuli ya paja ‘hamstring’ inasemekana anaweza akakosa mechi hiyo lakini mtandao wa klabu bado haujatoa taarifa za kutosha juu ya maendeleo ya staa huyo.

Jovetic mpaka sasa ametupia magoli mawili kambani katika mechi tatu alizozicheza mpaka sasa, na magoli hayo aliyapata katika mchezo dhidi ya Liverpool katika ushindi wa magoli 3-1.

Staa mwingine wa Man City ambaye yupo katika hatihati ya kucheza katika mchezo huo wa Jumamosi ni Fernando anayesumbuliwa na majeraha ya ‘groin’aliyoyapata katika mchezo wa ligi kuu walioupoteza kwa kichapo cha bao 1-0 na Stoke City.

Pia Pablo Zabaleta anaweza akaanzia benchi mara baada ya kupona majeraha aliyoyapata katika mechi ya kirafiki dhidi ya Ujerumani akiwa na kikosi chake cha Argentina.

katika mechi ya ligi kuu msimu uliopita wa 2013/14, Arsenal walipigwa magoli 6-3 na Man City katika mwendelezo wa rekodi mbovu za mzee Wenger dhidi ya timu zilizopo katika 'big-5'
Katika mechi ya ligi kuu msimu uliopita wa 2013/14, Arsenal walipigwa magoli 6-3 na Man City katika mwendelezo wa rekodi mbovu za mzee Wenger dhidi ya timu zilizopo katika ‘big-5′

Ikumbukwe mara ya mwisho kwa klabu hizi kukutana ilikuwa ni katika mchezo wa ‘Ngao ya jamii’ ambapo The Gunners waliwachapa Man City magoli 3-0 yaliyofungwa na Santi Cazorla, Ramsey na Giroud.

Tusubiri tuone kama The Gunners wataendeleza ubabe wao kwa Man City au kama kibao kitageukia upande wao.

Chanzo: taarifa.co.tz

UGONJWA MPYA WAINGIA TANZANIA

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt Seif Rashid
Hatimaye Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetoa matokeo ya sampuli zilizopelekwa Nairobi nchini Kenya, kubaini chanzo cha utata wa kifo cha Bertha Boniphace (25) aliyekuwa amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Geita, mkoani hapa baada ya kuenea uvumi kuwa alikuwa akiumwa ugonjwa wa ebola.

Akizungumza kuhusu matokeo ya sampuli hizo jana, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Geita, Dk Adam Sijaona alisema matokeo kutoka Nairobi yanaonyesha Bertha hakuwa na ugonjwa wa ebola bali alikuwa anaumwa ugonjwa unaojulikana kitaalamu kama Chikungunya Viral Hemorrhagic Fever (VHF).

“Matokeo yametoka rasmi hakuuawa na ugonjwa wa ebola kama tulivyozungumza awali ila unaelekea kwenye kundi la ebola, dengue na homa ya bonde la ufa. Ni ugonjwa wa kitropiki. Kitaalamu tunauita Arthropod borne virus, unaenezwa na mbu aina ya Aedes Aegyti,” alisema Dk Sijaona na kuongeza:

“Aina hii ya mbu ni wachache na wanapatikana kwenye maeneo yenye unyevuvyevu kama wengine, Bertha alikuwa akifanya kazi maeneo ya madini Kata ya Katoro ambako mbu hao ni rahisi kupatikana.

“Lakini siyo ugonjwa wa kawaida nchini ingawa siyo hatari kama virusi vya ebola. Ni kesi chache za aina hii kwa sababu tangu apatikane huyu hadi leo hakuna mgonjwa mwingine aliyeripotiwa, ila watu wanatakiwa kuchukua tahadhari.”

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dk Joseph Kisala alisema ugonjwa huo ni mpya nchini na kwamba, haujazoeleka barani Afrika na kama ilivyo kwa magonjwa ya VHF hauna tiba maalumu.

Chanzo: Mwananchi, Tanzania

CUBA KUPELEKA MADAKTARI MAENEO YA EBOLA

Baby tested for Ebola
Katika baadhi ya nchi kuna madakatari wachache sana wa kutibu maradhi ya Ebola
Cuba inapeleka wafanyakazi wa kitabibu kusaidia kupambana na mlipuko wa Ebola Afrika magharibi, maafisa wamesema.

Madaktari, wauguzi na wataalamu wa kudhibiti maambukizi wataenda Sierra Leone mwezi Oktoba na kukaa kwa muda wa miezi sita.

Tangazo hilo limetolewa huku shirika la Afya Duniani WHO likisema wagonjwa wapya wanaongezeka haraka, hivyo kushindwa kuhimili idadi kubwa ya walioathirika.

Zaidi ya watu 2,400 wamefariki dunia kutokana na virusi hivyo miezi ya karibuni na takriban watu 4,700 wameambukizwa.

Idadi kubwa ya waliokufa ni kutoka Liberia, Sierra Leone na Guinea.

Maafisa wa WHO wamesema idadi ya watu waliofariki dunia bila shaka ni kubwa zaidi kuliko inavyokadiriwa sasa.

Nchini Liberia wataalamu walisema hakuna hata kitanda kimoja kilichobaki cha kuwalaza wagonjwa wa Ebola.


Friday, 12 September 2014

WASHUKIWA WALIOMPIGA RISASI MALALA MBARONI

Pakistani schoolgirl activist Malala Yousafzai poses for pictures during a photo opportunity at the United Nations in the Manhattan borough of New York on 18 August 2014.
Malala alikuwa na umri wa miaka 15 tu alipopigwa risasi mara tatu kichwani
Wapiganaji wanaoshukiwa kumpiga risasi mwanaharakati Malala Yousafzai wamekamatwa, jeshi la Pakistan limesema.

Binti huyo alipigwa risasi kichwani na wapiganaji wa Kitaleban mwezi Oktoba 2012 kutokana na kampeni yake kuhusu elimu kwa watoto wa kike.

Walipanda kwenye basi lake la shule kaskazini-magharibi mwa Pakistan na kufyatua risasi, katika shambulio ambalo liliwajeruhi pia marafiki zake wawili.

Tangu wakati huo anaendelea vizuri kutokana na shambulio hilo, lililoishtua dunia na kumpa umaarufu ulimwenguni kote.

Alitajwa kama mmoja wenye ushawishi mkubwa duniani na jarida la Time mwaka 2013, aliteuliwa kupata tuzo ya Amani ya Nobel na amezindua hivi karibuni kitabu cha maisha yake.

Msemaji wa jeshi Jenerali Asim Bajwa alisema wanachama 10 wa kundi la TTP wamekamatwa katika harakati za pamoja za kijeshi na Pakistan, polisi na majasusi.

Jenerali Bajwa aliongeza kuwa, kundi hilo limekuwa likifanya kazi chini ya maelekezo ya Mullah Fazlullah,mkuu wa Taliban ya Pakistan.

Malala Yousafzai, aliyekuwa na umri wa miaka 15 wakati wa shambulio hilo, tayari alipata umaarufu kwa kudai haki za elimu na watoto nchini Pakistan.

Chanzo: BBC
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu


OSCAR PISTORIUS AKUTWA NA HATIA



 
Mwanariadha wa Afrika Kusini Oscar Pistorius amekutwa na hatia kwa kosa la kuua bila kukusudia (Culpable homicide) baada ya jaji kuona amemwuua mpenzi wake kwa bahati mbaya.

Jaji Thokozile Masipa amesema alikuwa “mzembe” alipofyatua risasi iliyopitia mlango wa chooni lakini akiwa “anaamini kulikuwa na mtu asiyemjua”.

Alisema upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kuwa alikuwa na nia ya kumwuua Reeva Steenkamp.

Pia alikutwa na hatia ya kushikilia silaha kwa uzembe iliyofyatuka kwenye mgahawa

Mwandishi wa BBC Andrew Harding, akiwa mahakamani, alisema kufuatia uamuzi huo, Pistorius alikaa tu, akafuta uso wake na kusogea kidogo kwa mbele.

Hakukuwa na hisia zozote mahakamani kwasababu kila mmoja alijua uamuzi gani ungetolewa, mwandishi huyo aliongeza.

Uamuzi huo unaashiria mshtakiwa huyo atakabiliwa na kifungo cha mpaka miaka 15, japo wataalamu wa kisheria wanasema huenda ikawa miaka saba hadi kumi baada ya hukumu kutolewa katika wiki chache zijazo.

TOTO TUNDU - UJAMBAZI WA KUJADILIANA?

Vimbwanga vya WhatsApp

MTOTO 'AZAMIA' NDEGE ZANZIBAR

Uwanja wa ndege Zanzibar

Polisi Zanzibar wameanza uchunguzi kubaini mazingira ya safari tata ya mtoto Karine Godfrey aliyesafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar kwa ndege bila tiketi wala kugundulika.

Mtoto huyo, Karine au Jenipher Godfrey anayesoma darasa la tatu katika Shule ya Msingi Jitihada, Dar es Salaam alionekana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Septemba Mosi saa 11.30 jioni, akieleza kuwa aliingia Zanzibar kwa ndege ambayo hata hivyo, haikufahamika mara moja ni ya shirika gani.

Alikutwa uwanjani hapo akijiandaa kuondoka kwenda mahali asipopajua.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis alisema mbali ya kushangazwa na mazingira ya safari ya mtoto huyo, polisi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar wanalifanyia kazi suala hilo.

“Ni jambo la kushangaza. Tunajiuliza, huyu mtoto alifikaje katika ndege bila ya kuwa na tiketi wala taarifa zozote kuelezea safari yake na je, huko Dar es Salaam aliondokaje hadi kuingia katika ndege bila ya hivyo vitu, sielewi ilikuwaje.

“Ina maana hakufanyiwa hata ukaguzi kama ilivyo kawaida kwa wasafiri. Tunalichunguza hili, huu ni uzembe wa hali ya juu ulioonyeshwa na wahusika wote wa viwanja vya ndege,” alisema.

Chanzo: Mwananchi, Tanzania


Thursday, 11 September 2014

MARUFUKU KUMWITA MWANAO 'MESSI'



Lionel Messi with his partner and son (Reuters)
Lionel Messi akiwa na mpenzi wake na mwanawe
Wazazi wanaotaka kuwaita watoto wao wa kiume jina kama la mchezaji nyota wa Barcelona Lionel Messi sasa watakatazwa kufanywa hivyo katika eneo alipozaliwa mchezaji huo.

Serikali ya Argentina imeamua kuzuia watoto wengine zaidi kuitwa ‘Messi’ kwa madai kuwa hali imevuka mipaka.

Hayo yote yameibuka baada ya Hector Varela kutoka Rio Negro kusini mwa Argentina alipopambana na mamlaka ili kuruhusiwa kumwita mtoto wake wa kiume Messi Daniel Varela.

Hili lilikuwa tukio la kwanza la namna hiyo kutokea nchini humo

Kulingana na gazeti la Hispania Marca, mkurugenzi wa usajili wa majina katika jimbo la Santa Fe, Gonzallo Carrillo, alisema Messi kwa sasa limepigwa marufuku kutumika kama jina la mwanzo.

Sasa ni “kinyume cha sheria”, lilisema gazeti hilo, katika njia ya kuondosha mchanganyiko.

Kuhusu jina la mwanawe, Varela alisema: “Mimi ni baba yake Messi. Watu wengi wamewapa watoto wao wa kiume jina la Lionel wakimaanisha Messi, lakini hili liko wazi zaidi”.

Aliomba ruhusa maalum kutoka serikalini, bila kujua kuwa mwanawe alikuwa ndio wa kwanza Argentina na lingeleta vurumai.

Hatimaye, mwanawe wa kiume alifanikiwa kusajiliwa kama “Messi Daniel Varela'.

Mapema mwaka huu, taasisi ya kuwashughulikia wanyama Catalonia ilitoa takwimu zilizopendekeza kuwa paka na mbwa 701 eneo hilo wamepewa majina ya nyota huyo wa soka.

Chanzo: yahoo sport
Imetafsiriwa na Mwandishi wetu

PISTORIUS AFUTIWA MASHTAKA YA MAUAJI


Jaji katika kesi ya Oscar Pistorius imemfutia mashtaka ya mauaji, lakini ameacha kutoa hukumu ya kosa la kuua bila kukusudia (culpable homicide) kwa mwanariadha huyo mpaka siku ya Ijumaa

Jaji Thokozile Masipa alisema waendesha mashtaka hawakutoa ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa alidhamiria kumwuua mpenzi wake Reeva Steenkamp, na kusababisha machozi kumtoka mkimbiaji huyo wa Olimpiki wa mbio fupi.

Lakini alisema alifanya uzembe. Bw Pistorius alisema alidhani kulikuwa na mtu asiyemfahamu  chooni kwake.

Kabla ya kuahirisha kesi hiyo, jaji huyo alisema mtu makini asingefyatua risasi

Mwandishi wa BBC Andrew Harding , aliyekuwa mahakamani mjini Pretoria, alisema jaji huyo anatarajiwa kutoa uamuzi wa kuua bila kukusudia.

Awali, Jaji Masipa alimwelezea Bw Pistorius kama shahidi anayekwepa lakini haimaanishi kuwa ana hatia.

Akimfutia mashatka ya mauaji, alisema asingeona mtu anayemwuua nyuma ya mlango wa chooni.

Mkimbiaji huyo wa Afrika kusini alikana kumwuua Bi Steenkamp baada ya mfarakano siku ya Valentine mwaka jana, akisema amempiga risasi kwa bahati mbaya.

Bw Pistorius, mwenye umri wa miaka 27, amekana mashtaka yote yanayomkabili, ikiwemo kufaytua risasi hadharani na kumiliki risasi kinyume cha sheria.


MUIGIZAJI MSHIRIKA WA JAMES BOND AFARIKI DUNIA

Muigizaji Richard Kiel - aliyecheza kama mwovu mwenye meno ya bati maarufu kama Jaws katika filamu za James Bond - amefariki dunia California akiwa na umri wa miaka 74.

Msanii huyo maarufu wa Marekani, aliyeigiza kwenye filamu ya The Spy Who Loved Me mwaka 1977 na Moonraker mwaka 1979,aliaga dunia katika hospitali ya Fresno siku ya Jumatano.

Msemaji wa Kituo cha Matibabu cha Saint Agnes amethibitisha kifo cha Kieli, lakini hakusema sababu.

Muigizaji huyo mwenye urefu wa mita 2.18 pia aliigiza kwenye filamu ya vichekesho ya Happy Gilmore, ambapo muigizaji mkuu alikuwa Adam Sandler mwaka 1996.

 Kiel alianza kuwika kwenye uigizaji katika miaka ya 50.

Alipata umaarufu sana kwa jina la Jaws akiigiza na Roger Moore mwenye jina la 007.

 Sir Roger alisema "amehuzunishwa mno" kutokana na kifo cha muigizaji mwenzake.

"Tulikuwa pamoja kwenye kipindi kimoja cha redio wiki moja tu iliyopita," alisema muigizaji huyo maarufu wa Bond, akiongeza "siwezi kuhimili taarifa hii".


MASKHARA MENGINE SIYO KABISAAAA

Vimbwanga vya WhatsApp

UAMUZI WA OSCAR PISTORIUS WAANZA KUTOLEWA



 
Jaji kwenye kesi ya Oscar Pistorius ameanza kutoa uamuzi wake dhidi ya mwanariadha huyo, mchakato unaoweza kuchukua saa tele.

Mwanariadha huyo anakabiliwa na miaka 25 gerezani iwapo atakutwa na hatia ya mauaji ya kupanga.

Anakana kumwuua mpenzi wake kwa makusudi Reeva Steenkamp siku ya Valentine mwaka jana, akisema alidhani kulikuwa na mtu asiyemfahamu kaingia nyumbani kwake.

Jaji huyo anaweza akamhukumu kwa kosa la kuua bila kukusudia, ambapo atapata kifungo cha muda mrefu jela. .

Bw Pistorius, mwenye umri wa miaka 27, amekana kwa makosa yote yanayomkabili, ikiwemo makosa mawili ya kufyatua risasi hadharani na kumiliki silaha kinyume cha sheria.

Jaji Thokosile Masipa alianza kwa kuelezea makosa yanayomkabili mwanariadha huyo na kurudia ushahidi alioutoa, akisoma taratibu na kwa umakini.

Baada ya hapo alianza kusoma kwa ufupi kuhusu kesi hiyo.


Chanzo: BBC