Shafii Dauda ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Azania jijini Dar es Salaam, anamkumbuka Asanterabi kama mwanafunzi mwenye akili aliyefanya vizuri sana katika masomo yake ya kumaliza kidato cha nne.
Shafii, ambaye sasa ni miongoni mwa watangazaji na wachambuzi maarufu wa
mchezo wa soka hapa nchini alikuwa kidato cha kwanza wakati Malima alikuwa kidato cha nne.
Akili ile ya Malima imemfikisha nchini Marekani ambako sasa amefanya ugunduzi wa kidude chenye saizi ya pini ndogo (milimita 0.250) kinachoweza kubaini magonjwa ya kuambukiza, kansa na moyo katika hatua ya awali kabisa.
Mtafiti wa Kisayansi
Ugunduzi huu, utakapofika mwisho wake, unaweza kuokoa maisha ya watu wengi duniani. Fikiria tu kwamba unakuwa na kifaa ambacho mojawapo ya magonjwa hayo yakikuanza unaubaini mapema na kwenda kutibiwa.
Mamilioni ya watu wataokolewa maisha yao na kijana huyu wa Kitanzania.
“Siku zote nimekuwa na ndoto za kugundua kitu ambacho kitaweza kuokoa maisha ya watu. Baba yangu alifariki kwa ugonjwa wa moyo ambao ungegundulika mapema kama kungekuwa na kifaa kama hiki.
“Kwa sasa sitaweza kuokoa maisha ya baba yangu lakini ninaweza kuokoa maisha ya wazazi au watoto wa watu wengine kutokana na ugunduzi huu nilioufanya. Nafurahi kwamba ndoto yangu imetimia.
“Kansa, baadhi ya magonjwa ya kuambukizwa na magonjwa ya moyo huwa yanachelewa sana kugundulika. Watu wengi hupoteza maisha, na kwa nchi zilizoendelea hutumia pesa nyingi sana kuwatibu waathirika.
“Kifaa nilichogundua ni kidude cha ukubwa wa pini (0.250mm) kinachoweza kupima na kugundua hayo magonjwa mapema. Ili, yaweze kutibika kirahisi, kuokoa maisha na kupunguza gharama,” anasema
Asanterabi katika mazungumzo yake na Raia Mwema yaliyofanyika kwa njia ya mtandao juzi Jumatatu.
Asanterabi ni mtoto wa aliyepata kuwa waziri wa fedha wa Tanzania, Profesa Kighoma Ali Malima, aliyefariki dunia Agosti 6, 1995 jijini London, Uingereza, katika mojawapo ya vifo vya kushtusha katika historia ya Tanzania.
Kifaa alichokigundia kijana huyu wa Kitanzania kinafahamika kwa jina la Biolom na ugunduzi huu aliufanya akishirikiana na wanafunzi wenzake wawili wa Chuo Kikuu cha Northeastern kilichopo Boston; Cihan Yilmaz na Jaydev Upponi.
Pamoja na udogo wake, kipini hicho kina jumla ya maeneo manne –yote yenye kazi maalumu, na ubunifu huo tayari umetambuliwa na Serikali ya Marekani.
Katika mazungumzo yake na vyombo vya habari vya Marekani, Asanterabi alipata kusema kwamba vifaa vingi vya kisasa hubaini magonjwa; kwa mfano kansa, katika wakati ambapo ni vigumu mtu kupata tiba na kupona.
“Kazi yetu hii itakapokamilika, tutaweza kubaini magonjwa haraka zaidi na mapema zaidi na hivyo watu watapata tiba mapema na kuokoa maisha.
“Nchini kwangu (Tanzania), akinamama wengi hufariki dunia kwa sababu ya kuugua ugonjwa wa kansa ya kizazi, kifaa hiki kitaweza kusaidia watu wengi kupona kutoka katika matatizo yao,” alisema.
Kidude hicho ni kidogo sana kwa umbo na namuuliza kama wameamua iwapo mtu anaweza kukinunua na kubaki nacho nyumbani akijitazama mwenyewe au ni lazima aende hospitali.
“Dhamira yetu hapo ni kipimo kitumike mtu akienda hospitali au kliniki (for annual check-up). Lakini japokuwa kinafanya kazi, kupata ruhusa kwa kukiingiza kama pini ni vigumu. Tunafanya vipimo (test) kwa kupima damu iliyotoka kwa mgonjwa,” anasema.
Elimu yake